Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uelewa mdogo unavyogeuza vyanzo vya maji kuwa mashamba Kilombero

Muktasari:

  • Wananchi kutokujua umuhimu wa utunzaji wa mazingira imebainika huchochea uharibifu wa maeneo oevu unaotishia uhai wa Mto Kilombero, mafuriko na hata uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP).



Morogoro. "Hatukuwahi kujua kuwa kulima hapa ni kuharibu chanzo cha maji."

Hayo ni maneno yanayofanana kwa wakazi wengi wa Kata ya Lumemo, Halmashauri ya Mji wa Ifakara, mkoani Morogoro, baada ya kukiri kuwa kwa miaka mingi wamekuwa wakifanya kilimo, kufyatua matofali, kukata miti na shughuli nyingine ndani ya maeneo oevu bila kufahamu athari zake kwa mazingira.

Uchunguzi wa Mwananchi unaonesha ukosefu wa elimu kuhusu uhifadhi wa maeneo oevu umechangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa Bonde la Mto Kilombero, moja ya maeneo muhimu zaidi ya ikolojia nchini, lenye mchango mkubwa katika uzalishaji wa chakula na maji yanayoendesha uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP).

Katika Kata ya Lumemo, baadhi ya wananchi hulima mpaka kwenye vyanzo vya maji kila kipindi cha kiangazi wakifuata unyevunyevu wa ardhi, bila kutambua kuwa hatua hiyo hupunguza uwezo wa eneo oevu kuhifadhi maji na kuyatoa taratibu wakati wa kiangazi.

Kassim Makua, mzee mkazi wa Kibaoni katika Kata ya Lumemo, anakiri kuwa kabla ya mafuriko makubwa yaliyotokea msimu wa masika mwaka huu 2026, hakuwahi kufikiria kuwa shughuli hizo zinaweza kubadili mfumo wa maji.

“Umewahi kuona maji yanayokuja kama mlima? Ndiyo yametokea hapa kwetu,” anasema Makua akiwa chini ya mti pamoja na wazee wenzake, akieleza kuwa walisalimika baada ya kupanda juu ya minazi na paa za nyumba huku wakiacha mifugo, mazao na mali zao nyingine zikisombwa na maji.

Mbali na mafuriko, Makua anasema waliathirika kwa mlipuko wa kipindupindu, akieleza: “Mafuriko yalifumua vyoo, vinyesi vilikuwa vinaelea kwenye makazi, maji ya mvua yalichanganyika na maji taka.

“Hapa Lumemo tunafuga, tunalima, tunafyatua matofali na kuchoma mkaa. Mafuriko na kipindupindu viliturudisha nyuma katika shughuli za kila siku.”

Anasema shughuli za kilimo Lumemo zinafanyika takribani mwaka mzima, likiwa ni eneo lenye unyevunyevu.

“Tunafanya hivi miaka yote. Hatujawahi kusombwa na mafuriko kama ya mwaka huu. Huwa yanatokea ya kawaida, safari hii yamekithiri,” anasema mzee mwingine, Juma Msamiri.

Si wazee pekee wasiofahamu. Binti wa miaka 21, Warda Mponda, anasema hajawahi kupata elimu yoyote kuhusu umuhimu wa kutunza maeneo oevu wala madhara ya kulima kwenye vyanzo vya maji.

Kutokana na uelewa huo mdogo, shughuli za kilimo, ufugaji, uchimbaji wa udongo wa matofali, ukataji miti na uchomaji mkaa zimeendelea kusogea mpaka kwenye vyanzo vya maji.

Mbali na hayo, baadhi ya wananchi hutupa holela vifungashio vya pembejeo za kilimo, ambavyo huingia mtoni.

Kwa mujibu wa Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Salome Mahenga, utupaji usio salama wa vifungashio hivyo unasababisha viumbe hai kupotea na hata kuwepo kwa wasiwasi wa kuzalisha magonjwa sugu.

Mmoja wa wakulima wa eneo la Mang’ula, mkoani Morogoro, aliyejitambulisha kwa jina moja la Asenga, alipoulizwa endapo anaelewa kuhusu utupaji sahihi wa vifungashio hivyo baada ya matumizi, alisema: “Ninatupa pembezoni mwa shamba langu. Sina mahali pengine pa kutupa, na sijawahi kusikia wala kufikiria kuwa kuna athari.”

