Uganda wapiga kura, mitandao ikifungwa

Thursday January 14 2021
ugandapic
By Mwandishi Wetu

Kampala. Wananchi wa Uganda leo wanapiga kura ya kumchagua Rais wa taifa hilo, huku kiongozi aliye madarakani, Yoweri Museveni akifungia mitandao ya Facebook na Twitter, akiituhumu kwa kuwa na hila dhidi ya utawala wake.

Museveni ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 35 sasa, anakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka mgombea wa chama cha NUP, Robert Kyagulanyi maarufu kwa jina la Bobi Wine, huku takribani watu 70 wakipoteza maisha tangu Novemba mwaka jana kampeni zilipoanza.

Akihutubia taifa Jumanne jioni muda mfupi baada ya kumaliza kampeni zake za siku hiyo, Rais Museveni alionya kuwa mtu yeyote atakayeshiriki vitendo vya wizi wa kura atakuwa anafanya kitendo cha uhaini.

Rais Museveni alisema utawala wake umechukua hatua ya kuifungia Facebook nchini humo kama hatua ya kulipiza kisasi kwa kitendo cha kampuni hiyo ya kimataifa kuwafungia wafuasi wa chama tawala cha NRM.

Kwa mujibu wa Facebook, waliamua kufunga majukwaa ya watu waliokuwa wakienda kinyume na sera ya kampuni hiyo kuhusu maadili.

Takribani watumiaji 100 wa Facebook walio na mafungamano na chama cha NRM waliathirika kutokana na hatua hiyo.

Advertisement

Licha ya tangazo la rais Museveni kuifungia Facebook, kamatakamata ya wanahabari wa mtandaoni wanaohusishwa Bobi Wine, imeripotiwa. Lakini baadhi ya wanahabari hao walio mafichoni wameapa kuendelea kuuelezea ulimwengu kinachoendelea Uganda.

Siku kadhaa zilizopita, wanasiasa wa upinzani walitoa tahadhari kwa wananchi kwamba serikali ilikuwa na mpango wa kuifungia mitandao ya kijamii kwa jumla ili kutatiza huduma za mtandao wa intaneti.

Wananchi sasa waligeukia matumizi ya ‘App’ mbadala kama vile VPN kuepukana na usumbufu huo. Mitandao ya kijamii ilitarajiwa kuwezesha mawasiliano kutoka sehemu mbalimbali za nchi ili matokeo ya uchaguzi yafahamike moja kwa moja.

Mtaalamu wa teknolojia na habari, Albert Muchunguzi alinukuliwa na shirika la habari la DW akitaja hatua ya Uganda kuifungia Facebook kuwa ni kinyume kabisa na mchakato wa kuwezesha uhuru wa kujieleza ambao ni haki ya binadamu.Katika hotuba yake kwa Taifa juzi kabla uchaguzi haujafanyika, Rais Museveni alitoa onyo kali kwa yeyote atakayejaribu kushiriki vitendo vya wizi wa kura.

Museveni alikaririwa akisema usalama umeimarishwa kote nchini humo na hakuna matukio yoyote ya kuvuruga uchaguzi yatakayotokea.

Advertisement