UDSM kufungua vituo vya uchenjuaji madini
Wanafunzi wa fani ya Madini na Jiosayansi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakisikiliza fursa zilizopo katika fani wanayosomea kwenye hafla iliyowakutanisha wajasirimali na wenye viwanda chuoni hapo.
Muktasari:
- Ni fursa kwa wanafunzi wa Shule ya Madini na Jiosayansi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam baada ya Shule hiyo kutangaza mpango wakuanzisha kituo cha uchenjuaji wa madini, ambacho kitajikita kutoa mafunzo kwa wanafunzi hao pamoja na ajira.
Dar es Salaam. Unaweza kusema ni fursa kwa wanafunzi wa Shule ya Madini na Jiosayansi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), baada ya kubainisha mpango wa kuanzisha vituo cha uchenjuaji wa madini katika mikoa ya Tabora na Shinyanga, ambayo vitoa mafunzo kwa vitendo na ajira.
Hayo yamebainishwa leo Julai 15,2023 na Mkuu wa Idara ya Uchenjuaji wa Madini wa chuo hicho Dk Aboubakar Salama, katika hafla iliyowakutanisha wanafunzi na wanaohitimu kwa lengo la kuwakutanisha na waajiri na pia kuwaonyesha fursa zilizopo.
Dk Salama amesema wakati vituo vyote viwili vinatarajia kuanzishwa mwaka, hata hivyo Tabora ndiyo itakuwa ya kwanza kupata kituo kitaanzishwa wilayani Nzega.
"Kituo hiki kitaanza mwakani na wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wapili wa fani ya Madini na Jiolojia, watakuwa na fursa ya kufanya mazoezi kwa vitendo na wengine wataajiriwa moja kwa moja," amesema.
Akizungumzia mpango huo, Amidi wa Shule ya Madini na Jiolojia chuoni hapo, Dk Elisante Mshiu, amesema: “…mbali na kituo cha madini wilayani Nzega, tutakuwa na kituo kingine cha uchenjuaji madini mkoani Shinyanga.”
Amesema katika kituo hiko, wafanyakazi 250 watahitajika na kwamba wanafunzi wanaopata mafunzo ndio watapewa kipaumbele.
Naye Mkuu wa Idara ya Madini, Dk Emmanuel Kazimoto, amesema idara hiyo ina mkakati wa muda mrefu na mfupi wa kuongeza wataalamu wa madini.
"Sasa hivi upo mchakato unaoendelea wa kuboresha mitaala na pia kuna mapinduzi ya nishati yanaendelea, tutazingatia namna gani mitaala yetu inajikita huko,” amesema na kuongeza;
“Tayari tumeanzisha makubaliano na mashirika makubwa ili kuongeza uwanda mpana wa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaohitimu fani hii, ili wanachojifunza kiendane na mahitaji ya jamii.”
Awali akifungua hafla hiyo, Mwakikishi wa Makamu Mkuu wa Udsm, Profesa Nelson Boniface amesema: “…ni muhimu wanafunzi hawa kutumia kila fursa wanayoipata kukuza taalamu zao kwa maana ya kujiajiri au kuajiriwa.”
Mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya Madini Jesca Kirita amesema hafla hiyo ni muhimu kuwatambulisha kwenye soko la ajira na kubaini fursa zilizopo katika sekta hiyo.