TFS kugawa miche 200,000 ya mbao na matunda Sengerema
Baadhi ya wakazi wa mji wa Sengerema wakipokea miche ya miti aina mbalimbali ya matunda na mbao inayotolewa bila malipo na Wakala wa Huduma ya Misitu (TFS) Wilaya ya Sengerema ikiwa ni sehemu ya maadhisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika. Picha na Daniel Makaka
Muktasari:
Idadi hiyo ya miche itakayogharimu zaidi ya Sh26 milioni ni utekelezaji wa mikakati na mipango ya TFS Wilaya ya Sengerema kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.
Sengerema. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza umeadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika kwa kugawa bure zaidi ya miche 200, 000 ya aina mbalimbali ya miti kwa wananchi, taasisi binafsi na za umma kuhimiza tabia ya kupanda miti kama sehemu ya uhifadhi wa mazingira.
Idadi hiyo ya miche itakayogharimu zaidi ya Sh26 milioni ni utekelezaji wa mikakati na mipango ya TFS Wilaya ya Sengerema kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.
Akigawa miche zaidi ya 10,000 kwa wananchi kwa ajili ya kupandwa kwenye mitaa na maeneo ya taasisi za umma kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru, Mhifadhi wa Misitu Wilayani Sengerema, James Aloyce amesema hadi sasa, zaidi ya miche 50,000 imetolewa na kupandwa maeneo mbalimbali wilayani humo.
‘’Katika mikakati hiyo, TFS imegawa bure kwa wananchi miche ya miti ya matunda na mbao; kwa leo pekee tumegawa na kupanda zaidi ya miche 1,000 katika maeneo mbalimbali ya ofisi na taasisi za umma,’’ amesema James
Meneja wa Benki ya NMB tawi la Sengerema ambayo ni miongoni mwa taasisi zilizopewa miche ya bure, Frank Kilonzo amepongeza uamuzi wa TFS wa kugawa bure miche ya miti kwa wananchi akisema itasaidia siyo tu kuhifadhi mazingira, bali pia kuongeza kipato kupitia biashara ya mbao na matunda miti hiyo itakapokomaa.
"Benki ya NMB tutashirikilikina na Serikali kuhamasisha umma kupanda na kutunza miti kama sehemu ya uhifadhi wa mazingira,’’ amesema Kilonzo
Nkalango Dotto, mmoja wa wakazi wa mji wa Sengerema waliopata miche ya matunda na mbao bila malipo ameshauri ugawaji wa miche hiyo kwa wananchi na hamasa kwa umma kuhusu kupata na kutunza miti kuwa jambo la kuduma kurejesha uoto wa asili ulioharibiwa kwa shughuli za kibinadamu.
Katibu Tawala Wilaya ya Sengerema, Cuthbert Midala ameahidi kuwa uongozi wa Serikali wilayani humo utaendelea kutekeleza mipango na mikakati ya uhifadhi wa mazingira kwa kuhimiza umma kupanda miti na kufanya usafi wa mazingira, kila mtu katika eneo linalomzunguka.
‘’Kila mtu ajihisi kuwiwa kupanda na kutunza angalau miche mitano ya miti ya matunda na mbao katika eneo lake; hii ifanyika bila kujali iwapo unapoishi ni nyumba yako au umepanga kwa sababu suala la mazingira ni letu sote kwa umoja wetu,’’ amesema Midala