Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uganda, mataifa mengine 39 duniani kufanya uchaguzi mwaka 2026

Muktasari:

  • Katika bara la Afrika pekee, nchi 14 zinatarajiwa kufanya uchaguzi mwaka huu huku baadhi ya viongozi waliotawala nchi zao kwa muda mrefu wakitarajiwa kutetea nafasi zao.

Dar es Salaam. Ni mwaka wa uchaguzi. Hivyo ndivyo unavyoweza kuuelezea mwaka 2026 katika ulingo wa siasa za kijiografia kwa sababu mataifa 40 duniani yanatarajiwa kufanya uchaguzi mwaka huu ili kupata viongozi watakaoziongoza serikali zake.

Baadhi ya mataifa hayo yatafanya uchaguzi mkuu wa kuwapata Rais, wabunge na madiwani huku nchi nyingine zikitarajia kufanya uchaguzi wa Rais pekee na nyingine zikitarajia kufanya uchaguzi wa wabunge pekee.

Kwa Afrika pekee, nchi 14 zinatarajiwa kufanya uchaguzi mwaka huu huku baadhi ya viongozi waliotawala nchi zao kwa muda mrefu wakitarajiwa kutetea nafasi zao.

Uganda ndiyo nchi itakayofungua mwaka kwa uchaguzi wake wa Januari 15 ambapo Rais Yoweri Museveni anatetea kiti chake huku akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Museveni ameliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki tangu mwaka 1986 alipoingia madarakani baada ya kutekeleza mapinduzi ya kijeshi.

Sasa, kiongozi huyo anawania muhula wake wa saba katika uchaguzi huo ambao wapinzani wamekuwa wakipigwa mabomu kwenye mikutano yao ya kampeni.

Mataifa mengine ya Afrika yatakayofanya uchaguzi mwaka huu ni pamoja na Jamhuri ya Congo (Machi 22), Benin, Libya, Djibout, Cape Verde (Aprili 2026), Cameroon (uchaguzi wa wabunge - Mei) na Ethiopia (Juni 1).

Nchi nyingine ni Algeria (uchaguzi wa wabunge - Juni), Zambia (Agosti 13), Sao Tome and Principe (Septemba), Morocco (uchaguzi wa Bunge - Septemba) pamoja na Gambia na Sudan Kusini zinazotarajia kufanya chaguzi zao Desemba, mwaka huu.

Sudan Kusini ambayo ni nchi changa zaidi duniani, haijawahi kufanya uchaguzi wake tangu ilipojitenga na Sudan mwaka 2011 kutokana na mapigano baina ya pande mbili, moja ikiongozwa na Rais Salva Kiir na nyingine makamu wake, Riek Machar.


Kwingineko duniani

Mbali na mataifa ya Afrika, yapo mataifa mengine duniani yatakayoendesha chaguzi zao mwaka huu huku wananchi katika Mataifa hayo wakitarajiwa kutumia haki yao ya kuchagua viongozi.

Januari 2026, nchi zitakazofanya uchaguzi ni pamoja na Myanmar (Januari 11 na duru ya pili Januari 25) na Ureno (Januari 18). Februari ni nchi za Costa Rica, Thailand (Februari 8) na Bangladesh (Februari 12).

Bangladesh itafanya uchaguzi wake wa kwanza wa kitaifa tangu vuguvugu la wanafunzi lilipouangusha utawala wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Sheikh Hasina Wazed uliodumu kwa miaka 15, mwaka 2024.

Wapigakura pia wataamua kuhusu “Mkataba wa Julai”, mpango wa mageuzi unaolenga kupunguza mamlaka ya mhimili wa Serikali, kuimarisha mhimili wa mahakama na kulinda vyombo vya dola, hususan polisi, dhidi ya kuingiliwa kisiasa.

Machi 2026, sambamba na wenzao wa Vietnam na Slovenia, wananchi wa Nepal watapiga kura kuchagua viongozi wao.

Uchaguzi huo wa Machi 5, umechochewa kwa kiasi kikubwa na maandamano ya vijana maarufu kama Gen Z yaliyofanyika Septemba 2025, yaliyosababisha kuanguka kwa Waziri Mkuu, KP Sharma Oli kutokana na madai ya rushwa na mdororo wa kiuchumi.

Vijana wengi walioshiriki maandamano hayo sasa wamejikita katika kampeni za kuhamasisha usajili wa wapigakura, wakionyesha kuwa vijana wa Nepal wana fursa ya kubadili vuguvugu lao kuwa nguvu ya kisiasa na kushiriki kikamilifu katika kuunda mustakabali wa nchi yao.

Aprili 2026, nchi za Hungary na Peru zitafanya uchaguzi. Uchaguzi wa Hungary utaamua mwelekeo wa siasa za ndani za nchi hiyo na uhusiano wake ya kimataifa.

