Uchunguzi ajali ya moto Sekondari Bigwa Sisters waanza rasmi
Mabweni ya Shule ya Sekondari ya Bigwa Sisters iliyopo Manispaa ya Morogoro yakiteketea kwa moto jana jioni wakati wanafunzi wakiwa kwenye ibada kanisani. Picha Hamida Shariff
Muktasari:
- Ajali hiyo ya moto ilitokea Julai 26, 2026 wakati wanafunzi na walimu wao ambao ni watawa wa kike wakifanya ibada katika kanisa lililomo ndani ya shule hiyo.
Morogoro. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro limeanza rasmi kuchunguza tukio la ajali ya moto ulioteketeza mabweni ya Shule ya Sekondari ya Bigwa Sisters iliyopo Manispaa ya Morogoro.
Ajali hiyo ya moto ilitokea jana Julai 26, 2026 wakati wanafunzi na walimu wao ambao ni watawa wa kike wakifanya ibada katika kanisa lililomo ndani ya shule hiyo.
Moto huo umeteketeza mabweni matatu na mali za wanafunzi zikiwamo nguo, madaftari na vifaa vingine vya kujifunzia.
Akitoa taarifa kuhusu ajali hiyo leo Julai 27, 2026, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shabani Marugujo amesema uchunguzi wake utafanyika kwa kutumia vifaa vya kisayansi pamoja na kuhoji baadhi ya wahusika wakiwemo wanafunzi, walimu na uongozi wa shule.
Amesema katika uchunguzi huo, watachunguza visababishi vya moto ikiwemo mifumo ya usambazaji umeme kwenye majengo ya shule hiyo na viashiria vingine.
“Tunao askari wenye utaalamu wa kisasa wa kuchunguza, tutaangalia kama moto huo ulianza kwenye eneo moja ama ulianza kwenye maeneo tofauti, kwa sababu mbali ya kufungua kwa mabweni lakini pia sehemu ya darasa nayo ilionekana kushika moto kabla ya kudhibitiwa kwa kuzimwa,” amesema Kamanda Marugujo.
Aidha, amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa shule hiyo ilikuwa na wanafunzi wasichana 423 wa kidato cha tano na sita na kati ya hao, 118 ndio waliopata madhara ya kuunguliwa vifaa vyao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, Musa Kilakala amewataka wananchi wakiwemo wazazi, walezi, wanafunzi na uongozi wa shule kuwa watulivu wakati uchunguzi huo ukiendelea.