Mkulima mwingine, Nathaniel Matinyi, licha ya kuwa na uelewa kuhusu vibanda maalumu vya kukusanyia taka hizo, amedai kuwa vipo mbali, hivyo ni ngumu kwa kila mkulima kuvifikia.

“Wengi tunalazimika kutupa taka huku huku shambani,” anasema.


Athari za wazi

Ofisa Mazingira, Mahenga, anasema uharibifu wa maeneo oevu umesababisha baadhi ya mito kupoteza mkondo wake, huku mingine ikikauka.

Anasema maeneo oevu yanapovamiwa hupoteza uwezo wa kunyonya na kuhifadhi maji.

“Lumemo ni eneo linaloathirika pia kwa kipindupindu kwa sababu ya watu wengi kutokuwa na vyoo, na walionavyo huvifungulia wakati wa masika. Hivyo, majitaka yanaingia kwenye vyanzo vya maji na kusababisha kuenea kwa kipindupindu,” anasema.

Anasema uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu, ikiwamo kilimo kwenye vyanzo vya maji, umesababisha mito mingi kutoweka na mingine kupoteza mkondo wake.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini hali hiyo haiishii Lumemo pekee. Katika maeneo ya Iruma, Mang'ula na Ndenje, wananchi pia wanaendelea kulima kwenye maeneo oevu, wafugaji wanaingiza mifugo kwenye kingo za mito, huku ukataji miti ukiendelea.

Matokeo yake ni kupungua kwa kina cha mito, kutoweka kwa baadhi ya vijito na kuongezeka kwa uchafu unaoingia kwenye mfumo wa maji.

“Nilifika Kilombero mwaka 1998. Kulikuwa na mito 38, lakini sasa mingi imepoteza mkondo na mingine imekauka au kupungua kiwango cha maji, hali inayohatarisha uhai wa Mto Kilombero,” anasema Ofisa Mazingira, Mahenga.

Anasema kabla ya mgawanyiko wa kiutawala uliounda halmashauri mbalimbali, eneo la Kilombero na Mlimba lilikuwa na idadi ya mito 38 na vijito vingi vilivyokuwa vikichangia mfumo wa maji katika Mto Kilombero, lakini sasa mingi imetoweka.

Fundi Sanifu wa Hidrojia wa Bonde la Rufiji, Gerald Hamisi, anasema athari za uharibifu huo haziishii kwa wananchi wa Kilombero pekee.

Anafafanua kuwa Mto Kilombero huchangia asilimia 62 ya maji yote yanayoingia katika Bonde la Rufiji na hatimaye kufika JNHPP kwa ajili ya uzalishaji wa umeme.

Anasema maeneo oevu yanapoharibiwa, uwezo wa bonde kuhifadhi maji hupungua na kuathiri mtiririko wa maji unaohitajika katika uzalishaji wa umeme.

"Kilombero ndiyo moyo wa maji wa Bonde la Rufiji. Tukiharibu maeneo yake oevu, athari hazitakuwa kwa wakazi wa hapa pekee, bali hata kwa usalama wa rasilimali za maji zinazotumika kuzalisha umeme," anasema, na kuongeza:

“Ili liendelee kuwa salama, inatakiwa uoto wa asili uendelee kuwepo na kufanya ardhi ibaki chepechepe, kwa kuwa inasaidia kipindi cha mvua uwezo wa ardhi kunyonya maji kuwa mkubwa zaidi.”

Anasema Bonde la Rufiji linachukua asilimia 20 ya eneo lote la mabonde nchini Tanzania na ndilo kubwa zaidi, likipita katika wilaya 34 za mikoa 10 ya Pwani, Morogoro, Singida, Tabora, Njombe, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Lindi na Dodoma.

“Mabonde hufuata mifumo ya kihidrolojia inayoelekeza maji yanaenda wapi. Ndiyo maana utakuta kuna mito inayotoka Mkoa wa Tabora inaingia moja kwa moja kwenye Bonde la Rufiji, ambalo limegawanyika katika madakio (catchments) ya Ruaha Mkuu, Kilombero, Luwegu na Lower Rufiji,” anasema.


Usikose sehemu ya pili kesho, ambayo itaangazia sheria zinavyoshindwa kuzuia uvamizi wa maeneo oevu na mikakati ya Serikali.