Uamuzi wa Jaji Siyani kesi ya kina Mbowe hatua kwa hatua- 3

Muktasari:

  • Jana katika sehemu ya pili ya mapitio ya kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu waliokuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), tuliona jinsi walivyojenga hoja kuipa nguvu kesi yao.


Dar es Salaam. Katika sehemu ya pili ya mapitio ya kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu waliokuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), tuliona jinsi walivyojenga hoja kuipa nguvu kesi yao.

Mnyukano wa kisheria kati ya upande wa utetezi na Jamhuri ulizua kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi baada mawakili wa utetezi kupinga kupokelewa kwa maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili, Adam Kasekwa, kwa madai kuwa aliteswa kabla na wakati akitoa maelezo hayo.

Pia walipinga kupokelewa kwa maelezo hayo kwa madai kuwa yalirekodiwa nje ya muda wa kisheria tangu mshtakiwa huyo alipokamatwa. Endelea…

Katika kuchambua hoja za pande zote, Jaji Mustapha Siyani alianza na hoja ya kwanza ya pingamizi iliyodai kuwa maelezo ya Kasekwa yalichukuliwa nje ya muda unaoruhusiwa kisheria chini ya kifungu cha 50 (1) (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Kifungu hicho kinaweka mipaka kwa ofisa wa polisi anayemhoji mtuhumiwa kufanya hivyo ndani ya saa nne tangu alipomkamata mtuhumiwa.

Mwanya pekee wa kuongeza muda huo umetolewa chini ya kifungu cha 51 kwa masharti ya kuongeza muda huo ni kupeleka maombi kwa hakimu na kwa sababu za msingi zilizotajwa na sheria. Kwa mujibu wa ushahidi, Kasekwa alikamatwa Agosti 5, 2020 lakini maelezo yake yalichukuliwa Agost 7, 2020 katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam.

Katika kesi dhidi ya Mbowe na wenzake hapakuwa na ushahidi kwamba ruhusa iliombwa kuongeza muda wa kuchukua maelezo nje ya muda wa kisheria.

Hali hii ilimwacha Jaji Siyani na kitendawili cha kuamua kama maelezo hayo ya Kasekwa yanaweza kupokelewa kwa kutumia kifungu cha 50 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Jaji Siyani alirejea ushahidi wa Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ramadhani Kingai na Mahita Omar walioshiriki kumkamata Kasekwa ulioonyesha kuwa kabla ya kukamatwa, Kasekwa alikuwa na watuhumiwa wengine wawili eneo la Rau Madukani, Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Mmoja wao aliitwa Moses Lijenje ambaye uwepo wake katika eneo hilo uliungwa mkono na mshtakiwa Mohamed Ling’wenya.

Kwa mujibu wa ushahidi wa Jamhuri, mpango ulikuwa ni kuwakamata wote watatu, lakini waliishia kuwakamata wawili tu; Kasekwa na Ling’wenya.

Kwa mujibu wa mashahidi hao, Kasekwa ndiye aliyeongoza timu ya makachero katika maeneo mbalimbali kumtafuta Lijenje na jitihada za kumsaka ziliposhindwa, alisafirishwa hadi Dar es Salaam ambapo walifika saa 11:30 alfajiri ya Agosti 7, 2020 na kuhojiwa siku hiyo hiyo kuanzia saa 1:30 asubuhi mpaka saa 3 asubuhi.

Mbali na ushahidi Kasekwa mwenyewe na Mohamed Ling’wenya, Jaji Siyani alisema hata shahidi Lilian Kibona ambaye ni mke wa Kasekwa alijua kuwa mume wake aliletwa Dar es Salaam kutokea Moshi, na ndio maana alisema katika ushahidi wake alimtafuta katika vituo vya polisi na hospitali mbalimbali hapa Dar es Salaam. Hoja ya Jamhuri ni muda uliotumiwa na polisi kumtafuta Lijenje na kuwasafirisha watuhumiwa hadi Dar es Salaam, utolewe kwa kuhesabu muda wa msingi wa saa nne zilizowekwa na sheria kwa polisi kumhoji mtuhumiwa tangu alipokamatwa.

