Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utafiti wabaini urasimu ukusanyaji kodi

Mchumi kutoka Taasisi ya CHR Michelsen (CMI) Profesa Odd- Helge akizungumza wakati wa kuwasilisha matokeo ya utafiti ukusanyaji kodi.

Muktasari:

 Utafiti mpya umebaini kuwa, urasimu uliopo katika mfumo wa ukusanyaji na ufuatiliaji kodi unaweza kuwa kikwazo kwa uwekezaji na biashara nchini

 Dar es Salaam. Wakati Serikali ikijiwekea lengo la kuongeza biashara na uwekezaji nchini, utafiti mpya umebaini kuwa jitihada hizo zinaweza kukwazwa na urasimu katika mfumo wa ukusanyaji kodi.

Matokeo ya utafiti mpya yaliyoangazia hali ya ufanyaji biashara nchini na mfumo wa usimamizi, ukusanyaji na ufuatiliaji wa kodi, wafanyabiashara waliohojiwa wamesema, bado kuna urasimu hasa katika eneo la kodi.

Utafiti huo uliofanywa na  Taasisi ya Utafiti  Utafiti, Sera na Uchumi   (Repoa) kwa kushirikiana na Taasisi ya Chr. Michelsen (CMI) na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) ukihusisha kampuni 1,000 katika Mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar.

Matokeo ya utafiti huo uliojikita katika sekta ya viwanda, utalii na biashara yameonesha kuna baadhi ya sekta ambazo bado zinakabiliwa vikwazo hasa katika eneo la kodi na kuwepo mazingira magumu na muda mwingi unaotumika katika kufanikisha mchakato wa ulipaji kodi.

Kufuatia hali hiyo utafiti huo umependekezwa kuwepo kwa mfumo utakaopunguza urasimu na kuwarahisishia wafanyabiashara kulipa kodi kwa urahisi sambamba na kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara.

Akizungumzia matokeo ya utafiti huo leo Machi 21, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa Dk Donald Mmari amesema kilio hicho kimetolewa hasa na wafanyabiashara katika sekta ya utalii, wakilalamikia aina nyingi ya tozo na changamoto katika mfumo wa ukadiriji na utozaji wa kodi kwenye sekta hiyo.

“Katika maeneo yaliguswa kwenye utafiti huo sekta ya utalii ndiyo imeonekana bado kuwa na changamoto, wahojiwa wameeleza bado kuna tozo nyingi katika sekta hiyo na hata mfumo wa ukadiriaji na utozaji wa tozo una changamoto.

 “Mambo haya yasipofanyiwa kazi inawezekana kabisa yakafifisha juhudi za Serikali za kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara. Tunapaswa kutambua kuwa nchi zinashindana katika kuweka mazingira bora ya biashara ili kuwavutia wawekezaji kutoka kwenye mataifa yenye mitaji mikubwa,” amesema Dk Mmari.

Mchumi huyo amesema kama itaonekana mifumo yetu ya utozaji kodi Tanzania haiko vizuri, itakuwa nadra kuingia kwenye ushindani hivyo ni muhimu kufanyika mapitio katika mfumo mzima wa kodi ili uweze kurahisishwa kwa lengo la kutengeneza uwanja sawa wa ulipaji kodi.

Pendekezo hilo limetolewa pia na mchumi kutoka taasisi ya CMI, Profesa Odd-Helge aliyeeleza kuwa kuna umuhimu wa kurahisisha mazingira ya ulipaji kodi na kuwepo sera na sheria zinazotabilika.

“Mabadiliko ya sera na sheria yasiwe ya mara kwa mara, hii inachangia kuwaondolea uhakika wa biashara zao na uwekezaji wanaofanya.

“Kingine muhimu ni kuhakikisha hakuna vikwazo kwa wale ambao wako tayari kulipa kodi na kinyume chake hatua kali zichukuliwe kwa wale wanaokwepa kulipa kodi,” amesema Profesa Helge.

Makamu wa Rais wa viwanda TCCIA, Abdul Mwilima amekiri kuwepo kwa malalamiko ya wafanyabiashara hasa katika sekta ya utalii kutokana na uwepo wa kodi nyingi ambazo zinaathiri kinachokusanywa kutoka kwa mtalii.

“Unapoweka kodi na tozo nyingi kwenye sekta ya utalii itamlazimu mfanyabiashara kumtoza fedha nyingi mtalii, sasa mtalii akikutana na hali hiyo anaona kwa nini asiende nchi nyingine ambazo gharama zao ziko chini. Hii inasababisha idadi ya watalii isiwe kubwa licha ya vivutio vingi tulivyonavyo.

“Tutachukua haya matokeo na kuyawasilisha kwa mamlaka husika, kwa kuwa yameibua maswali muhimu ambayo yanaathiri mfumo na ukusanyaji wa kodi,” amesema Mwilima.