Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Teknolojia ya simu janja inavyoliza wengi

Dar es Salaam. Wakati teknolojia ikizidi kukua na kurahisha mambo mbalimbali, maendeleo hayo yamekuwa mwiba kwenye baadhi ya sekta za biashara na hata ajira za watu.

Miongoni mwa vitu ambavyo vimekuwa havikwepeki kwa sasa ni matumizi ya simu janja (smart phones) ambazo kila kukicha zinaongezewa uwezo wa kiteknolojia na kufanya vitu ambavyo awali vilikuwa vinafanywa kama biashara kutoweka.

Simu za mkononi zimeondoa au kupunguza biashara ya kalenda, tochi, saa, redio ndogo kwani vitu vyote hivyo vinapatikana kwenye simu hata zile za bei ya chini kabisa.

Ujio wa ‘smart phones’ umechangia kwa kiasi kikubwa kuondoa biashara ya` internet café’ (sehemu za kupata huduma ya mtandao kwa kompyuta) ambayo hapo awali ilikuwa imeshika kasi maeneo ya mijini.

Miaka 20 iliyopita ilikuwa ukitaka ukitaka kutuma na kusoma barua pepe kupitia anuani yako ilikuwa lazima uende kwenye` internet café’, ulipie ndipo uunganishwe kutumia huduma hiyo lakini kwa sasa kila mwenye simu janja anaweza kupata huduma hiyo.

Kilio kimekwenda pia kwa watoa huduma za ‘stationary’ (biashara ya vifaa vya maofisini) ambako kulikuwa na biashara ya kutoa ‘photocopy’, ‘scanning’ na ‘typing’.

Akizungumza na Mwananchi, Hanifa Mbonde alisema kadiri siku zinavyokwenda wateja wanaofika kwenye duka lake kuhitaji huduma hizo wanapungua ikilinganishwa na ilivyokuwa hapo awali.

“Nimefanya kazi kwenye stationary mbalimbali kwa miaka tisa sasa, hali inabadilika kila siku, baadhi ya huduma zilizokuwa zinahitaji kompyuta hatuzitoi kama ilivyokuwa hapo awali.

Watu walikuwa wanakuja kuchapa barua au nyaraka hiyo kitu imepungua mno hata kutoa `copy’ (kudurufu) labda uwe jirani na ofisi za serikali, shule au chuo,” alisema Hanifa.

Uhalisia wa alichokielezea Hanifa unaonekana kwenye tekinolojia iliyoko kwenye simu kama ya kusaidia kudurufu nyaraka na kuandika taarifa ambazo hizo zote humuwezesha mtu kujihudumia mwenyewe na hata kutuma nyaraka bila kuziweka kwenye mfumo wa karatasi.

Ukuaji huu wa teknolojia umechangia pia kurahisisha mawasiliano, awali barua ndio ilikuwa njia kuu ya mawasiliano kwa walio mbali sasa hivi unaweza kupiga simu na kutuma ujumbe kwa mtu aliye ndani au nje ya nchi, kutuma barua pepe.

Waliokuwa wakiishi kwa kutegemea kupiga picha mitaani nao wameathiriwa kwa kiasi fulani na ujio wa simu janja, haimlazimishi mtu kutegemea kupigwa picha kwani kamera zilizopo kwenye simu zimetengenezwa na uwezo wa kupiga picha na kuzihifadhi kwa kumbukumbu.

Ule utaratibu wa kupiga picha kisha kusubiri isafishwe kwa siku mbili hadi tatu ndio uiweke kwenye bahasha umtumie mtu mkoani sasa hivi haupo picha inapigwa kwenye simu na kwa kutumia tekinilojia iliyoko kwenye simu au mitandao ya kijamii kama Whatsapp, Instagram, Telegram inatumwa ndani ya muda mfupi.

Mkazi wa Keko Machungwa jijini Dar es Salaam, Andrew Kilumanga alisema amelazimika kuachana na kazi ya kupiga picha kutokana na kupungua kwa kiasi kikubwa kwa wahitaji wa huduma hiyo.

“Upigaji picha mitaani ndio kazi nimeifanya kwa muda mrefu na nilikuwa na studio kabisa ila nimeshindwa kuendelea nayo si biashara inayolipa tena. Siku hizi kila mtu ana simu wanazitumia kupiga picha na kutumiana,” alisema Kilumanga.

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimeamua kwenda na kasi ya ukuaji wa teknolojia mbalimbali zinazohusisha simu za mkononi na kuzitumia katika kurahisisha utoaji wa huduma.

Hivi karibuni umetangazwa utaratibu mpya wa tiketi mtandao, ambapo kwa kupitia simu janja msafiri sasa anaweza kuchagua gari analotaka kupanda na kukata tiketi akiwa mahali popote.

Hatua hii inakwenda kupunguza adha ya wapiga debe na kwa upande mwingine itaongeza ugumu wa maisha kwa vijana ambao kazi yao ilikuwa kukatisha tiketi na wale waliokuwa wakilipwa chochote kulingana na idadi ya abiria wanaowapelekea kwenye ofisi ya basi husika.

Akizungumzia hilo, Salome Masinde, ambaye anaishi Chamazi jijini Dar es Salam anasema ukuaji wa teknolojia unazidi kuwapunguzia vijana shughuli za kujiingizia vipato hivyo ni muhimu kwao kuumiza vichwa kuendeana na kasi hiyo ya ukuaji.

Kabla ya hilo zimeshuhudiwa huduma nyingine kadhaa zikirahisishwa kupitia simu ya mkononi mfano manunuzi ya bili za umme wa luku, malipo ya bili za maji, malipo ya ving’amuzi na tozo mbalimbali za serikali, malipo ya kodi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na huduma nyingine nyingi.