Uchawa unaharibu uwajibikaji Tanzania

Muktasari:

  • Ndiyo maana nimetangulia kusema uwepo wa ugonjwa huu mpya katika siasa na jamii unaliharibu taifa letu na kulipofusha katika suala zima la uwajibikaji, suruali wanaiita shati na shati wanaiita suruali, tukiliendekeza hili hatutaboa wala kulisaidia Taifa.

Katika siku za karibuni taifa letu linanyemelewa na ‘ugonjwa’ wa uchawa ambao baadhi ya watu kwa sababu ya masilahi binafsi au ya kisiasa wanajitokeza na kusifia jambo au kuunga mkono uamuzi fulani hata kama unaumiza wananchi.

Bahati mbaya sana, tabia hii ambayo inafanywa sana na baadhi ya wateule wa Rais na baadhi ya wasanii limewaambukiza hadi wasomi wetu ambapo unamkuta Profesa au msomi mwenye shahada ya uzamivu (PhD) naye anafanya uchawa.

Mfano mzuri na wa karibuni kabisa ni suala zima la tozo za miamala ya simu na ile ya benki ambayo wananchi wanapaza sauti zao kuwa wanalipa kodi mara mbili mbili, lakini wanatokea chawa niliowasema, wanatetea kwa hoja dhaifu mno.

Hoja yao kubwa ni kwamba nchi lazima ijengwe na Watanzania wenyewe, au tozo zimejenga madarasa, hospitali na kadhalika, lakini msingi wa hoja ya wananchi ni ukubwa wa tozo na double taxation ambazo ni kutozwa kodi mara mbili.

Mathalani, mfanyakazi ambaye ameajiriwa na analipwa mshahara wake kupitia benki, unakuta alishakatwa kodi ya Lipa Kadri Unavyopata (Paye), sasa anapotaka kutumia kwenye hicho kidogo kilichobaki kama akiba yake, anatozwa tena kodi.

Unakuta anamega kidogo kutoka kwenye fedha yake iliyopo benki ili amtumie mzazi wake kijijini, anapoihamisha kwenda kwenye simu ya mzazi anakatwa kodi na mzazi anapoitoa fedha hiyo kwa wakala, naye anakatwa tena tozo.

Mfanyabiashara alishafanyiwa makadirio ya kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) au Halmashauri na akalipa na faida aliyoipata baada ya kutoa gharama za uendeshaji na kuiweka benki, anapokwenda kuitoa anakutana tena na tozo.

Kwa kanuni za fedha hili linakataa, lakini tumeshuhudia baadhi ya wateule wa Rais, wasomi wetu na baadhi ya wasanii wakitetea suala hili bila kujali maumivu wanayoyapitia watanzania, na ukichunguza sana ni uchawa tu unawasumbua.

Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Margaret Thatcher aliyehudumu kati ya mwaka 1979 hadi 1990 aliwahi kusema na hapa namnukuu “No nation ever grew more prosperous by taxing its citizens beyond their capacity to pay”.

Kwa tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili, Thatcher anasema hakuna nchi iliyowahi kuendelea kwa kuwatoza wananchi wake kodi kuliko kiwango chao cha kuweza kulipa, na hili ndilo linalotokea katika tozo, tumekamua hadi damu.

Desemba 10,1990 Baba wa Taifa, hayati mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema naye namnukuu “hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kujidanganya kuwa hayapo”, na hiki nathubutu kusema ndicho wanachokifanya hawa chawa.

Tabia hii ya uchawa ilishamiri sana kipindi cha Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, ambapo baadhi ya wasaka vyeo wakiwemo wasomi wetu walimsifia na kumpamba Rais, lakini walifanya hivyo si kwa masilahi ya umma.

Walifanya hivyo kupalilia vyeo au nyadhifa zao, wakiacha maumivu kwa wananchi na nilifurahi sana Februari mwaka huu wakati wa Jubilee ya miaka 25 ya Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara nilipomsikia Rais Samia Suluhu akikataa kutukuzwa.

Rais Samia alikuwa akijibu kauli iliyotolewa na Askofu wa jimbo hilo Severine Niwemugizi, aliyemuomba kutokubali kulinganishwa na Mungu kwa namna yoyote ile, naye akasema atajitahidi kuwa na hekima na uvumilivu na awe na sikio la kusikiliza yale yanayosemwa na wengine, na huu ndio uongozi tunaoutaka.

Nikimnukuu, Rais alisema “Baba Askofu katika kufunga hotuba yako umeniasa mambo ya kukataa kutukuzwa na mimi nataka nikuahidi mbele ya umma huu kwamba, hii si tabia yangu na ninajitahidi kujishusha niwe sawa na wengine”

Naishukuru Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba kwa kusikiliza kilio cha Watanzania, licha ya suala hilo kuanza kufanyiwa uchawa na makundi niliyotangulia kuyasema.

Makundi haya ndio ambayo kama nilivyotangulia kusema, yanachangia kuondoa uwajibikaji kwani kiongozi anasifiwa hadi analewa sifa na kujisahau na hili limefanywa na hata baadhi ya wabunge ndani chombo hicho cha uwakilishiwa wananchi.

Leo hii Rais Samia anaponya majeraha na kusaka maridhiano ya kitaifa si kwamba taifa halikuwa na viongozi ambao wangeliepusha kufika hapo, la hasha ni kwa sababu kulikuwepo na chawa waliosifia kila kitu kwa maslahi ya kisiasa na binafsi.

Ndiyo maana nimetangulia kusema uwepo wa ugonjwa huu mpya katika siasa na jamii unaliharibu taifa letu na kulipofusha katika suala zima la uwajibikaji, suruali wanaiita shati na shati wanaiita suruali, tukiliendekeza hili hatutaboa wala kulisaidia Taifa.