TCCIA wakaribisha wawekezaji Tanzania
Muktasari:
Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Paul Koyi amesema kufanya biashara kwa uadilifu,uwazi na kulipa kodi kwa wakati kutakuza maendeleo ya Tanzania na kuiwezesha Serikali kuwafikishia wananchi huduma muhimu.
Dar es Salaam. Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Paul Koyi amesema kufanya biashara kwa uadilifu,uwazi na kulipa kodi kwa wakati kutakuza maendeleo ya Tanzania na kuiwezesha Serikali kuwafikishia wananchi huduma muhimu.
Kauli hiyo ameitoa jana Juni 10,2021 wakati akisaini makubaliano ya kufanya kazi na Jukwaa la wawekezaji kutoka Afrika Kusini wanaofanya shughuli zao hapa nchini(SABF).
Koyi amesema kwakuwa TCCIA inatengeneza mazingira wezeshi kwa wawekezaji kutoka nje lakini wana wajibu wa kufanya kazi nao na kubadilishana uzoefu ikiwemo kulipa kodi na kujenga baadhi ya huduma kwa jamii ya Tanzania.
“Mfano hapa mmesikia Kampuni ya Geita Aglo Ashanti Maining ilikuwa inaongoza kwa kulipa kodi kwa mwaka uliopita na wamekuwa wakitoa huduma muhimu ya kujenga shule, kusaidia kilimo ni jambo zuri na inaonesha tunapokutana hivi tunabadilishana uzoefu,”amesema.
Naye Rais wa SABF Manish Thakral amesema amefurahi kuingia kwenye ushirikiano na TCCIA na watatumia fursa hiyo kuyakaribisha majukwaa mengine kwakuwa mazingira ya uwekezaji hapa nchini ni mazuri.
Amesema kwa muda mrefu walikuwa wanazungumza pamoja na TCCIA kuona namna wanavyoweza kufanya biashara kwa ushirikiano.