Waziri Mkuu Viktor Orbán, mshirika wa karibu wa Russia ambaye ameushutumu Umoja wa Ulaya kwa kuchochea vita kuhusiana na mzozo wa Russia na Ukraine, anakabiliwa na changamoto kubwa tangu achaguliwe mwaka 2010 kutoka kwa mpinzani wake, Peter Magyar wa chama cha Tisza.

Matokeo ya uchaguzi huo yataamua mizani ya kisiasa ya Hungary na msimamo wake kati ya Umoja wa Ulaya na Russia huku yakibeba athari pana kwa uthabiti wa Ulaya na mwelekeo wa vita nchini Ukraine.

Mwezi unaofuata, Mei, Cyprus, Colombia na Lebanon zitafanya chaguzi zao kwa nyakati tofauti. Raia wa Colombia watawapigia kura rais mpya baada ya muhula wa Rais wa sasa, Gustavo Petro, kukamilika na kutoruhusiwa kikatiba kugombea tena.

Ivan Cepeda wa muungano wa Historic Pact wa Petro anakabiliana na mgombea wa mrengo wa kati, Sergio Fajardo na Abelardo de la Espriella wa mrengo wa kulia.

Uchaguzi huo utaamua kama Colombia itaweza kusukuma mbele mchakato uliokwama wa makubaliano ya amani na waasi wa FARC, kukabiliana na rushwa, kudhibiti ongezeko la vurugu, na kusimamia changamoto za kikanda zinazotokana na nchi jirani ya Venezuela.

Hivyo, matokeo yake yatakuwa muhimu kwa uthabiti wa nchi na uhusiano wake na Marekani.

Uchaguzi wa Lebanon unaotarajiwa kufanyika Mei utakuwa mtihani mkubwa wa kwanza wa kidemokrasia kwa serikali ya Waziri Mkuu, Nawaf Salam na Rais Joseph Aoun.

Nafasi ya Hezbollah itakuwa miongoni mwa mambo makuu yatakayotoa mwelekeo wa uchaguzi wa Lebanon wa mwaka huu, kwani kura hiyo itaamua uzito wake wa kisiasa, itaathiri mjadala kuhusu kuondolewa silaha, na kuunda upya mizani ya madhehebu ya nchi hiyo katika kipindi cha misukosuko ya kiuchumi.

Juni 2026, Armenia itafanya uchaguzi wake wakati Fiji ikitarajia kufanya uchaguzi Julai na Haiti ikifanya uchaguzi Agosti. Septemba 2026, Sweden itafanya uchaguzi mkuu wakati Russia nayo ikitarajia kufanya uchaguzi wa wabunge.

Kwa upande wa chaguzi za Oktoba, Latvia na Brazil zimejiandaa kwa hilo. Oktoba 4, raia wa Brazil watawapigia kura Rais, wabunge wa Bunge la kitaifa na viongozi wa serikali za majimbo, huku nchi ikikabiliwa na hali ya kutokuwa na uhakika wa kiuchumi, ongezeko la uhalifu wa vurugu na uhusiano wenye mvutano na Marekani.

Rais wa sasa, Luiz Inácio Lula da Silva, anatafuta kuchaguliwa tena na atakabiliwa na wapinzani wake, akiwemo Flávio Bolsonaro, mtoto wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Jair Bolsonaro aliyefungwa.

Matokeo ya uchaguzi huo yanaweza kubadili upya uhusiano wa Brazil na Marekani, kuamua mwelekeo wa uchumi wa ndani na usalama, na kuufanya uchaguzi huo kuwa miongoni mwa chaguzi zenye athari kubwa katika eneo la Amerika ya Kusini.

Mwezi huohuo, Israel pia itafanya uchaguzi wa wabunge. Waziri Mkuu aliyedumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Israel, Benjamin Netanyahu, anaingia mwaka 2026 akikabiliwa na upinzani mkali wa kisiasa wa kusalia madarakani.

Ingawa kikatiba uchaguzi unatakiwa kufanyika Oktoba 27, Netanyahu anaweza kuitisha uchaguzi wa mapema hata Juni.

Chama chake cha Likud kinakabiliwa na shinikizo kubwa ndani ya nchi kutokana na kushindwa kwa mifumo ya kijasusi na namna serikali ilivyoshughulikia shambulizi la Oktoba 7, 2023, pamoja na lawama za kimataifa kuhusiana na vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelea Gaza.

Nchi nyingine zitakazofanya uchaguzi Oktoba ni Denmark, Bosnia na Bahamas. Novemba 2026, Wamarekani watafanya uchaguzi wa wabunge wao wakati Desemba 2026, New Zealand nayo inatarajiwa kufanya uchaguzi wake.