TMA yatoa tahadhari upungufu mvua za vuli

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agnes Kijazi (katikati)wakati akitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za vuli kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba

Muktasari:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeshauri matumizi mazuri ya chakula kwa uangalifu katika ngazi ya kaya na taifa huku wakishauri malisho ya mifugo yaandaliwe mapema kuzuia migogoro ya wakulima na wafugaji.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema, kutakuwa na upungufu wa mvua katika kipindi cha mvua za vuli zinazotarajiwa kuanza Oktoba hadi Desemba 2022, zitakazosababisha kupungua kwa unyevunyevu katika udongo hivyo kuleta athari mbalimbali.

Imeelezwa kutakuwa na vipindi virefu vya ukame na kuna uwezekano wa kutokea kwa mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ambayo inaweza kuleta athari.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Septemba 2, 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka TMA, Dk Agnes Kijazi wakati akitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za vuli kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba.

Amesema hali hiyo inasababishwa na migandamizo midogo ya hewa ambayo imeendelea kuwepo katika ukanda mvua maeneo ya Somalia na hivyo kutarajiwa kuchelewa kwa mvua za vuli nchini.

Amesema migandamizo hiyo inatarajiwa kuanza kupotea ifikapo Desemba 2022 na hapo ndipo mvua kubwa zitaanza kunyesha nchini.

“Wananchi ambao maeneo yao yatakuwa makavu wanashauriwa kuacha kuotesha mazao mpaka pale mvua zitakapoanza,” amesema Dk Kijazi.

Ameshauri na kutoa angalizo kuwa ingawaje maeneo mengi yatapata mvua chini ya wastani kuna uwezekano wa kutokea vipindi vifupi vya mvua kubwa hivyo tahadhari inahitajika.

“Katika upande wa kilimo na usalama wa chakula upungufu wa unyevunyevu kwenye udongo na kutajitokeza kwa visumbufu vingi ikiwemo mchwa, viwavi jeshi, panya, nzige vinatarajiwa na ushauri unaotolewa na wakulima ni vizuri kupanda mazao kwa wakati na yanayostahimili ukame ikiwemo viazi, mihogo,mtama, viazi vitamu, mtama na jamii ya mikunde,” amesema Kijazi.

Ameshauri pia kutumika kwa mbinu na teknolojia ya kilimo kuhifadhi unyevunyevu kwenye udongo huku akishauri matumizi mazuri ya chakula kwa uangalifu ngazi ya kaya na taifa.

“Uwezekano kutokea migogoro kati ya wakulima na Wafugaji ni mkubwa kutokana na kutafuta malisho ya mifugo, matumizi sahihi ya maji na uhifadhi wa malisho yanashauriwa pia wafugaji na wavuvi wafuate ushauri wa utabiri wa hali ya hewa,” amesema Kijazi.