Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wataalamu lawamani utoaji holela antibaotiki kwa wagonjwa nchini

Dar es Salaam. Ukishamaliza matibabu, dawa unazopewa na wataalamu wa afya umewahi kuhoji au kujiuliza ni za aina gani, zitasaidia nini na zinaweza kukupa athari gani baada ya kuzitumia?

Watafiti wamechambua hilo na kubaini wataalamu wa afya wamekuwa wakitoa dawa nyingi za antibaotiki kwa wagonjwa tofauti na kiwango kinachotakiwa kimataifa, huku zile za mstari wa tatu na nne ambazo hazishauriwi zikitumika.

Hali hiyo imetajwa kusababisha ongezeko la usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antibaotiki mwilini ‘Antimicrobial resistance AMR’.

Hiyo ni kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (Muhas) zilizoonyesha Tanzania imefikia matumizi ya asilimia 88.0 kwa dawa za antibaotiki kinyume na mwongozo uliowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) unaoelekeza nchi zitumie asilimia 20.0 hadi 26.8.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha makadirio ya usugu wa vimelea dhidi ya antibaotiki ni asilimia 59.8 huku utafiti ukionyesha wengi hutumia antibaotiki bila ushauri wa daktari.

Akielezea tafiti hizo, Mfamasia na mkufunzi wa shule ya famasia kutoka Muhas, David Myemba anasema utafiti wa kwanza uliangazia matumizi ya antibaotiki katika vituo mbalimbali vya afya iwapo wanafuata mwongozo wa matumizi ya dawa hizo uliowekwa na WHO.

Anasema waliangalia matumizi yakoje katika vituo vya afya, idadi ya dawa zinazotolewa kwa ujumla, mgonjwa anazopatiwa, iwapo zipo katika mwongozo wa dawa wa Serikali na iwapo zipo katika orodha ya dawa muhimu.

“Tulibaini wastani wa wagonjwa wanapewa dawa nyingi tofauti na kiwango kinachotakiwa na kati ya hizo idadi ya dawa za antibiotiki ni mkubwa. Lakini pia tuliangalia zinaandikwaje, iwapo zinaandikwa kwa majina sahihi na kama zipo kwenye mwongozo wa dawa za serikali,” anasema.

Anasema mwongozo wa WHO unataka dawa anazopatiwa mgonjwa kwa asilimia 100 ziwepo katika orodha ya dawa muhimu, lakini tafiti zilibaini katika vituo vingi zipo chini ya asilimia hiyo.

Myemba anasema pia mwongozo unataka ziandikwe kwa majina ambayo si ya biashara, lakini dawa nyingi zinaandikwa kwa majina ya biashara ijapokuwa wapo wataalamu wachache wanaofuata mwongozo.

Anasema mwongozo huo umeainisha dawa kwa mistari minne zipo zinazoshauriwa kutumika, lakini wataalamu wengi wamekuwa wakitumia dawa zisizoshauriwa ambazo ni za mstari wa tatu na nne.

“WHO inashauri dawa za mstari wa kwanza ndizo zitumike na mstari wa pili zinashauriwa zitumike mara chache, mstari wa tatu na nne zisitumike kabisa. Mgonjwa asifike kwa mara ya kwanza na kupewa aina hizo kwa kuwa zina nafasi kubwa ya kujenga usugu.

“Hivyo zikitumika mara kwa mara ni rahisi wadudu au bakteria kupata usugu kwa urahisi, na za mstari wa chini zinashauriwa kwa kuwa si rahisi kutengeneza usugu na hizi za mstari wan ne zinaunganishwa mbili kwenye dawa moja, zinatakiwa zisitumike kabisa lakini tumezikuta zinatumika kwenye vituo vya afya,” anasema.

Myemba anasema dawa hizo zinazuiwa si kwamba zina madhara kuweza kumuua mgonjwa, lakini hazina ushahidi wa kisayansi wa kutosha kwamba ukiunganisha ampicillin na dawa nyingine inaweza kuwa na matokeo zaidi ikilinganishwa na kila moja ikitumika kivyake.

Hata hivyo anasema sababu ambazo zimekuwa zikitolewa na wataalamu ni kwamba zinapochanganywa dawa hizo mbili uwezekano wa kupata usugu ni mdogo.

