Tigo wajitenga na sakata la kuvuja taarifa za Lissu
Dar es Salaam. Kampuni ya Honora Tanzania Public Limited Company ("TIGO") imejitenga na taarifa za kuvujisha taarifa za simu za Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu, ikisema kampuni mama ya sasa ya Tigo haikuwa mmiliki wake wakati tukio lililoripotiwa.
Taarifa hiyo inatokana na kesi inayoendelea nchini Uingereza kati ya Kampuni ya Millicom iliyokuwa ikimiliki Tigo na aliyekuwa mfanyakazi wake, Michael Clifford ambaye sasa amefukuzwa kazi.
Kwa mujibu wa Gazeti la The Guardian la Uingereza la Septemba 24, 2024, Clifford aliwasilisha maelezo yake katika mahakama ya London kuwa, chanzo cha kufukuzwa kwake ni kutoa ripoti ya jinsi kampuni hiyo ilivyotoa taarifa za mawasiliano ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu.
Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa kwenye gari lake alipokuwa akielekea kwenye makazi yake baada ya kuhudhuria vikao vya Bunge jijini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa la Honora Tanzania Public Limited Company leo Septemba 26, 2024 imeleza kutambua taarifa ya kesi inayoendelea nchini Uingereza ya ajira katika mahakama ya London inayomhusisha mfanyakazi wa zamani wa Millicom, kampuni mama ya Tigo hadi mwaka 2022.
“Kampuni mama ya sasa ya Tigo haikuwa mmiliki wake wakati tukio lililoripotiwa lilipotokea,” imesema taarifa hiyo.
Imesema japo hawawezi kutoa maoni kuhusu undani wa kesi hiyo kwa kuwa hawahusiki moja kwa moja, bali wanahakikisha ulinzi wa taarifa za wateja wao.
“Tunataka kuwahakikishia wateja wetu na wadau wetu kwamba kulinda data zao binafsi kwa kuzingatia sheria na kanuni za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bado ni kipaumbele chetu kikuu,” imesema taarifa hiyo.”