TMDA yatoa dawa za Sh25 milioni magereza Simuyu

Muktasari:

Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba Kanda ya Ziwa Mashariki imetoa dawa zenye thamani ya Sh25.2 milioni kwa magereza mkoani Simiyu.
Bariadi. Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba Kanda ya Ziwa Mashariki imetoa dawa zenye thamani ya Sh25.2 milioni kwa magereza mkoani Simiyu.

Akikabidhi dawa hizo meneja wa mamlaka hiyo, Sophia Mzilai leo Ijumaa ya 2 Desemba, 2022 amesema kuwa wamekuwa wakifanya shughuli hizo za kijamii kuhakikisha kwamba sehemu ya kile kinachopatikana kinaweza kusaidia jamii.

Dawa hizo ni zile zilizoondoshwa sokoni ili kufanyiwa uchunguzi na baada ya kuonekana kuwa ni bora na zina ufanisi, zinaweza kutoa matokeo chanya kwa ugonjwa stahiki ndipo zinatolewa msaada kwa watu wenye uhitaji.

Zoezi ambalo limekuwa likifanyika kwenye magereza tofauti tofauti, ambapo dawa zinazotolewa zimekuwa zikipelekwa katika zahanati na magereza ili ziweze kusaidia kwenye matibabu ya wafungwa na mahabusu ambao wameshikiliwa.

"Kwa hiyo tumeona magereza kuna ndugu zetu ambao wameshikiliwa kwa sababu mbali mbali pia wana haki ya kupata huduma za kiafya pamoja na huduma nyingine," amesema Mzilai.

Akipokea msaada huo Mkuu wa Magereza Mkoa wa Simiyu, Alexander Mmasi amesema utasaidia kwenye kazi zetu za kila siku za magereza kwa sababu kuna watu wapo ndani na hawapati msaada. Pia hawana huduma nyingine ambayo wanaweza kupata kulingana na hali halisi kuwa shughuli nyingi za madawa zinahitaji bima ya afya au msamaha.