TFS yaeleza changamoto za uhifadhi wa mazingira

Baadhi ya makamishna wa uhifadhi na kutoka Tanapa na TFS na washiriki wengine wa kongamano la Wahariri wa Wadau wa Uhifadhi Mazingira na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji  linalofanyika Iringa leo Desemba 19, 2022. 

Muktasari:

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Profesa Dos Santos Silayo amesema wameandaa mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuhifadhi misitu na kupambana na changamoto za uharibifu.

Iringa.  Mahitaji makubwa ya mazao ya miti hasa kwa ajili ya nishati, uchimbaji holela wa madini, kilimo cha kuhamahama, uvamizi kwa ajili ya makazi vimetajwa kuwa changamoto kubwa katika uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza katika Kongamano la Wahariri na Wadau wa Uhifadhi, Mazingira na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji, Mtendaji Mkuu wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo amesema wameandaa mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuhifadhi misitu huyo.

Amesema mahitaji makubwa ya nishati ikiwamo kuni na mkaa imekuwa ikisababisha uharibifu mkubwa wa misitu.

Amesisitiza kuwepo kwa nishati mbadala itakayosadia uhifadhi wa mazingira hasa mazao ya miti.

Profesa Silayo amefafanua kuwa tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 73 ya uharibifu wa misitu zinatokana na shughuli za kilimo.

Alikumbushia mwaka 1976 wakati wa Azimio la Iringa lililokuwa linaitwa Siasa ni Kilimo, umuhimu wa uhifadhi wa misitu ulitajwa kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa maji.

Hata hivyo amesisitiza kuwa wakati wa Uhuru, Tanzania ilikuwa na misitu 11 iliyohifadhiwa lakini sasa imeongezeka hadi kufikia 24, ukiwemo Msitu wa Hifadhi wa Saohill.

Profesa Silayo amesema wanaendelea kutoa elimu kwa jamii na mikakati mbalimbali ya kusaidia kuwepo kwa uhifadhi wa mazingira.

“Wapo watu wanaamini kwamba kuchoma moto hovyo ni kuwasiliana na Mungu, lakini mwaka huu wamechoma na mvua haijanyesha, mvua ikionyesha imani hiyo huwa inaendelea,” amesema Profesa Silayo.