TMDA yaidhinisha usalama dawa ya Benylin

Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo.
Muktasari:
- Aprili 13 mwaka huu, dawa ya maji aina ya 'Benylin pediatric syrup' toleo namba 329304 lilibainika kuwa na kiasi kisichokubalika cha vichafuzi aina ya Diethylene Glycol na Ethylene Glycol.
Dar es Salaam. Matokeo ya ufuatiliaji wa ubora na usalama wa dawa ya maji ya watoto maarufu Benylin, uliofanywa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba Tanzania (TMDA), umeonyesha dawa hiyo ni salama.
Dawa hii hutumika kuleta nafuu kwa watoto wenye umri kati ya miaka miwili hadi 12 wanapopata dalili au magonjwa yanayotokana na hali ya mzio, kama vile kukohoa na mafua yanayosababisha homa.
Benylin toleo namba 329304 lilibainika kuwa na kiasi kisichokubalika cha viambata vichafuzi aina ya Diethylene Glycol na Ethylene Glycol, vinavyoweza kusababisha madhara ya kiafya ikiwa ni pamoja na vifo kwa watumiaji.
Aprili 13, 2024 TMDA ilitoa tangazo kwa umma juu ya ubora na usalama wa dawa hiyo inayotengenezwa na kiwanda cha Johnson & Johnson (Pvt) kilichopo Capetown, Afrika Kusini.
Taarifa iliyotolewa Jumapili Mei 12, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo, imeeleza toleo hilo lilitengenezwa Mei, 2021 na tarehe ya mwisho wa matumizi yake ilikuwa Aprili, 2024.
Amesema ilidaiwa baada ya uchunguzi wa kimaabara, dawa hiyo ilibainika kuwa na kiasi kisichokubalika cha viambata au vichafuzi.
"Kufuatia kuwepo kwa taarifa hiyo, TMDA iliahidi kufanya uchunguzi wa kina wa dawa husika na inapenda kuwajulisha kuwa toleo tajwa (329304) pamoja na matoleo mengine ya dawa ya Benylin hayana tatizo lolote la ubora, usalama na ufanisi," amesema na kuongeza;
"Kwa matokeo haya, wananchi waendelee kuitumia kama kawaida. Aidha, wauzaji wa dawa jumla na rejareja wanaelekezwa kuendelea kusambaza na kuuza matoleo ya dawa tajwa yaliyopo kwenye soko."
Amevitaka vituo vya kutolea huduma za afya na hospitali binafsi na umma, kuendelea na matumizi ya dawa hiyo.