TPSF, Diaspora kushirikiana kwenye uwekezaji

Muktasari:

  • Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwa kushirikiana na Watanzania wanaoishi nje ya nchi (TDH), wameingia makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya uwekezaji.

  

Dar es Salaam. Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwa kushirikiana na Watanzania wanaoishi nje ya nchi (TDH), wameingia makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya uwekezaji.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo leo Desemba 15, 2021, Mkurugenzi Mtendaji TPSF, Francis Nanai amesema mbali na kuingia makualiano hayo, pia TDH wako kwenye mchakato wa kujiunga na kuwa mwanachama wa TPSF.

Nanai amesema TPSF lengo lake kubwa ni kuendeleza juhudi za sekta binafsi Tanzania na adhma ni kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma kutoka wafanyabiashara wakubwa hadi wafanyabiashara wadogo.

“Na katika hili wawekezaji wa nje (diaspora) ni watu muhimu sana. Tulivyokwenda Marekani Septemba, moja ya vitu tulichokifanya ni kuongea na TDH kuwakaribisha Tanzania lakini pia kuwaahidi tutawashika mkono katika masuala mbalimbali ya kufanikisha juhudi na ndoto zao za kuwekeza kwa mafanikio nchini.

“Diaspora ni daraja na kiunganishi kizuri kati ya wafanyabiashara Tanzania na nje lakini pia ni kiunganishi kizuri kati ya serikali ya Tanzania na serikali kutoka nje.

“Kwahiyo kwangu mimi naona hii ni tunu au lulu ambayo watanzania tunatakiwa tuitumie kwa kiasi kikubwa. Tuwaone hawa ni wenzetu, rafiki zetu na tuwawezeshe ili waweze kuwekeza hapa nchini,” amesema Nanai.

Naye Mwenyekiti wa TDH, Nassoro Basalama amesema wameamua kuitikia wito wa Rais Samia Suluhu Hassan katika suala la uwekezaji.

Amebainisha kwasasa wapo katika hatua za mwanzo za miradi mbalimbali ikiwamo katani, samaki na parachichi.

“Sisi kama sehemu ya Watanzania tuna nafasi kubwa ya kushiriki katika fursa hizo za uwekezaji. Hivyo kwasasa tupo katika hatua za mwanzo za miradi kadhaa na tunategemea kufanya uzinduzi wa mradi wa Katani (Tanga) keshokutwa na leo tunaelekea Njombe kwaajili ya mradi wa parachichi na tutatembelea maeneo mbalimbali.

“Tumekuja kueleza kwamba tuko tayari katika suala la uwekezaji, na huu ni mfano wa vitendo katika miradi hii. Tupo zaidi ya 180 na namba inazidi kuongezeka, na kila mradi hauruhusu kuzidi watu 40,” amesema Basalama.