Tesla kuja na gari la umeme lenye kasi zaidi

Gari  Model S Plaid lililoingia sokoni Juni mwaka 2021

Muktasari:

  • Gari hiyo ya Roadster 2.0, inalotarajiwa kuwa na mwendokasi wa kilometa 402 kwa saa (250mph), ikiwa ni kasi kubwa kuliko magari yote yaliyowahi kutengenezwa na kampuni hiyo.

Dar es Salaam. Kampuni maarufu ya magari ya umeme (Tesla) imeanza utengenezaji wa toleo jipya la gari aina ya Roadster 2.0 kwa mwaka huu 2024. 

Gari hiyo ya Roadster 2.0, inalotarajiwa kuwa na mwendokasi wa kilometa 402 kwa saa (250mph), ikiwa ni kasi kubwa kuliko magari yote yaliyowahi kutengenezwa na kampuni hiyo.

Tesla imesema gari hilo litakuwa zaidi ya toleo la Model S Plaid lililopo sokoni tangu Juni mwaka 2021, likiwa na mwendokasi wa kilometa 321.8 kwa saa (200mph). 

Kwa mujibu wa taarifa ya mtandao wa kimataifa wa ElectricalSuv, maandalizi ya ujio wa gari hilo yalianza mwaka 2017, huku mmiliki wa kampuni hiyo, Elon Musk, akisema anakusudia kufanya mageuzi ya utengenezaji wa gari hilo la Roadster 2.0. 

“Gari hili lina kasi zaidi kuwahi kutengenezwa, litakuwa na mwendokasi wa kilometa 1.6 kwa kila baada ya sekunde 8.9 hatua itakayoifanya  kuwa na kasi zaidi ya rekodi ya sekunde tisa iliyopo sasa,” alinukuliwa Musk na vyombo vya habari.

Magari ya Tesla

Tesla imetimiza takribani miaka 15 tangu ilipoanza utengenezaji wa magari ya umeme Februari mwaka 2008. Uzalishaji uliokuwa sanjari na betri na vifaa maalum vya kuvuna na kutunza umeme wa jua.

Kwa mujibu wa tovuti ya Tesla,  Musk alianza kuwekeza katika kampuni hiyo mwaka 2004 kabla ya kuwa mkurugenzi mtendaji (CEO) mwaka 2008. Magari yote ya alitengeneza ya kuchaji chini ya dakika 30

Gari la kwanza kutengenezwa na kampuni hiyo lilikuwa ni Roadster Februari mwaka 2008, lenye uwezo wa kuhifadhi nishati ya umeme kwa umbali wa kilomita 394 kabla ya toleo la pili Model S mwaka 2012, umbali wa kilomita 426 na Model X SUV, umbali wa kilomita 580 iliyozinduliwa Mwaka 2015.

Kwa mujibu wa Business insider, toleo la kwanza liliuza magari 2,450 kwa thamani ya dola 109,000 hadi mwaka 2012 ikiwa ni kinyume na matarajio ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Elon Mask. 

Pia kuna Model 3 Sedan ya mwaka 2017 yenye uwezo kutembea kilometa 568 kabla ya kuchajiwa tena. Lina uwezo wa kujiendesha lenyewe pamoja na maboresho ya mfumo wa mtandao.

Toleo la Model Y Crossover mwaka 2020 liliboreshwa zaidi ya Model X. Licha ya umbali wa kilomita 525, gari hilo lina teknolojia ya kujiendesha lenyewe. Pia lina mwendokasi wa kilometa 97 kwa sekunde 5.3.

Kuanzia Juni mwaka 2021, Tesla imeendelea kuuza toleo jipya la Model S Plaid linalofanya vizuri sokoni. Sifa kubwa ya gari hilo ina nguvu, imara na kasi kubwa ikiwa na thamani ya dola 135,990 za Marekani.

Picha ni toleo la Model S Plaid lililoingia sokoni Juni mwaka 2021.