Ufaulu wafamasia wazidi kuwa mfupa mgumu, nusu waanguka

Dar es Salaam. Zimwi likujualo halikuli likakwisha, hivyo ndivyo unavyoweza kusema juu ya matokeo ya usajili wa wanafunzi wa ngazi ya stashahada kada ya famasia kuonyesha kati ya wanafunzi 1,054 waliofanya mtihani mwaka huu zaidi ya nusu wameanguka.

Kulingana na matokeo ya mitihani ya usajili yaliyotolewa na Baraza la Famasia Tanzania, kati ya wanafunzi 1,054 waliosajiliwa kufanya mtihani huo Oktoba mwaka huu, wanafunzi 643 sawa na asilimia 61.2 watapaswa kuurudia mtihani huo,

Kundi jingine ni la wanafunzi 244 sawa na asilimia 23.3 wamefeli mtihani huo hivyo watalazimika kurudia darasa, wanafunzi wanane sawa na asilimia 0.8 wakibainika kuukacha mtihani, asilimia 15.6 sawa na wanafunzi 164 wakifaulu pekee.

Ikumbukwe si mara ya kwanza kwa wanafunzi wa kada hiyo kufeli, Aprili mwaka huu baraza hilo lilitangaza matokeo ya wanafunzi 1,104 kati yao 1,618 walirudishwa kufanya mtihani huo kwa mara nyingine.

Kwa wakati huo, anguko hilo la wanafunzi ilikuwa ni asilimia 68.2 ikilinganishwa na wanafunzi 380 sawa na asilimia 23.5 waliofaulu, 134 sawa na asilimia 8.3 wakipata daraja sifuri.

Wanafunzi wanaosoma famasia ndio wanaohusika kutoa dawa kwa mgonjwa baada ya kuandikiwa na daktari na husimamia ufanisi wa dawa kwa wagonjwa waliolazwa wodini.

Jana akizungumza na Mwananchi, kwa simu juu ya matokeo hayo, Msajili wa Baraza la Famasia Tanzania, Elizabeth Shekalaghe alisema tatizo la wanafunzi hao ni kutosoma.

“Ninachowaambia wasome, tatizo lililopo wanafeli sana hesabu ndio maana tukasema hesabu liwe somo la lazima,”alisema.
 

Tatizo liko wapi

Mfamasia ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema shida kubwa ni wanafunzi dhaifu kudahiliwa kusoma kada hiyo ya afya.

“Famasia ngazi ya diploma kushuka chini, ndiyo kada yenye vigezo vya chini kuliko kada zote, yaani ukilinganisha na udaktari, maabara au uuguzi ngazi ya diploma vigezo ni kuwa na D mbili pekee za kemia na biolojia.

Vigezo viko chini lakini kada hiyo ni ngumu kwa kuwa ina masomo ya Fizikia, Hesabu na Kiingereza lakini mwanafunzi anadahiliwa bila vigezo vya Kiingereza, Hesabu au Fizikia,”alisema.

Tatizo jingine analotaja ni walimu wenye stashahada kuwafundisha wanafunzi wa stashahada akishauri, walimu wenye shahada za juu ndio wawafundishe wanafunzi hao.

Aliitaja sababu nyingine ni wingi wa wanafunzi vyuoni hivyo kuathiri utoaji na upokeaji wa elimu hususan ufundishaji kwa vitendo.

Naye aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanafunzi Wafamasia Tanzania, Hamisi Msagama alisema kiini cha tatizo hilo ni wanafunzi wengi hufanya maandalizi ya mitihani hiyo kwa wiki mbili hadi tatu.

“Sasa kwa wanafunzi ambao wamesoma nje wanakuja nchini kufanya mtihani, hii huchangia maandalizi duni ukizingatia kuna somo linalohusisha hesabu.
Hivyo ushauri wangu kwa wanafunzi walio nje ya nchi wanaotarajia kupata leseni nchini, kuanza maandalizi haya mapema kwa kuwa na mawasiliano na waliopo kwenye vyuo vya ndani,”alisema.

Chanzo kingine cha anguko hilo, kimetajwa ni ongezeko la wanafunzi wa vyuo vya kati wasioendana na ubora wa mafunzo yanayotolewa.

Kwa upande wake Mfamasia, Jumanne Matumla alishauri udahili wa wanafunzi wa afya kwa ngazi ya diploma, uanzie kwa wale waliohitimu kidato cha nne ili ajiunge na kada hiyo akiwa na alama C tatu na na D moja katika masomo ya Kemia, Biolojia na Fizikia.

“Hizi kozi za afya ni muhimu kuwa na wataalamu wenye ufaulu wa juu na uelewa wa juu kwa sababu wanashughulika na afya za watu, kosa dogo linaleta ulemavu au kifo,” alisema Matumla.

Alisema mbali na wanafunzi kulaumiwa, miundombinu pia ya kuwezesha wanafunzi kuelewa masomo wanayofundishwa bado haijakidhi vigezo.

“Tupunguze idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kwenye vyuo vya diploma za famasia au tuwe na mtihani wa Taifa wa kuwachuja, wanapotoka mwaka wa pili kwenda mwaka wa tatu ambao huwa ni wa mwisho na alama za kufaulu ziwe asilimia 50 hadi 60 ili kupata wahitimu bora,” alisema.

Mitihani ya usajili wa kupata leseni kwa wanafunzi kada ya afya imeendelea kuwa mfupa mgumu kwani Julai mwaka huu madaktari tarajali 640 waliofanya mtihani 366 walianguka mtihani huo.

Kutokana na anguko hilo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu aliunda kamati ya kuchunguza matokeo hayo na baadae ikapendekeza madaktari tarajali wote waliofeli mitihani iliyoandaliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) warudie.

Kwa mujibu wa Kamati hiyo ambayo mwenyekiti wake ni aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohammed Bakari ilitaja sababu ya anguko la madaktari matarajali ni kwa baadhi yao licha ya kufaulu vyuo vyao na kupewa shahada ya udaktari, bado hawakidhi viwango vya ubora.

Sababu nyingine ya anguko la madaktari hao matarajali, ni hisia hasi kuwa MCT imeweka mitihani hiyo kudhibiti wanafunzi waliopata mafunzo ya udaktari nje ya nchi.