TMDA yashauriwa kuongeza wataalamu wa vifaa tiba

Ofisa Ufuatiliaji Usalama wa Vifaa vya Tiba na Vitenganishi kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Amina Kingo akitoa elimu kwa Watumishi wa Afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

Watumishi wa Afya zaidi ya 70 kutoka Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure wamefundwa utoaji taarifa za vifaa tiba na vitendanishi visivyo na ubora, madhara na matukio yatokanayo na matumizi hayo ili kuepusha magonjwa na ulemavu unaoweza kutokea.

Mwanza. Baadhi ya watumishi wa afya jijini Mwanza wameiomba Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuongeza wataalamu wa afya watakao simamia na kukagua vifaa tiba ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya vifaa hivyo visivyo na ubora. 

Wakizungumza leo Jumatano Septemba 20, 2023 wakati wa mafunzo ya utoaji taarifa za madhara na matukio yatokanayo na matumizi ya vifaa tiba na vitendanishi kwa zaidi ya watumishi wa afya 70 wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwanza Sekou Toure wamesema uwepo wa wataalam hao utaepusha magonjwa na ulemavu utokanao na matumizi ya vifaa hivyo visivyo bora.

“Kabla sikuwai kupatiwa mafunzo ya namna hii japo kuwa nimewahi kushuhudia mtu ambaye alipata madhara yaliyotokana na vifaa tiba ambavyo havikuwa na ubora….nilishindwa kutoa taarifa ila sasa tumepewa mafunzo hata ikitokea nitakuwa mstari wa mbele,” amesema Daktari wa Kinywa na Meno hospitalini hapo 

Mfamasia wa hospitali hiyo, Donatha Ollomy ameshauri TMDA iongeze ufuatiliaji zaidi kwa kukagua vifaa tiba sambamba na utoaji elimu kwa wataaalamu wa afya na wananchi. 

“Wataalamu na wananchi wengi hawajui kuwa wakipata madhara yatokanayo na vifaa tiba watoe taarifa wapi, kwa hiyo hii elimu nafikiri itakuwa na msaada mkubwa kwetu lakini katika hilo nitoe wito kwa mamlaka husika ufuatiliaji uongezeke na wazidi kuongeza hamasa kwa watu wengine,”amesema Ollomy

Ofisa Ufuatiliaji Usalama wa Vifaa vya Tiba na Vitenganishi wa TMDA, Amina Kingo amesema watumishi wa afya wamepewa mafunzo hayo kwakuwa wao ndio watumiaji wakubwa akiamini baada ya elimu hiyo wataanza kupata taarifa ya vifaa tiba vyenye shida au dosari.

Mratibu Ubora wa Huduma Sekou Toure, Dk Denis Kashaija ametoa wito kwa wataalamu wa afya kutoa taarifa juu ya vifaa tiba vitakavyoonekana kuleta madhara kwa wananchi au kutokuwa na ubora unaohitajika. 

“Elimu hii ni nzuri sana kwa wataalamu wa afya na katika hili nitoe wito kwao kuwa baada ya kutoka hapa wawe mabalozi wazuri kwa wengine lakini pia wahakikishe wanatoa taarifa ya vifaa tiba na madhara kupitia fomu tuliyowapatia,”amesema Dk Kashaija