Twenzetu Butiama yahitimishwa, Serikali yaahidi kutia mguu
Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Zuwena Farah akisisitiza jambo alipozungumza na wakimbiza baiskeli wakati wa kilele cha mbio za baiskeli za Twenzetu Butiama zilizofanyika kwenye uwanja wa Mwenge mjini Butiama. Picha na Peter Saramba
Muktasari:
Hospitali ya Wilaya ya Butiama imenufaika baada ya kupokea msaada wa vifaa tiba vikiwemo vitanda vya kujifungulia na upasuaji, mashine tatu za hewa ya oksijeni, mashine mbili za kuwahifadhi na kuwatia joto watoto njiti (radiant warmer) na mashine za phototherapy.
Butiama/Mwanza. Mbio za Baiskeli za Tenzetu Butiama zinafanyika kila mwaka kuanzia jijini Dar e Salaam hadi mjini Butiama kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere zimehitimishwa leo Oktoba 14, 2023.
Hafla ya kilele cha mbio hizo imefanyika katika uwanja wa Mwenge mjini Butiama baada ya wakimbiza baiskeli 78 waliosindikizwa kwa muda na nyakati tofauti na wenzao zaidi ya 200, kutumia siku 14 kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 1, 500 kutoka jijini Dar es Salaam hadi Butiama ambako ni nyumbani kwa Hayati Mwalimu Nyerere.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi wa Tehama kutoka kampuni ya Vodacom Tanzania, wadhamini wa mbio za mwaka huu, Athumani Mlinga amesema mbio hizo zilizopita katika wilaya 20 za mikoa 10 nchini zimetumika kutoa ujumbe kuhimiza jamii kuhusu falsafa ya Mwalimu Nyerere ya kuhifadhi mazingira na vita umaskini, maradhi na ujinga.
‘’Tunajivunia kuwa sehemu ya mbio za mwaka huu kwa udhamini wa zaidi ya Sh200 milioni kupitia Vodacom Tanzania Foundation. Ushiriki wetu pamoja na wadau wengine umewezesha kupandwa kwa zaidi ya miche 6, 000 ya miti mbalimbali, kutoa msaada wa madawati 610 kwa shule 13 na kambi ya afya iliyowapa fursa zaidi ya watu 2,000 kupima na kupata matibabu bila malipo katika mikoa ya Mwanza na Mara,’’ amesema Mlinga
Pamoja na kurejesha sehemu ya faida kwa jamii, Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Zuwena Farah amesema taasisi hiyo imeamua kuyadhamini mbio hizo kwa sababu zina matokea chanya katika maendeleo ya sekta za elimu, afya na uhifadhi wa mazingira, mambo yaliyokuwa miongoni mwa vipaumbele vya Hayati Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake.
Faida kwa umma
Kambi ya afya iliyoratibiwa na madaktari kutoka taasisi ya Afya Check kwa kushirikiana na wadau wengine ni miongoni mwa faida kwa jamii zilizoambatana na mbio za Baiskeli za Twenzetu Bitiama mwaka huu baada ya watu zaidi ya 2,000 kupata huduma ya vipimo na matibabu bila malipo.
Mkurugenzi wa Afya Check, Dk Isaac Maro amesema kambi ya matibabu katika mikoa ya Mwanza na Mara imeonyesha uwepo wa tatizo la magonjwa yasiyoambukiza miongoni mwa wananchi waliojitokeza huku akitaja tatizo la macho kuongoza katika orodha ya magonjwa yaliyobainika kusumbua wengi.
Hospitali ya Wilaya ya Butiama nayo imenufaika baada ya kupokea msaada wa vifaa tiba vikiwemo vitanda vya kujifungulia na upasuaji, mashine tatu za hewa ya oksijeni, mashine mbili za kuwahifadhi na kuwatia joto watoto njiti (radiant warmer) na mashine za phototherapy.
Mwenyekiti wa wakimbiza Baiskeli mbio za Twenetu Butiama, Gabriel Landa amesema kwa kipindi cha siku 14 walizokimbia kutoka Dar es Salaam hadi Butiama, wamepata fursa ya kuhamasisha jamii kupanda miti huku nao wakishiriki kupanda zaidi ya miche 6,000 katika maeneo mbalimbali za wilaya 20 za mikoa 10 walikopita.
‘’Tumetumia mbio hizi kuhamasisha jamii kushiriki na kufanya mazoezi kama njia ya kuimarisha afya na kukabiliana na maradhi,’’ amesema Landa
Ahadi ya Serikali
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamadunia, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, mgeni rasmi katia hafla ya kilele cha mbio hizo amewapongeza wadau wote waliofanikisha safari ya Twenzetu Butiama mwaka huu huku akiahidi kuwa Serikali kupitia wizara hiyo itakuwa mshiriki muhimu kufanikisha malengo ya mbio hizo ambayo siyo tu ni falsafa aliyoamini Mwalimu Nyerere, bali pia ni miongoni mwa mipango ya Serikali.
"Kuanzia mwakani sisi tutakuwa sehemu ya maandalizi yam bio hizi kwa sababu mbali ya kumuenzi Mwalimu Nyerere, pia zinahusisha suala la mazoezi ya kutunza mwili kiafya, uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya sekta ya elimu; haya ni mambo pia Serikali inayasimamiwa na kuyatekeleza,’’ amesema Msigwa
Ametaja miongoni mwa mambo yatakayosimamiwa kikamilifu na Serikali kuwa ni kuhamasisha ushiriki wa taasisi nyingi na jamii ili kuyafanya mbio za baiskeli za Twenzetu Butiama zilizoanza mwaka 2019 kuwa siyo tu jambo la Kitaifa, bali pia linakuwa na ukubwa unaoakisi nafasi na mchango wa Malimu Nyerere katika ujenzi na maendeleo ya Taifa.
Butiama watoa ya moyoni
John Matiko, mkazi wa mjini Butiama ameshauri kilele cha mbio za baiskeli za Twezetu Butiama kupewa kipaumbele kwa kutopangwa siku moja na kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru.
‘’Kilele cha mbio za biaskeli za kumuenzi Mwalimu Nyerere na kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru ni matukio mawili makubwa yanayobeba historia ya Hayati Baba wa Taifa yanayostahili kila kimoja kuwa na siku yake maalum tofauti na sasa ambapo zote hufanyika Oktoba 14 kila mwaka,’’ amesema Matiko
Akifafanua, Matiko amesema; ‘’Kutenganisha siku hizi kutatoa furs aka viongozi wakuu Kitaifa kushiriki shughuli zote mbili tofauti na sasa ambapo viongozi wengi hushiriki kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru huku kilele cha mbio za baiskeli za kumuenzi Mwalimu Nyerere zikikosa msisimko unaostahili,’’
Hoja hiyo imeungwa mkono na Halima Ramadhani akisema haileti picha nzuri Taifa kukosa hotuba ya viongozi wakuu wa Kitaifa kutokea mjini Butiama siku ya kilele cha mbio za kumuenzi Mwalimu Nyerere zinazofanyika kila mwaka kwenye mji huo, nyumbani kwa muasisi huyo wa Taifa.
‘’Kilele cha tukio lolote linalohusiana na kumbukizi yoyote ya Mwalimu Nyerere inatakiwa kuhusisha viongozi wakuu wa Kitaifa, tena tukio lenyewe linapofanyika Butiama ambako ndiko nyumbani kwa Mwalimu. Serikali kwa kushirikiana na wadau lazima warekebishe kasoro hii ili kuyapa hadhi inayostahili mbio hizi,’’ amesema Halima