Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tume ya Umwagiliaji yabaini janja ya matajiri

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde.

Muktasari:

  • Tume imetaja kuwa wakulima wengi katika maeneo ambayo kumejengwa miundombinu ya umwagiliaji ambao wanawashawishi wananchi na kununua maeneo yao ili wawo watumie fursa hiyo kwa kukodisha mashamba na kuwafanya wkaulima hao wawe vibarua.

Dodoma. Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeeleza kuwa tamaa ya fedha ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wakulima.

Imesema baadhi yao wanauza ardhi zao kwa wenye mitaji mikubwa licha ya Serikali kuwekeza katika miundombinu ya umwagiliaji kwa lengo la kuinua uchumi wao.

Tume hiyo imebainisha kuwa katika maeneo mengi yenye miradi ya umwagiliaji, kuna watu wenye uwezo wa kifedha wanaowashawishi wakulima kuuza mashamba yao, kisha kuyamiliki na kuyakodisha, hali inayowageuza wakulima hao kuwa vibarua katika ardhi zao za awali.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Aprili 23, 2026, na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, wakati akimkaribisha Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde katika ufunguzi wa Baraza la Taifa la Tume hiyo.

Hata hivyo, Mndolwa amesema tayari hatua zimeanza kuchukuliwa kukabiliana na changamoto hiyo, ikiwemo mpango wa kupima maeneo yote yenye shughuli za umwagiliaji na kuwapatia wakulima hati miliki.

Amefafanua kuwa hatua hiyo itasaidia kudhibiti ununuzi holela wa ardhi na kufanya iwe vigumu kwa wawekezaji wakubwa kununua maeneo makubwa kwa wakati mmoja.

Amesema upimaji huo unalenga kubainisha mipaka ya mashamba kwa uwazi, kuimarisha usimamizi wa ardhi, pamoja na kuzuia migogoro inayoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji.

Mndolwa amesema baadhi ya watu wenye uwezo wa kifedha wamekuwa wakiwahamisha wananchi kwa njia zisizo rasmi, hali inayohatarisha lengo la Serikali la kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na uwekezaji huo, na hivyo kupotosha dhima halisi ya miradi ya umwagiliaji.

Amesema Tume inaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji kwa kuzingatia ubora unaotakiwa, huku ikihakikisha ushirikishwaji wa wananchi ili wawe sehemu ya ulinzi na uendelevu wa miradi hiyo, kwa manufaa ya muda mrefu.

New Content Item (1)

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema Serikali inaipa kipaumbele sekta ya umwagiliaji, akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya maswali yanayoulizwa bungeni yanahusu suala hilo.

Kutokana na umuhimu huo, aliwataka watumishi wa Tume kuongeza bidii, weledi na ubunifu katika kazi zao, akisisitiza kuwa taasisi hiyo ina jukumu kubwa la kuwainua wakulima wadogo na wakubwa kutoka kilimo cha kutegemea mvua kwenda kilimo cha umwagiliaji.

“Umwagiliaji ni ajenda kubwa ya kisiasa; wabunge wanahitaji majibu kwa niaba ya wapiga kura wao. Ni vigumu kujibu maswali bungeni bila kugusia umwagiliaji. Hata hivyo, migogoro haipaswi kuvumiliwa, kwani imeanza kujitokeza kufuatia kuongezeka kwa bajeti,” amesema Silinde.

Ameongeza kuwa bajeti ya Tume imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, akitolea mfano kuwa katika mwaka wa fedha 2021/22 zilitengwa Sh51.5 bilioni, mwaka 2025/26 Sh382 bilioni na kwa mwaka 2026/27 zinatarajiwa kufikia Sh384.2 bilioni.

Silinde amesema Serikali imeiwezesha Tume hiyo kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, jambo linaloanza kuleta matokeo chanya kwa wananchi, hususan wakulima wanaotegemea miundombinu ya umwagiliaji.