TTB kuuza kilo 125 milioni za tumbaku msimu wa 2022/23

New Content Item (1)
Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku nchini, Stan Mnozya (wa kwanza kshoto) akiwa na watumishi wa bodi hiyo wakiangalia tumbaku katika masoko ya tumbaku mjini Tabora. Picha na Robert Kakwesi

Muktasari:

Masoko ya tumbaku yameanza rasmi leo Jumatano Aprili 26, 2023 kwa makampuni ya ununuzi wa zao hilo kuanza kununua tumbaku kwa wakulima.

Tabora. Bodi ya Tumbaku nchini (TTB) inatarajia kuuza kilo 125 milioni za tumbaku katika msimu wa 2022/23 zenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani 250 milioni sawa na Sh575 bilioni.

Akizungumza leo Jumatano Aprili 26, 2023 wakati akikagua masoko ya tumbaku mkoani Tabora, Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Stan Mnozya amesema mauzo ya tumbaku msimu huu yanatarajiwa kuvuka mauzo ya miaka 10 iliyopita ambapo wakulima walipata Dola 213 milioni baada ya kuuza kilo 126 milioni za zao hilo.

“Msimu huu tuna uhakika wa kufanya vizuri na kuongoza katika mauzo  kwa fedha za kigeni,”amesema

Amesema masoko ya tumbaku yameruhusiwa mapema msimu huu ili wakulima wauze na kufanya shughuli zao zingine akidai msimu uliopita wakulima waliuza tumbaku kilo 60 milioni zenye thamani ya zaidi ya Sh245 bilioni na kufanya matarajio ya mauzo msimu huu kuwa mara mbili zaidi ya msimu uliopita.

Ameziagiza kampuni za ununuzi wa tumbaku kuhakikisha zinanunua tumbaku haraka iwezekanavyo huku akiwataka wakulima nao kuuza tumbaku yao mapema kwani masoko ya tumbaku hayatafika Julai mwaka huu.

Nao baadhi ya wakulima waliouza tumbaku yao kupitia kampuni ya ununuzi wa zao hilo ya Mkwawa leaf Tobacco wamesema masoko ya tumbaku yameanza vizuri na wanapata bei nzuri ya wastani wa Sh5,000 hadi Sh6,000 kwa kilo moja.

Solomon Issa amesema amepata Sh5,000 kwa kila kilo moja ya tumbaku aliyouza katika kampuni hiyo.