TUHUMA: Polisi yaua watuhumiwa - VIDEO

Muktasari:

  • Kamanda wa polisi aeleza namna ramani yao ilivyovujishwa na wananchi wa Pugu

Dar es Salaam. Kikosi Kazi cha Kupambana na Ujambazi cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kimeua watuhumiwa wawili wa ujambazi maeneo ya Ukonga na kupata bastola moja aina ya Chines, risasi tatu na maganda manne ya risasi.

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema tukio hilo lilitokea Februari 9 saa 3:30 usiku.

“Wakiwa (polisi) katika msako huo walipata taarifa kuwa maeneo ya Pugu Mnadani milimani kumeonekana kuna pikipiki moja aina ya Boxer haina namba za usajili ikiwa na watu wawili waliokuwa wamevalia makoti marefu,” alisema.

Alisema askari wakiwa njiani kuelekea eneo hilo, ghafla waliiona pikipiki hiyo na walipoamuru isimame dereva alikaidi na kuanza kuwarushia polisi risasi.

Mambosasa alisema polisi walijibu mapigo na kuwajeruhi watuhumiwa hao ambao walipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) lakini walifariki dunia kabla ya kufikishwa.

Novemba 29 mwaka jana, polisi waliwaua watuhumiwa sita wa ujambazi maeneo ya Ufi Ubungo.

“Tupo vizuri kuhakikisha mtu yeyote anayetaka kuwaua Watanzania wasiokuwa na hatia au kuwatia ulemavu anajutia kwa yale ambayo atayapata,” alisema.

Alipongeza wananchi kwa kuhamasika na kuendelea kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu na kwamba polisi wanazienzi kwa kuzifanyia kazi haraka na majibu yanapatikana.

Mambosasa alisema kwamba wanaotaka kupambana na Polisi hawatashinda kwa sababu wanapigana kwa haki hivyo wao wapo tayari kwa ajili ya kuwalinda Watanzania.

Pia, polisi mkoani Mwanza juzi waliwaua watuhumiwa watatu eneo la Nyakabungo ikidaiwa kuwa walikuwa kwenye harakati za kufanya uhalifu eneo hilo.