Tusiwaweke watoto hatarini wanaposaka elimu

Muktasari:
- Saa tatu kasoro usiku ndani ya daladala zinazofanya safari zake kati ya Muhimbili na Kisewe jijini Dar es Salaam, namuona mwanafunzi wa kike akiwa anasinzia.
Saa tatu kasoro usiku ndani ya daladala zinazofanya safari zake kati ya Muhimbili na Kisewe jijini Dar es Salaam, namuona mwanafunzi wa kike akiwa anasinzia.
Baada ya kumhoji nikafahamu kuwa anaitwa Amina, na ni mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Muhimbili huku akiwa anaishi Kisewe.
Amina analazimika kuamka saa 10 alfajiri ili awahi usafiri kabla watu hawajaanza kuwa wengi kituoni, na wakati wa kurudi anatumia muda mwingi kukabiliana na hekaheka za vituoni.
Kwa sababu hii suala la kusinzia kwenye daladala ni kitu cha kawaida. Swali hivi wazazi tunafahamu ni namna gani tunawaweka hatarini watoto na kuwafanya hata wachukie kusoma?
Kutoka Kisewe hadi Muhimbili kuna shule ngapi ambazo mtoto huyu ameziacha, kiasi cha kuwekwa katika mazingira hatarishi kama hivi.
Kwa nini wazazi hatushtushwi na matukio ya ukatili yanayoendelea kutokea dhidi ya watoto na kutafuta namna bora ya kuwaondoka kwenye mazingira hatarishi, ikiwamo changamoto za usafiri wa umma?
Anachopitia Amina wanapitia watoto wengi ambao safari yao ya kusaka elimu huwaweka katika mazingira hatarishi, yanayoweza kuwaweka kwenye hatari ya kufanyiwa vitendo vya ukatili njiani.
Inafikirisha sana mzazi anaweza vipi kuwa na amani saa mbili usiku mtoto wake hajarudi nyumbani na anapitia katika eneo hatarishi, ambalo anaweza kufanyiwa chochote kibaya!
Inaelezwa kuwa watoto wengi wanafanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia wakiwa kwenye vyombo vya usafiri au hata katika jitihada za kutafuta usafiri wanapoelekea shuleni au kurudi nyumbani.
Mara kadhaa imekuwa ikielezwa kuwa wazazi na walezi, wanaaamini kuwapeleka watoto shule za mbali na nyumbani ni ufahari, ukweli ni kwamba wanawaweka katika mazingira hatarishi.
Bado najiuliza ina maana suala la usafiri kwa wanafunzi ndiyo limeshindikana kabisa, yaani hakuna mkakati ambao unaweza kuleta utatuzi wa kudumu wa changamoto hiyo ambayo imekuwepo kwa muda mrefu?
Wapo wanaoamini kwamba bodaboda ndio salama, unakuta asubuhi mzazi anamkabidhi mtoto wake kwa bodaboda ampeleke shule na kumrudisha nyumbani. Inaweza ikawa njia nzuri ya kumsaidia mtoto lakini pia inaweza kumuangamiza. Boda boda ndio wanaoongoza kuwafanyia unyayasaji wa kingono wanafunzi.
Kingine ni muhimu wazazi kuwa na utaratibu wa kuwakagua watoto wao wanaporudi ili kubaini kama wamefanyiwa aina yoyote ya ukatili kwa kuwa wengi huhofia kusema wanayokutana nayo.
Kulingana na watoto wengi wanaobainika kufanyiwa ukatili huwa wamepitia katika hali hii kwa muda mrefu, wanashindwa kutoa taarifa kwa wazazi au watu wa karibu hali inayosababisha wahusika wasichukuliwe hatua.
Bahati mbaya wanaofanya vitendo hivi huwatishia watoto kwamba wakitoa taarifa watawaua wazazi wao, hilo husababisha hofu na kuvumilia maumivu makali ambayo wanapitia kutokana na ukatili huo.
Kwa mujibu wa mratibu mradi wa msaada wa kisheria wa asasi ya Dignity Kwanza Community Solution inayotoa msaada wa kisheria kwa wakimbizi, Bishara Msallam, kuna changamoto kubwa ya malezi hali inayosababishwa na wazazi kukosa ukaribu na watoto.
Ni vigumu kwa mtoto kukuelezea changamoto aliyokutana nayo au anayotarajia kukutana nayo, endapo hautamweka karibu na kumfanya ajisikie huru kuzungumza na wewe.
Hata kama umebanwa na majukumu kiasi gani, mzazi au mlezi jaribu kutenga muda wa kuzungumza na mtoto wako na kuwa rafiki yake ambaye anaweza kumuelezea chochote au hatari anayokabiriana nayo.
Nitolee mfano wa Amina pamoja na kupitia katika mazingira hatarishi, hawezi kuwaelezea wazazi wake kwa kuwa hawajampa nafasi hiyo, anaendelea kupitia kwenye changamoto hiyo.
Ombi langu kwa mzazi unayempeleka mtoto hasa wa shule ya msingi katika shule ambayo inamlazimu kutumia usafiri, hakikisha anapata usafiri kwa wakati na katika mazingira salama.
Mfanye mtoto atamani kwenda shule ila shule isiwe mzigo kwake kiasi kwamba aichukie au kutamani kwenda njia nyingine tofauti na hiyo.
Hilo likishindikana mtafutie mtoto shule jirani na nyumbani hata kama ni mbali kidogo, lakini iwe ni mwendo wa kutembea katika mazingira yasiyo hatarishi.
Elizabeth Edward ni mwandishi wa Mwananchi. Anapatikana kwa barua pepe: [email protected]