Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

INEC: Usahihi wa taarifa kurahisisha uandikishaji wapigakura

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Jaji, Jacobs Mwambegele akizungumza na wahariri na waandishi wa habari hawapo pichani jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Mfumo umeboreshwa kuwezesha mtu kuanza mchakato wa kujiandikisha kwenye simu ya mkononi au kompyuta.

Dar es Salaam. Uzinduzi wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura ukitarajiwa kufanyika mkoani Kigoma Julai Mosi, 2024 wananchi wanapaswa kuzingatia mambo kadhaa ikiwamo usahihi wa taarifa binafsi, kuepuka kuchukua muda mrefu kwenye vituo vya uandikishaji.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema katika uboreshaji wa majaribio uliofanyika katika Kata ya Ng’ambo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na Kata ya Ikoma, Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, moja ya changamoto iliyojitokeza ni baadhi ya wananchi kusahau majina waliyotumia walipojiandikisha awali, hivyo kuchukua muda mrefu kuhudumiwa.

Uboreshaji wa daftari unafanyika kwa kuandikisha wapigakura wapya wenye miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu 2025.

Pia kutoa fursa kwa wapigakura waliopo kwenye daftari ambao wamehama kuhamisha taarifa zao, wenye kuzirekebisha, kutoa kadi mpya kwa waliopoteza au zilizoharibika na kuwaondoa waliopoteza sifa za kuwamo kwenye daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa Tanzania au kifo.

Akizungumza leo Jumatano Juni 12, 2024 kwenye mkutano wa wahariri wa vyombo vya habari,  Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele amesema kutokuwapo taarifa sahihi zikiwamo za majina kwa wapigakura wanaohamisha au kurekebisha taarifa kunasababisha kuchukua muda mrefu kupata huduma.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Daftari na Tehama wa INEC, Stanslaus Mwita amesema mfumo endeshi wa android unaotumika katika usajili wa kielektroniki (BVR kits) unawezesha mtu kuandikishwa na kupata kadi ya mpigakura ndani ya dakika tano hadi nane.

Mbali na hilo, amesema kwa kutumia mfumo saidizi wa OVRS mwombaji atajaza maombi kwa kuingiza taarifa kwa kutumia simu ya mkononi au kompyuta na atapata ujumbe, hivyo atakapofika kituoni ataendelea na utaratibu mwingine hivyo kupunguza muda wa kuhudumiwa.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima amesema vyombo vya habari ndiyo chachu ya kufanikisha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura.

“Tunawategemea kuwahamasisha wananchi, kutoandika habari zinazoweza kusababisha watu wasione umuhimu wa kujitokeza kujiandikisha, kuboresha au kuhamisha taarifa zao,” amesema.  

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile akizungumzia umuhimu wa uboreshaji wa daftari hilo, amesema wananchi hawana utaratibu wa kutoa taarifa za watu wasiokuwa na sifa  za kuwepo katika daftari, wakiwamo waliofariki dunia.

"Wananchi hawana tabia ya kuchukua vyeti vya vifo kwa ajili ya kuondoa baadhi ya kumbukumbu katika mamlaka husika, lakini iwapo taarifa zitatolewa na kuwekwa katika mbao za matangazo ni rahisi kwa wananchi kusoma na kutoa maelezo kwa wasiokuwa na sifa," amesema.