Uanaume una mengi yasiyozungumzwa

Takwimu za wastani wa umri wa kuishi katika nchi nyingi zinaonesha wanaume huwatangulia wake zao kufariki dunia. Uwezekano wa mke kuwa mjane ni mkubwa zaidi kuliko mwanamume kuwa mgane.

Kwa nini hali iko hivyo? Kuna mengi. Moja kubwa, ni hulka ya wanaume kuthubutu kufanya vitu vinavyohatarisha usalama wao. Nani anaongoza kuendesha kwa mwendo kasi usio salama? Nani hutumia mabavu zaidi katika kutatua migogoro yake? Nani hushiriki shughuli ngumu zinazomweka kwenye mazingira magumu? Unaweza kuona namna tabia zinavyoweza kufupisha maisha ya wanaume wengi.

Lakini kuna hili la matarajio makubwa kwa mwanamume. Tangu mtoto wa kiume anapozaliwa, jamii inamtegemea aoneshe tofauti yake na mwenzake wa kike. Kazi atakazopewa ni zile zinazohitaji nguvu, kuonesha ustahimilivu na ushujaa.

Inapotokea amekutana na hali ya kukatisha tamaa, akaonesha huzuni au akalia, jamii inamkejeli. Ufahamu wa mtoto wa kiume unajengwa kuamini kuwa kuonesha hisia ni udhaifu. Imani hizi zina maana yake. Jamii zilihitaji mashujaa wanaoweza kuilinda.

Ushujaa ukaonekana lazima uambatane na ubabe, ukorofi, kutokuonesha hisia na umwamba. Unaweza kuona mwanamume mwenye sifa hizo ndiye aliyehitajika na jamii.

Kisha kuna hili la majukumu. Kadiri mtoto wa kiume anavyoendelea kukua ndivyo anavyozongwa na majukumu. Umri wa kuanza kujenga ukaribu na wanawake ukifika, kazi ya kuanzisha mapenzi inamhusu.

Mwanamume, kwa mfano, ndiye atakayepambana kuhakikisha ‘mtoto wa watu’ anamwamini na kumkubali. Haya ni mapambano ya kujitahidi kupenda hata kama saa nyingine anatamani tu.

Bidii hizi zikilipa hatimaye mwanamume huyu anakubaliwa. Mwanamke anaumimina moyo wake kwake akiamini sasa amepata mtu wa kumlinda, kumfanya ajisikie salama na kubwa zaidi kumpenda kama tamthlia za ki-Filipino zinavyomwaminisha.

Kupenda tu haitoshi. Kwa wanawake wengi, kupata mpenzi kunabeba tafsiri sawa na kupata ajira mpya. Kuanzia hapo mwanamume ndiye atakuwa mfadhili wa kuwezesha maisha ya mwanamke yaendelee.

Mwanamume ndiye atakayenunua muda wa maongezi; kulipia gharama za saluni; kodi ya nyumba; mitoko na kila aina ya mahitaji kulingana na mtindo wa maisha aliouchagua mwanamke. Hata pale mwanamke anapokuwa na kipato, bado mwanamume ndiye mwenye jukumu la kuhakikisha maisha ya mwanamke yanafadhiliwa.

Taratibu za kufunga ndoa zitakapoanza, mwanamume ndiye anayeangaliwa. Mahari atalipa yeye. Harusi nayo, katika jamii zetu nyingi, hilo ni jukumu lake. Ikiwa unashangaa kwa nini vijana wanaogopa ndoa usilisahau hilo. Hofu kubwa ni majukumu yanayoambatana na familia, akiwaza gharama za harusi na familia anaona bora aendelee kusubiri.

Akishaingia kwenye ndoa, kazi ya kuonesha naye ana akili za maendeleo inaanza. Kama alikuwa hajajenga, sasa ana shinikizo la kupambana kufa kupona ahamie kwake. Kama alikuwa hana usafiri, inabidi apambane awe na usafiri wake. Mungu akiwajalia watoto, shule nazo zinaanza kudai ada.

Familia tandaa nazo hizi hapa. Jukumu la kuwatunza wakwe zake na familia yake mwenyewe hawezi kulikwepa. Haya yote yanaanza kula muda wake. Kipato hakitoshi. Ndoto zake zinaanza kugeuka kuwa ndoto kweli. Huu ndio wakati ambao yale matumaini yake alipokuwa kijana yanaanza kufifia. Kichwa cha mwanaume kinajazwa mambo mengi.

Mkusanyiko wote huu unatengeneza sonona ya ndani kwa ndani ambayo, wakati mwingine, inaweza kuathiri urijali wake. Muda wa kufikiria mahaba na mapenzi haupo kwa sababu kichwa kinaumizwa na maswali yasiyo na majibu na kwa bahati mbaya hana wa kumsaidia kupata majibu.

Kafundishwa kwamba mwanamume wa kweli hasemisemi shida zake kwa mke wake. Kaaminishwa kumshirikisha mke kila kitu kinachokusumbua huo ni udhaifu. Ingawa anakutana na wanaume wengi, kimsingi hana rafiki anayeweza kumwambia masuala halisi. Moyo wake unajaa mambo mengi yanayomsumbua ingawa kwa nje, lazima aoneshe kuwa yeye ni mtu ngangari, mwanamume wa shoka halalamiki.

Kama ni mcha Mungu, huu ndio muda wa sala na ibada. Huko wanakutana na mazingira yanayowaweka karibu na watu wenye matumaini. Lakini kama ataamua kutafuta faraja kwa watu, uwezekano ni mkubwa akaanza kutumia muda mwingi akilewa. Kuchelewa kurudi nyumbani kunaanza kulipa kwa sababu anaepuka ‘makelele’ ya mke wake.

Kwa upande mwingine, mke wake naye anaanza kushindwa kuelewa.

Malalamiko haya yana ukweli ndani yake. Mwanamke ameanza kujihisi kama mtu asiyependwa tena, aliyetelekezwa, asiye na mwenyewe. Moyo wake unakata tamaa lakini hajaweza kuelewa kile hasa kinachoendelea kwenye maisha ya siri ya mume wake.

Ujumbe wangu ni mdogo kwa wanawake. Wanaume wanapitia mambo mengi kimya kimya. Kikubwa wanachokihitaji kwenu ni kutiwa moyo, kutambua juhudi wanazofanya na angalau kuwafanya waamini ninyi ndio mbeleko ya uhakika badala ya kuwalalamikia, kuwakosoa, kuwahukumu na kuwakejeli.