TMDA yanasa madawa, vifaa tiba zisizo na ubora

Sehemu ya bidhaa zisizo na ubora zilizokamatwa wakati wa operesheni ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki katika mikoa ya Mara, Mwanza na Simiyu.
Muktasari:
Operesheni ya TMDA iliyofanikisha kunaswa kwa tani mbili za bidhaa ikiwemo dawa za binadamu na mifugo, vifaa tiba na vitendanishi vyenye thamani ya Sh30 milioni zisizo na ubora zilizoingizwa nchini kinyume cha taratibu ilifanyika katika Mikoa za Mwanza, Mara na Simiyu.
Mwanza. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki imekamata tani mbili za dawa za binadamu na mifugo, vifaa tiba na vitendanishi vyenye thamani ya Sh30 milioni zisizo na ubora zilizoingizwa nchini kinyume cha taratibu.
Bidhaa hizo zimekamatwa zikiwa zimehifadhiwa sehemu zisizofaa ikiwemo maduka, makazi ya watu, sokoni na maghala yasiyoidhinishwa katika mikoa ya Mara, Simiyu na Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Mei 18, 2023, Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki, Sophia Mzirayi amesema bidhaa hizo zimekamtwa wakati wa operesheni maalum iliyofanyika katika mikoa hiyo mwezi huu.
‘’Tayari tumeanza kuteketeza bidhaa hizo kwa awamu katika tanuru maalum la moto lililopo Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando,’’ amesema Sophia
Amesema kupitia ukaguzi huo, TMDA imeanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu waliobainika kuingiza nchini bidhaa zisizo na ubora wala salama kwa matumizi ya kiafya kwa mujibu wa Sheria ya TMDA Sura namba 219.
Amewataka wananchi wenye taarifa zinazohusiana na uingizaji wa bidhaa nchini kinyume cha sheria kutoa taarifa kwa mamlaka za dola kufanikisha udhibiti kabla ya madhara ya kiafya kutokea.
"Wananchi ambao ndiyo watumiaji wa bidhaa hizi na ambao ndio wako karibu na waingizaji na wafanyabiashara wa bidhaa hizi watoe taarifa TMDA na mamlaka nyingine za Serikali kuwezesha uchunguzi na hatua za kisheria dhidi ya wahusika,’’ amesema Sophia