TMDA: Si sahihi kumwambia mgonjwa meza dawa kutwa mara tatu

Mkaguzi wa Dawa kutoka TMDA Kanda ya Mashariki, Joy Hezekieh

Muktasari:

  • Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), imesema sio sahihi kumwambia mgonjwa meza dawa kutwa mara tatu kwani kwa kufanya hivyo, inamfanya mgonjwa ameze dozi nzima ya dawa kwa mgawanyiko wa saa 12 pekee kitu ambacho sio sawa.

Kibiti. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), imesema sio sahihi kumwambia mgonjwa meza dawa kutwa mara tatu kwani kwa kufanya hivyo, inamfanya mgonjwa ameze dozi nzima ya dawa kwa mgawanyiko wa saa 12 pekee kitu ambacho sio sawa.

Hayo yamesemwa na Mkaguzi wa Dawa kutoka TMDA Kanda ya Mashariki, Joy Hezekieh, alipokuwa akitoa elimu ya matumizi sahihi ya dawa kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari zilizopo katika Halmashauri ya wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.

Joy amesema makosa hayo yamekuwa yakijitokeza kwa jamii na ikichukuliwa kuwa ni sahihi na ndio maana kwa sasa wameamua kutoa elimu kwa kuwafikia wanafunzi ambao wanaamini baadaye watakuwa mabalozi wazuri kwenye jamii juu ya matumizi sahihi ya dawa.

“Mfano unakuta cheti cha dawa  kimeandikwa 2x3, ambapo 2 inawakilisha idadi ya vidonge ambavyo mgonjwa anatakiwa kutumia kwa wakati huo na 3 inawakilisha muda, siku 1 ina masaa 24 ukigawanya kwa 3 unapata masaa 8, hivyo mgonjwa atatakiwa kutumia vidonge vyake kila baada ya saa 8.

“Lakini neno kutwa huleta maana isiyo sahihi na kimantiki huwafanya wagonjwa wameze dozi nzima ya dawa kwa mgawanyiko wa saa 12 pekee jambo ambalo sio sahihi,” amesema Mkaguzi huyo.

Joy amewataka wanafunzi hao kutokutupa hovyo dawa zilizokwisha muda wa matumizi majumbani badala yake wapeleke kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vilivyo karibu.

Pia mkaguzi huyo amewataka wanafunzi hao kuacha tabia za kutumia dawa pasipo kupima na kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pindi wanapohisi dalili za ugonjwa ili waweze kupata matibabu sahihi na kwa ugonjwa sahihi.

Hidaya Kimambi, mmoja wa wanafunzi, amesema ujio wa mamlaka hiyo shuleni kwao umempa manufaa ikiwenmo kujua dawa hunywea kila baada ya saa nane na sio saa tatu kama wengi wanavyofanya huko mtaani, na kuahidi kuwa balozi mzuri wa kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na waliyofundishwa.

Mwalimu Sikudhani, alisema TMDA imewasaidia kuwapa wanafuzi elimu ya matumizi ya dawa za uzazi wa mpango kwani wengi wao huzitumia bila kujua madhara yao na mapema kabla ya umri wao.

“Kupitia watoto hawa nina imani jamii inaenda kupata uwelewa wa matumizi sahihi ya dawa, kwa muda sahihi na mtu sahihi,” amesema Mwalimu Sikudhani.