Anasema tafiti nyingine ambayo Muhas waliifanya wakiangalia matumizi ya antibaotiki kwa watoto wadogo na wataalamu kwa kipindi cha mwaka 2019/2022 wakiangazia vitu vinavyoongeza matumizi ya dawa hizo.
Anasema waliangalia upande wa watumiaji ambao ni wazazi, jamii, wataalamu wa afya, wafamasia na madaktari.

“Tulilenga kuangalia kitu gani kinachangia matumizi ya antibiotiki, kinachochangia matumizi sahihi na yasiyo sahihi,” anasema.
 

Mwongozo wa WHO

Myemba anasema mwongozo wa WHO unataka dawa zote zitumike kwa usahihi, kwa mgonjwa sahihi, ugonjwa sahihi, dozi sahihi na itolewe katika njia sahihi na mgonjwa kufuatiliwa wakati akiitumia.

“Ili antibaotiki iweze kutolewa lazima kifanyike kipimo cha ‘culture’ kwa kuchukua sampuli kutoka kwa mgonjwa waoteshe bakteria, waangalie ni bakteria gani na ni dawa gani inaweza kumtibu bakteria husika.”

“Baada ya hapo ndipo mgonjwa aweze kupatiwa ile dawa, lakini tafiti zetu zimeonyesha kuwa katika vituo vingi vya afya hasa vile vya ngazi za chini, hospitali za rufaa za mikoa, hospitali za kanda mpaka zile za taifa utaratibu haufuatwi,” anasema.

Hata hivyo Myemba anasema katika tafiti hiyo, wamebaini miundombinu ya kimaabara na kiuchunguzi kuwa sababu ya wengi kushindwa kufuata mwongozo huo.

“Kemikali zinazotakiwa kutumika katika vile vipimo zinakuwa chache lakini pia gharama zinazotakiwa zitumike kwa mgonjwa wengi wanashindwa kuzimudu lakini pia kuna muda, wakati mwingine mgonjwa anakuja anaumwa sana mpaka uanze vipimo na kutoa majibu muda unakua umepita sana,” anasema.
 

Wagonjwa

Baadhi ya wagonjwa wamelalamikia kupewa dawa nyingi na wataalamu bila maelezo ya kina na hivyo kujikuta wakifanya kazi ya kumeza kwa lengo la kujitibu.

“Wataalamu wanatuandikia dawa nyingi sana hasa kama unatumia bima. Tofauti na nikiwa nalipa fedha kutibiwa. Sijajua ni nini lakini tunatamani tuwe tunaambiwa dawa ni za nini hasa itatusaidia,” anasema Aneth John mkazi wa dar es Salaam.

Baadhi yao wamekiri kuwa wamekuwa wakiwashirikisha wataalamu wengine wa afya pindi wanapopewa dawa na mara nyingi hushauriwa kuachana nazo, hasa zile antibaotiki za watoto.

Mifuko ya bima imekuwa ikipata changamoto zaidi baada ya wanachama wake kuwekewa dawa nyingi zikiwemo za antibaotiki na vituo vya afya ili kutengeneza fedha.

Ofisa Uhusiano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Grace Michael anasema wameweka udhibiti kwa baadhi ya dawa kutolewa baada ya majibu ya vipimo vya usugu wa vimelea ‘culture’ katika kuhakikisha mnufaika anakuwa salama.

“Mfuko unalipa madai kulingana na miongozo ya tiba, hivyo inapotokea mtoa huduma ametoa dawa nje ya mwongozo wa matibabu madai yake huwa hayalipwi,” anasema.
 

Madaktari watoa sababu

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Rais Mteule wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk Mugisha Nkoronko anasema bado matumizi ya dawa za antibaotiki hapa nchini na duniani kwa ujumla yanakutana na matumizi mabaya ikiwemo kutofuata miongozo na upatikanaji wake kiholela hasa katika nchi zinazoendelea.

Anasema idadi ya wataalamu wanaotoa huduma za afya nchini haijakidhi mahitaji ya WHO wakiwemo wafamasia, afisa tabibu msaidizi, tatibu msaidizi, daktari msaidizi, daktari, daktari bingwa na daktari bingwa mbobezi.

