Tume Huru ya Uchaguzi yasogeza mbele uandikishaji wapigakura
Muktasari:
- Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imebadilisha ratiba ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa kusogezwa mbele hadi Julai 20, 2024 ikiwa ni siku sita badala ya Julai Mosi, 2024, tarehe iliyokuwa imepangwa awali na INEC.
Kigoma. Maoni ya wadau wa uchaguzi wakiwemo wa vyama vya siasa, yamebadilisha ratiba ya kuanza uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa kusogezwa mbele hadi Julai 20 – 26, 2024 badala ya Julai Mosi hadi 7, tarehe iliyokuwa imepangwa awali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Hayo yamebainishwa leo Juni 22, 2023 na Mwenyekiti wa (INEC), Jaji Jacobs Mwambelege wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma, huku akibainisha kuwa hatua hiyo imekuja baada ya mkutano wa tume hiyo na wadau wa uchaguzi ngazi ya mkoa kilichofanyika Juni 19, 2024 mkoani Kigoma.
Amesema vyama vya siasa vilitoa maoni na kushauri kusogeza mbele uboreshaji wa daftari ili kuwapa fursa kwa wao kuhamasisha wananchi na wafuasi wao kujitokeza kushiriki kwa wingi.
“Vyama vya siasa vilitoa maoni na kushauri kupatiwa muda wa kutosha kwa ajili ya kuwapata mawakala wa uandikishaji ili mawakala hao washiriki kwenye uboreshaji kikamilifu,” amesema mwenyekiti huyo wa Tume.
Jaji Mwambelege amesema wadau walishauri Tume ijipe muda wa kutosha kutoa elimu ya mpigakura kwa wadau na wananchi kabla ya kuanza kwa uboreshaji wa daftari hilo ili waweze kuelewa na kujitokeza uboreshaji utakapoanza.
Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, wamesema kusogezwa mbele kwa tarehe ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kuende sambamba na utoaji wa elimu kwa wananchi ili siku ikifika, kila mwananchi aone umuhimu wa kwenda kujiandikisha na kuboresha taarifa zake.
Mwananchi, Amosi James amesema wananchi wengi hawana uelewa kuhusu uboreshaji wa daftari na kujiandikisha taarifa zao, lakini kama uelimishaji utafanyika kwa kipindi chote hadi kufikia siku hiyo, watu watajitokeza kwa wingi.
“Tumepokea taarifa kwa mikono miwili na tumeona Tume imezingatia maoni ya wadau na kuyafanyia kazi, hivyo ni jambo nzuri wamefanya tuwaombe sasa wafike kila eneo hadi ngazi ya familia kutoa elimu hadi vijijini ndani kwa watu wasiokuwa na redio wala Tv ili taarifa ziwafikie na siku ikifika wajitokeze kwa wingi,” amesema Salma Rashid.