Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TLS yawasihi viongozi kukaa kimya kilichotokea Oktoba 29

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi akizungumza leo Jumatatu, Februari 2, 2026, wakati akiwasilisha salamu za TLS katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini 2026, yanayofanyika jijini Dodoma 

Muktasari:

  • Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimetaka itafutwe namna bora na shirikishi, yenye kuaminika na wote, kumaliza tatizo lililopo, na kwamba msingi wa kufanikisha hilo uwe ukweli, haki, uwazi na uwajibikaji.

Dar es Salaam. Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, amewasihi viongozi wa umma, pale ambapo hakuna ulazima wa kuzungumza, wakae kimya badala ya kuongea mambo yanayotonesha mioyo ya wananchi kuhusu matukio ya Oktoba 29 mwaka jana.

Sambamba na hilo, Mwabukusi ametaka itafutwe namna bora na shirikishi, yenye kuaminika na wote, kumaliza tatizo lililopo, na kwamba msingi wa kufanikisha hilo uwe ukweli, haki, uwazi na uwajibikaji.

Oktoba 29 mwaka jana, kulitokea maandamano yaliyozaa vurugu na kusababisha vifo vya raia, uharibifu wa mali za watu binafsi na za umma. Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan ameshaunda tume kuchunguza tukio hilo, na mwezi huu inamaliza kazi yake na kuwasilisha ripoti.

Mwabukusi ameeleza hayo leo, Jumatatu, Februari 2, 2026, alipozungumza wakati wa hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria na kuanza kwa Mwaka wa Mahakama 2026, jijini Dodoma, ambayo Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, alikuwa mgeni rasmi.

Ameeleza TLS inatambua yaliyojitokeza kabla, wakati na baada ya uchaguzi, na kwamba wanapendekeza kila anayetakiwa kuwajibika awajibike kwa maslahi mapana ya Taifa.

“Katika kipindi hiki tuwaombe hata viongozi wetu wenye dhamana, anapokuwa hana jambo muhimu la kuzungumza, asizungumze jambo ambalo litatonesha mioyo ya wananchi. Tuombe hekima kwa Mungu ili kulirejesha Taifa pamoja.

“Hapa tulipo siko, na tusipokuwa makini huko tuendako siko kabisa. Tutafika mahali tutashindwa kurudi tulikotoka. Rai yetu ni kwamba tuangalie namna bora na shirikishi, yenye kuaminika na wote, na msingi wa kutuongoza katika hili uwe ukweli, haki, uwazi na uwajibikaji,” amesema Mwabukusi.

Amesema ni muhimu kama Taifa tuongee kwa ukweli bila kufarijiana kwamba tumejitia aibu, lakini lazima itafutwe namna ya kutoka, na njia hiyo iongozwe na ukweli, haki, uwazi na uwajibikaji.

Sambamba na hilo, Mwabukusi amesema Mahakama ina wajibu wa kulinda haki za msingi za wananchi kwa kutoa uamuzi huru bila upendeleo, pamoja na kutoa mwongozo katika utatuzi wa migogoro ya kijamii, kiuchumi, kiutawala na kisiasa.

Amesema Mahakama pia ina wajibu wa kuhakikisha uwajibikaji wa mamlaka nyingine, jambo ambalo ni muhimu na ni nguzo ya demokrasia ya nchi.

Mwabukusi amesema inapoboreshwa Mahakama, mawakili wa kujitegemea wasisahaulike.

Mwabukusi awataka viongozi kuchunga kauli zao

Katika kutekeleza wajibu wake, amesema TLS imeendelea kutoa mapendekezo ya kitaalamu ili kuimarisha mazingira ya utendaji kazi na mabadiliko ya sheria mbalimbali.

“Tutaendelea kufanya hivyo kama wajibu wetu, japo kuna changamoto ya maoni haya mara nyingi kutozingatiwa. Ni vema waone umuhimu wa kushirikisha mawakili kwa kuwa hili ni eneo letu,” amesema.

Amesema wamekuwa wakitoa huduma za msaada wa kisheria moja kwa moja kwa wenye uhitaji, na wananchi 421 walisaidiwa kwa mwaka jana pekee.

“TLS itafanya kazi na kila mmoja, sehemu ya kushauri tutashauri, sehemu ya kukemea bila woga, na sehemu ya kupongeza tutapongeza. Kwa hiyo, tukikemea tuliyekupongeza usinune, na tukipongeza tuliyekukemea usichukie. Ni kawaida tu katika kufanya kazi yetu, kwa sababu kazi yetu ni uangalizi na uwajibikaji vilevile,” amesema.

Katika maelezo yake, Mwabukusi amesema wakili anapotekeleza wajibu wake, kuwe na mfumo mzuri wa kumlinda na kumhakikishia usalama.

“Wakili asihusishwe na makosa ya watu anaowawakilisha, awe mbakaji, awe muuaji, awe mwizi, awe fisadi, ana haki ya kuwakilishwa kwa mujibu wa sheria, na tunapomuwakilisha ni mtiririko uleule wa kisheria,” amesema.

Kuhusu ucheleweshwaji wa mashauri, hasa ya jinai, amesema angalau mahakamani kwa sasa kuna matumaini, ingawa bado kuna changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi.

Amesema TLS ina majukumu ya kijamii, na hata inapotokea wanamstaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ni utekelezaji wa wajibu wake na si kwamba ni maadui.

“Tukiwa na sheria nzuri lakini mtu hawezi kupata huduma za mawakili, siku zote nasema ni sawa na jitihada za mtu kukonyeza gizani, ujumbe wako hautafika,” amesema.

Ameeleza kuwepo kwa utofauti wa mifumo ya utoaji haki kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, akitolea mfano visiwani humo kuwa kama kosa halina dhamana, mshtakiwa atadhaminiwa iwapo itafika miezi sita bila kesi kusikilizwa.

“Tanzania Bara, makosa yasiyo na dhamana yanatumika vibaya kwa kuwa hakuna ukomo wa lini kesi inaanza kusikilizwa. Ni vema tufunge mtu tunayejua huyu ni mhalifu kuliko kutoa mwanya ambao unaweza kutumika kwa namna ya kuathiri wananchi wasio na hatia,” amesema.

Amesema ni vema kuona dhamana iwe chini ya mamlaka ya Mahakama ili ipime kama mshtakiwa anastahili kudhaminiwa au vinginevyo.

Ametaka maboresho ya Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST) kwa kuhakikisha kunakuwa na mfumo mzuri wa kuchuja na kuwapata watu sahihi ili kuepuka kuzalisha mabomu.

“Tuweke utaratibu mzuri wa kuhakikisha mtu anayekuwa wakili anathibitishwa kwa uwakili wake. Kama kuna namna tunataka kurahisisha au kuona mtu, kwa uzoefu wake, anahitaji kupata uwakili, basi tuweke chujio linalobana mno ili LST ipitie jicho kali,” amesema.

Amesema ni muhimu kufanya hivyo kwa sababu kumekuwa na matukio ya mawakili kutelekeza wateja mahakamani, na wakati mwingine kuchukua fedha za wananchi na kuwakimbia.

“Wakili anapokuja huku ni uadilifu, kutokufaulu mtihani wako ni kukosa uadilifu vilevile, si kuonewa. Pengine hauna wito kwenye hilo au hauna uadilifu, kwa hiyo tusiwaonee huruma,” amesema.