Upande wa utetezi uliamini kuwa baada ya kuchelewa kumhoji mtuhumiwa kama sheria inavyotaka, Jamhuri ilipaswa kwanza kuongezewa muda chini ya kifungu cha 51 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kabla ya kuendelea kumhoji.

“Kwa heshima ya wakili Mallya, kifungu cha 51 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinaweza kutumika pale tu ofisa anapogundua kuna muda wa kumhoji zaidi mtuhumiwa nje ya saa nne baada ya kuwa amekwishaanza kumhoji.

“Katika kesi hii hapakuwa na mahojiano yoyote rasmi aliyofanyiwa Adam Kasekwa kabla ya Agosti 7, 2020, hivyo kifungu cha 51 (1) kisingeweza kutumika kuomba muda zaidi wa kumhoji mtuhumiwa,” alisema Jaji Siyani.

Siyani aligeukia pingamizi la pili lililodai kuwa Kasekwa aliteswa kabla na wakati wa kuchukuliwa maelezo ambayo utetezi walipinga yasipokelewe kama kielelezo.

Kuthibitisha kuwa Kasekwa alitoa maelezo akiwa Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, upande wa mashtaka ulitegemea zaidi ushahidi wa ACP Kingai, Inspekta Mahita na DC Msemwa. Wakati wote ACP Kingai na Inspekta Mahita hawakushuhudia mtuhumiwa huyo akichukuliwa maelezo, ushahidi wao ulikuwa na madhara ya kuonyesha ukweli kwamba Kasekwa aliletwa Dar es Saalaam toka Moshi na alikabidhiwa kwa DC Msemwa.

Aliwasilisha mahakamani regista ya watuhumiwa wanaoshikiliwa inayoonyesha kuwa Kasekwa alipokewa Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam Agosti 7, 2020 saa 12:09 asubuhi. Kielelezo hicho kinaonyesha zaidi kuwa siku hiyo saa 1:11 asubuhi alitolewa selo kwa mahojiano na kurudishwa saa 3:05 asubuhi. Kinaonyesha pia ACP Kingai ndiye aliyemtoa Adam nje kwa mahojiano.

“Kupokelewa kwa regista hiyo hakukupingwa kabisa,” alisema jaji Siyani.

Kwa upande mwingine, ushahidi wa utetezi ulionyesha kuwa Kasekwa alitendewa kinyume na ubinadamu kwa kuteswa akiwa Kituo Kikuu cha Polisi, Moshi. Ilionyeshwa pia alisaini nyaraka kwa vitisho wakati akiwa Kituo cha Polisi, Mbweni.

“Nimezingatia ushahidi wa utetezi kuhusu pingamizi hili.

Kwa maoni yangu na kama ilivyoelezwa kwa usahihi na Kidando (Wakili wa Serikali Mwandamizi), maelezo hayo yamekwenda nje ya pingamizi lililowekwa kwa kuwa ushahidi wote wa utetezi unapingana na ukweli kwamba Kasekwa aliletwa Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam ambapo ACP Kingai anadaiwa kurekodi maelezo yake yanayopingwa.

“Kwa kuwa ACP Kingai aliomba kuwasilisha maelezo yaliyodaiwa kutolewa na Kasekwa Agosti 7, 2020 akiwa Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, na upande wa utetezi ulijua kuwa kamwe Kasekwa hakuletwa katika kituo hicho, hivyo ilitarajiwa pingamizi lingekuwa Kasekwa hakutoa maelezo yoyote akiwa Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kwa sababu hayo ndiyo maelezo ambayo ACP Kingai aliomba yapokelewe mahakamani.

“Kasekwa alitoa maelezo yoyote akiwa Kituo Kikuu cha Polisi, Moshi na kutia saini maelezo hayo kwa vitisho akiwa Kituo cha Polisi, Mbweni, hivyo maelezo hayo bado hayajawasilishwa mahakamani na pingamizi lolote kwa ushahidi ambao haujaletwa mahakamani litakuwa limeletwa kabla ya muda

“Mapingamizi mawili hayana mashiko hivyo nayatupilia mbali. Ninasema maelezo yaliyochukuliwa na ACP Kingai yalichukuliwa ndani ya muda unaoruhusiwa kisheria na yalitolewa kwa hiari na mshtakiwa wa pili, Adam Kasekwa,” alimalizia Jaji Siyani.