Tukiingia madarakani hatutamvunjia heshima Magufuli

Muktasari:

Mgombea mwenza wa urais wa Chadema, Salum Mwalimu amesema endapo chama chake kitashinda dola kitamheshimu na Rais wa sasa John Magufuli na kumpatia haki zake zote kama Rais mstaafu.

Dar es Salaam. Mgombea mwenza wa urais wa Chadema, Salum Mwalimu amesema endapo chama chake kitashinda dola kitamheshimu na Rais wa sasa John Magufuli na kumpatia haki zake zote kama Rais mstaafu.

Akiwa katika mkutano wa kampeni za kunadi sera za chama chake na kuwaombea kura wagombea udiwani, mbunge na urais, Mwalimu alisema Magufuli licha ya kuwa utawala wake ulikuwa na changamoto lukuki lakini hapaswi kuwa na wasiwasi.

“Kuthibitisha kuwa sina Kinyongo naye mimi nikiwa kama makamu wa Rais nitahakikisha Magufuli anapata haki zake zote kama mstaafu na katika kuthibitisha hilo kwa kuwa Lissu atakuwa na kazi nyingi na nyingine atakuwa akimtuma yeye kumwakilisha, atamtuma Magufuli ili walau achangamke asikae tu,” alisema.

Alisema atafanya hivyo kwa kuwa Magufuli akikaa tu atazeeka na atakuwa amekosa fursa kurushwa na TBC wakati ni miongoni mwa vitu ambavyo amevizoea.

Kadhalika, Mwalimu alisema Serikali ya chama hicho itaheshimu na kulinda biashara kubwa, ndogo na za kati na mamlaka ya ukuasanyaji wa kodi haitakuwa chanzo cha kuua biashara, bali kuzikuza kama ambavyo kanuni za uchumi zinaelekeza.

Mwalimu jana alilazimika kufupisha mkutano wake wa kampeni katika jimbo la Tarime kutoka na mvua iliyonyesha muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano.

Mwalimu alipanga kufanya mkutano wa kunadi sera za chama chake saa 9 kamili katika viwanja vya sabasaba lakini muda mfupi kabla ya kufanyika kwa mkutano huo mvua zilianza kunyesha hali iliyosababisha asubiri kwa muda, hata hivyo baada ya muda kidogo mvua zilikatika kisha akaelekea katika viwanja hivyo.

Alipofika uwanjani Mwalimu alikaribishwa na mgombea ubunge wa chama hicho kwa tiketi ya Chadema, Esther Matiko na alipopanda mvua ilianza kunyesha tena.

Hata hivyo mamia ya wananchi waliokuwapo katika viwanja hivyo waliendelea kumsikiliza naye aliwaomba azungumze kwa ufupi kutoka na hali ya hewa lakini pia alikuwa anawahi mkutano mwingine Musoma Mjini.

Mwalimu alisema anaelewa kuwa miaka mitano ya utawala wa Rais Magufuli umeacha maumivu kwa watu wote na huu ndiyo wakati wa watu kuchukua hatua dhidi ya maamuzi waliyopitia kwa kuwachagua wagombea wa Chadema kuanzia Rais, wabunge na madiwani.