Waandishi waitaka Serikali kuchukua uamuzi mgumu kuokoa mazingira

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Fillip Mpango (wa kwanza kushoto) akiwa kweneye Kongamano la Wahariri wa Wadau wa Uhifadhi Mazingira na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji  linalofanyika Iringa leo Desemba 19, 2022.

Muktasari:

Wakati uharibifu wa mazingira ukitajwa kuwa kwa kiwango cha juu huku Mto Ruaha Mkuu kwa siku 130 sasa, Serikali imetakiwa kufanya maamuzi magumu kuokoa hali hiyo.

Iringa. Serikali imetakiwa kufanya uamuzi mgumu ili kuokoa chanzo cha maji cha Bonde la Ihefu lililovamiwa na wawekezaji wakubwa wanaochepusha maji hayo kwenye mashamba yao.

Uchepushaji huo wa maji unadaiwa kuwa chanzo kikubwa cha kukauka kwa Mto Ruaha Mkuu unaotegemewa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kuzalisha umeme kwenye mabwawa ikiwamo Mtera, Kidatu na Mwalimu Nyerere.

Akizungumza katika Kongamano la Wahariri wa Wadau wa Uhifadhi Mazingira na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji leo Desemba 19, Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na Taarifa (MECIRA), Habibu Mchange amesema Tanzania ipo katika hatua mbaya ya uharibifu wa mazingira.

Mchange amesema hali hiyo ndiyo ambayo imechangia vyanzo vingi vya maji kukaua.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na Taarifa (MECIRA), Habibu Machange akizungumza wakati wa Kongamano la Wahariri wa Wadau wa Uhifadhi Mazingira na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji  linalofanyika Iringa leo Desemba 19, 2022.

Amesema kupitia ripoti ya mazingira, asilimia 16 ya ardhi ya Tanzania ni jangwa huku asilimia 63 ikiwa imeharibiwa.

“Mto Ruaha, Malagarasi, Ruvu, Ruvuma na mingine mingi kama hatua za haraka hazitachukuliwa tutavuna mabua.

“Leo ni siku ya 130 mto Ruaha hautiririshi maji, sisi wanahabari hatutakuachia wewe jukumu la mazingira, tutakunywa sumu kwa ajili ya mazingira.”

Amesema, Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wanao uwezo mkubwa wa kusababisha maji ya Mto Ruaha kutiririka mwaka mzima tofauti na hali ilivyo sasa.

Awali, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema inasikitisha kuona kwamba uharibifu wa mazingira ni wa kiwango cha juu huku zikiwepo familia 12 zinazojinufaisha kupitia Bonde la Ihefu. 

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile akizungumza wakati wa Kongamano la Wahariri wa Wadau wa Uhifadhi Mazingira na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji  linalofanyika Iringa leo Desemba 19, 2022.

Amesema wakati wakulima wakiendela kulima, wafugaji wanaingiza mifugo yao huku wakikandamiza ardhi na kusababisha uharibifu.

Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Wahariri wa Wadau wa Uhifadhi Mazingira na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji linalofanyika Iringa leo Desemba 19, 2022.

Ameshauri mambo mawili kufanyika, moja ikiwa kuondoa familia hizo na mbili kujenga tuta kubwa litakalozuia wakulima na wafugaji kuingia na kutumia maji ya bonde la Ihefu.