Uamuzi wa Mdee, wenzake wapigwa kalenda

Muktasari:

  • Mahakama Kuu ya Tanzania imeahirisha kutoa uamuzi wa maombi ya Halima Mdee na wenzake 18 ya kutaka kibali cha kufungua kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hadi Ijumaa ya Julai 8, 2022.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania imeahirisha kutoa uamuzi wa maombi ya Halima Mdee na wenzake 18 ya kutaka kibali cha kufungua kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hadi Ijumaa ya Julai 8, 2022.

Uamuzi huo ulikuwa utolewe leo Jumatano Julai 6, 2022 na Jaji Mustapha Ismail lakini Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Elimo Massawe amesema, haujakamilika na utatolewa Ijumaa hii.

Uamuzi huo unatarajia kutoa hatima ya safari yao ya kupigania uanachama wao na kulinda ubunge wao.

Mdee na wenzake wanaomba ridhaa ya kupinga uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11, 2022 kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama, yaani ipitie uamuzi wa Chadema kisha itoe amri mbili.

Pia, wanataka Mahakama itengue uamuzi wa Chadema kuwavua uanachama kwa madai hawakupewa haki ya kusikilizwa kabla ya kuvuliwa uanachama.

Novemba 27, 2020 Kamati Kuu ya Chadema iliwatia hatiani kwa kosa la kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu bila ridhaa ya chama.

Mwenendo wa mapambano

Mapambano ya Mdee na wenzake yalianza rasmi mahakamani Mei 12, 2022, walipowasilisha mahakamani maombi yao ya ridhaa.

Pia, walifungua maombi ya zuio la muda ili kulinda ubunge hadi maombi yao ya ridhaa ya kufungua maombi ya kupinga kuvuliwa uanachama yatakaposikilizwa na kuamuliwa.

Lengo la maombi hayo lilikuwa kumzuia Spika wa Bunge na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutekeleza uamuzi huo wa Chadema, yaani wasitangaze nafasi zao ziko wazi.

Mbali na Bodi ya Wadhamini wa Chadema, wajibu maombi wengine ni NEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Maombi hayo yalitajwa Mei 16, mwaka huu na Mahakama ikapanga kusikiliza maombi ya zuio Juni 13.

Mawakili wao ni Aliko Mwamanenge, Ipilinga Panya, Edson Kilatu na Emmanuel Ukash ambao waliomba Mahakama iamuru kina Mdee waendelee na ubunge hadi hapo itakapoamua vinginevyo.

Mawakili wa Chadema, Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya walipinga kutolewa kwa amri hiyo wakiainisha kasoro za kisheria katika maombi hayo.

Jaji John Mgetta aliridhia maombi ya mawakili wa kina Mdee na kutoa amri waendelee na ubunge wao mpaka maombi hayo ya zuio yatakaposikilizwa.

Pingamizi la Chadema

Juni 22, 2022, Jaji John Mgetta alitupilia mbali maombi ya kina Mdee baada ya kukubaliana na mawakili wa Chadema kuwa yalikuwa na kasoro za kisheria.

Jaji Mgetta alikubali kuwa katika sehemu ya uthibitisho, walithibitisha taarifa zilizomo katika hati ya kiapo badala ya hati ya maelezo na kukosea jina la mjibu maombi wa kwanza.

Jaji alikubali katika maombi yao, kina Mdee waliitaja Bodi ya Chadema kama ‘The Board of Trustee of Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)’, badala ya The ‘Registered Trustee’ of Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Kina Mdee hawakupoteza muda, Juni 23 walifungua upya maombi hayo baada ya kurekebisha kasoro.

Mawakili wa Chadema waliibua pingamizi dhidi ya maombi hayo ya zuio na Jaji Ismail akapanga kusikiliza pingamizi hilo Juni 29 mchana.

Pia, Jaji Ismail alitoa amri ya kulinda ubunge wa kina Mdee hadi siku ya usikilizwaji wa pingamizi la Chadema.

Serikali haikuwasilisha kiapo kinzani; na Chadema iliwasilisha kiapo kinzani dhidi ya maombi yote ya ridhaa na ya zuio, lakini nje ya muda walioamuriwa na Mahakama.

Badala ya Juni 28, wao waliwasilisha Juni 29 asubuhi, huku wakiwa wameibua pingamizi dhidi maombi ya ridhaa.

Wakati huohuo, mawakili wa kina Mdee waliandaa mapingamiizi ya awali dhidi ya viapo kinzani vya Chadema, wakidai kuwa kiapo kinzani dhidi ya maombi ya zuio, kimewasilishwa nje ya muda.