“Idadi kubwa ya matabibu na daktari msaidizi ndiyo inayobeba kwa kiasi kikubwa utumishi wa umma katika upande wa watoa huduma za afya kwahiyo madaktari, mabingwa na wabobezi wapo wachache hivyo huenda wanaoandika pia ni wa kada ya chini,” anasema.

Hata hivyo Dk Nkoronko anasema tafiti kama hizo zinaamsha mawazo ya kutaka kuangalia ni kwa namna gani miongozo inafuatwa.

“Hapa nchini kuna miongozo mikubwa miwili inayotumika, kwanza ni mwongozo wa orodha ya dawa na pili ni mwongozo wa tiba ambazo hizo zinatumika zaidi katika ngazi za msingi yaani kituo cha afya, zahanati na mpaka hospitali ya wilaya.

“Hatujawa na msisitizo mkubwa sana kwenye hospitali za rufaa za mikoa, kanda na taifa zenyewe hutegemeana na miongozo ya kanuni mbalimbali ambazo zina ongoza ugonjwa husika,” anasema.

Dk Nkoronko anasema tafiti hizo zinataka nchi ijitazame na kujisahihisha pale ambapo haifuati miongozo.

“Lakini wakati mwingine unaweza usifuate miongozo mizuri kwakuwa pia upatikanaji wa dawa unayumba mara kwa mara mtaalamu anaamua kutoa dawa iliyopo.”

Anakiri kwamba dawa ya antibaotiki lazima kuwepo na udhibitisho wa kuotesha bakteria kwa kuangalia dawa ipi inafaa ndipo aandikiwe mgonjwa na kwamba kuna mapungufu ya kimfumo na kiudhibiti yanayotakiwa kufanyiwa kazi.

Akielezea athari kwa mgonjwa, Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama Isaya Mhando anasema matumizi holela ya antibaotiki huchangia kwa kiasi kikubwa udugu wa dawa na baadhi ya wagonjwa hushindwa kutibiwa baadaye.

“Athari zake mgonjwa atapata usugu na kama akiugua ugonjwa fulani dawa iliyojenga usugu itashindwa kumsaidia na matokeo yake hawezi kupona ugonjwa isipokuwa itafutwe dawa iliyotengenezwa kwa viwango vya juu zaidi ambayo ni gahrama na kama hakuna anapoteza maisha,” anasema Dk Mhando.

Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST) Fadhili Hezekiah anasema lazima kuwe na usimamizi wa sheria kwa dawa zinazoathirika na usugu wa vimelea.

Anasema hiyo itasaidia ziweze kujilikana na kufuatiliwa kwani hata kwa sasa idadi ya antibaotiki ngapi zinaingia nchini na zinatoka kwa cheti hilo jawabu haliwezi kupatikana.

“Usimamizi wa sheria, dawa hizi ambazo tunaziita zinaathirika na usugu wa vimelea ni dawa za cheti, tuhakikishe dawa hizi zinapatikana kwa cheti tu hivyo tutadhibiti usugu, wafamasia wasimamiwe vizuri kwa kufuatiliwa kwa hakika ili kuziuza kwa kuzingatia sheria,” anasema Hezekiah.
 

Serikali yajipanga

Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi anakiri kuwepo kwa matumizi ya juu ya dawa za antibaotiki na kwamba kumekuwepo na uhamasishaji matumizi ya mwongozo wa matibabu unaoelekeza uandishi wa dawa.

Anasema Wizara ya Afya imeimarisha kamati za tiba na dawa kwa kuboresha mwongozo wa kamati hizo na kuongeza uratibu na ufuatiliaji wa utendaji wake.

“Tumehuisha mpango kazi wa mapambano juu ya usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa unaotekelezwa kwa utaratibu wa afya moja. Ndani yake kuna malengo,” anasema.

Msasi anasema katika hospitali za mikoa, kanda na Taifa wameanzisha kamati za uwakili (stewardship) wa kuratibu mapambano juu ya usugu wa dawa na sasa wanaangalia takwimu za kushuka kwa usugu wa dawa hizo.

Novemba 9, 2023 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliliondolea jukumu la usimamizi wa maduka ya dawa Baraza la Famasi nchini na kuipa mamlaka hayo rasmi Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) kutokana na ongezeko la matumizi holela ya dawa hizo.