TRA yakusanya wastani wa Sh2.2 trilioni kwa mwezi

Muktasari:

  • Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeongeza makusanyo kwa asilimia 11.6 baada ya kukusanya Sh6.63 trilioni katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2023/24

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekusanya Sh6.63 trilioni katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2023/24, ikiwa ni ongezeko la asilimia 11.6 ya makusanyo ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka wa fedha uliopita.

Katika mwaka wa fedha uliopita mamlaka hiyo ilikusanya Sh5.94 trilioni. 

Hayo yameelezwa leo Jumanne, Aprili 2, 2024 katika taarifa iliyotolewa na TRA na kusainiwa na Kamishna wa mamlaka hiyo, Alphayo Kidata.

Taarifa hiyo inaeleza kiasi hicho kilichokusanywa ni ufanisi wa asilimia 95.17 ya lengo la kukusanya Sh6.97.

Mchanganuo wa makusanyo hayo kwa kila mwezi unaonyesha Machi, mwaka huu mamlaka hiyo imekusanya Sh2.49 trilioni chini ya lengo la kukusanya Sh2.56 trilioni.

“Makusanyo haya (ya Machi) ni ongezeko la asilimia 6.94 ukilinganisha na kiasi cha Sh2.32 kilichokusanywa katika mwezi kama huu robo tatu ya mwaka uliopita,” inaeleza taarifa hiyo.

Pia, Februari TRA ilikusanya Sh2.02 trilioni chini ya lengo la kukusanya Sh2.1 trilioni sawa na ufanisi wa asilimia 93, huku Januari ikikusanya Sh2.12 trilioni, sawa na ufanisi wa asilimia 94.4.

Kwa mujibu wa TRA, kilichochagiza makusanyo hayo ni kuongezeka kwa uhiari wa ulipaji kodi, muitikio mzuri wa walipakodi kuwasilisha ritani za kodi kwa mwaka 2024 na kuongezeka kwa ufanisi katika huduma za forodha.

Ili kufikia lengo la makusanyo la mwaka huu wa fedha, taarifa hiyo imeeleza TRA inawahimiza wananchi kutoa taarifa za vitendo vya ukwepaji kodi nchini ikiwemo biashara za magendo.

“Wafanyabiashara wote wanashauriwa kuendelea kutoa risiti za kielektroniki zenye viwango sahihi kila wanapouza bidhaa au kutoa huduma,” imeeleza taarifa hiyo.