Uamuzi mdogo kesi ya Sabaya Januari 14

Watuhumiwa wa kesi ya uhujumu uchumi akiwemo aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya na wenzake sita wakizungumza na Mawakili wanaowatetea katika kesi hiyo (Picha na Janeth Mushi).

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imepanga Januari 14, 2022 kutoa uamuzi mdogo endapo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya na wenzake sita wana kesi ya kujibu au la.

Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imepanga Januari 14, 2022 kutoa uamuzi mdogo endapo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya na wenzake sita wana kesi ya kujibu au la.


Uamuzi huo mdogo unatarajiwa kutolewa baada ya upande wa Jamhuri kuieleza mahakama kuwa wanafunga kesi.


Leo Januari 10, 2022 mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Patricia Kisinda, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Sekule ameieleza mahakama kuwa shauri lilipangwa kwa ajili ya kusikiliza ila upande wa Jamhuri wanaomba kufunga ushahidi dhidi ya washitakiwa hao.


Wakili wa Utetezi, Mosses Mahuna ameileza mahakama kuwa hawana pingamizi na ombi liliwasilishwa na upande wa utetezi.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27, 2021 Jamhuri walikuwa na mashahdi 13 na vielelezo zaidi ya nane.


Mbali na Sabaya watuhumiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.


Akiahirisha kesi hiyo Hakimu Kisinda amesema mahakama itatoa uamuzi huo mdogo Januari 14, mwaka huu.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano, la kwanza wakidaiwa Januari 22,2021 ni kuongoza genge la uhalifu na kosa la tano ambalo ni utakatishaji fedha linawakabili washitakiwa wote saba  wanadaiwa kupata Sh 90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Francis Mrosso, huku wakijua kupokea fedha hizo ni zao la kosa la vitendo vya rushwa.


Kosa la pili,tatu na nne Sabaya peke yake ameshitakiwa kwa makosa ya kujihusisha na rushwa ambapo anadaiwa kuchukua Sh 90 milioni matumizi mabaya ya ofisi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro.