Tisa wachukua fomu CCM kugombea uspika

Msaidizi Mkuu Idara ya Oganaizesheni CCM Taifa, Solom Itunda akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Muktasari:

Wanachama tisa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamechukua fomu za kuomba kuteuliwa kukiwakilisha Chama hicho kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania.

Dodoma. Wanachama tisa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamechukua fomu za kuomba kuteuliwa kukiwakilisha Chama hicho kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Januari 10, 2022 na Msaidizi Mkuu Idara ya Oganaizesheni CCM Taifa, Solomon Itunda wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

“Mtakumbuka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilitoa ratiba kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi juu ya mchakato wa kumpata mgombea wa chama atakayegombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania”amesema

Amesema kwa upande wa Ofisi ya chama Dodoma aliyejitokeza ni Dk Simon Ngatunga, Tumsifu Mwasamale, Merkion Ndofi, Dk Tulia Ackson, Godwin Kunambi na Abwene kajula.

Wengine ni Patrick Lubano, Stephen Masele na Hamidu Chamani kutoka ofisi ndogo Dar es salaam ambapo kwa upande wa Zanzibar hakuna aliyejitokeza kuchukua fomu.

Amesema ratiba imeanza leo na kutarajiwa kumalizika Januari 15, 2022 ambapo limeendeshwa kwenye ofisi za Makao makuu ya chama (Dodoma), Ofisi ndogo Dar es Salaam na Ofisi kuu Zanzibar.