Ugonjwa usiofahamika ulivyozua hofu Lindi

Muktasari:

Wakati watu watatu kati ya 13 walioripotiwa kuugua ugonjwa usiofahamika wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi wakifariki dunia, wananchi wameelezwa kukumbwa na hofu kiasi cha kuogopa kwenda hospitali kuangalia wagonjwa.

Wakati watu watatu kati ya 13 walioripotiwa kuugua ugonjwa usiofahamika wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi wakifariki dunia, wananchi wameelezwa kukumbwa na hofu kiasi cha kuogopa kwenda hospitali kuangalia wagonjwa.

Pia wameiomba Serikali kutoa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa huo ambao umeshasababisha vifo vya watu watatu mpaka sasa.

Mkazi wa Kijiji cha Mkaranga, Kata ya Nambilanje wilaya ya Ruangwa Abdala Chigope, alisema yeye ni muhanga wa ugonjwa huo, kwani dada yake, Esha Issa aliupata, lakini baada ya kupatiwa matibabu amepata nafuu na anaendelea vizuri.

“Mimi ni miongoni mwa wahanga wa ugonjwa huu, kwani dada yangu alipatwa na tatizo hilo. Tunaiomba Serikali kufanyia kazi, ili kuondoa hofu kwa wananchi.”

Abdala alisema Julai 5, saa nne asubuhi alipokea taarifa kuwa dada yake kapatwa na ugongwa wa ajabu wa kuanguka na anatokwa damu puani na amekimbizwa kituo cha afya Mbekenyera.

Alisema baada ya kupata taarifa wanafamilia walikwenda kituo hicho cha afya na kubaini kuwapo kwa mtu mwingine mwenye matatizo kama hayo akitokea kitongoji cha Naungo ambaye hali ilikuwa mbaya kuliko ya ndugu yao.

“Tulipofika kituo cha afya Mbekenyera kumwangalia mgonjwa tulikatazwa kuingia kwenye wodi aliyolazwa na wakati huo mgonjwa mwingine aliongezeka, hali iliyotutia hofu na kuona tatizo ni kubwa,” alisema.

Abdala Kimwaga, mkazi wa Lindi mjini, alisema: “Tunaisha kwa mashaka makubwa sasa, tunaogopa hata kwenda kuangalia wagonjwa hospitali. Tunaiomba Serikali kupitia Nimr kuingilia kati kufanya utafiti wa haraka, ili kuokoa maisha ya watu.”

Alisema hali hiyo inatokana na ukweli kwamba bado hawajajua ugonjwa huo unaambukizwa kwa njia gani, hivyo hata kushindwa kuchukua tahadhari za kujilinda.

Pia alisema inawezekana mabadiliko ya hali ya hewa yanachangia kuwapo kwa ugonjwa huo kama alivyoeleza Rais Samia Suluhu Hassan, kwani kwa mikoa ya pwani mara nyingi kipindi hiki huwa kunakuwa na hali ya joto kali, lakini sasa hali imekuwa tofauti.

“Hivi sasa kuna mvua, upepo mkali na baridi kali, jambo ambalo halijazoeleka…inawezekana hali hii ikachangia kuwapo kwa maradhi haya.

Mohamedi Nurubi, kiongozi wa dini na mkazi wa Lindi mjini anasema katika historia ya maisha yake hajawahi kuona wala kusikia ugonjwa wa namna hiyo.

“Hili tatizo kwetu ni jipya, hivyo ni vema wadau wa sekta ya afya wa ndani na nje ya nchi washirikiane na Serikali kufanya uchunguzi, ili kubaini chanzo,” alisema.

Mohamedi alisema pia viongozi wa dini wana wajibu wa kukaa na kutafakari namna ya kuisaidia Serikali kupambana na tatizo hilo, ikiwemo kutoa elimu kwa waumini wao kuhusu ugonjwa huo na namna ya kujikinga.

Nurudini Abdala, Diwani wa Njinjo wilayani Kilwa mkoani Lindi aliwataka wananchi kuchukua tahadhari mapema, kwani ugonjwa huo umeanzia wilayani Ruangwa, hivyo unaweza kufika maeneo mengine na kuleta athari kubwa.

Alisema ni wajibu wa Serikali kufika maeneo ya waathirika na kutoa elimu, huduma za kinga za kiafya pamoja na kuchukua vinasaba, ili kwenda kupima na kuondoa hofu ya wananchi katika maeneo hayo.


Hatua ilizochukua Serikali

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichwale alisema wameshaunda timu ya wizara iliyowashirikisha wataalamu kutoka idara mbalimbali walioungana na wa mkoani Lindi.

Alisema wataalamu hao ni kutoka idara ya mifugo, magonjwa ya dharura na majanga, Epidemiolojia, Mkemia Mkuu wa Serikali, Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr), Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Hatua nyingine ni kuendelea kutafuta watu wengine wenye dalili kama hizi, ili kutambua mapema na kuwatenga ili kuzuia ugonjwa usisambae,” alisema Dk Sichwale.

Hatua nyingine ni kuorodhesha watu wote waliotangamana na wagonjwa, wahisiwa, marehemu na kuwafuatilia kwa siku 21.

Pia alisema watatoa matibabu kwa wagonjwa waliobainika kuwa na dalili za ugonjwa huo na kuwashauri wajitenge wakati wakisubiri majibu ya vipimo vya maabara.

Dk Sichwale alitaja hatua nyingine ni kutoa elimu, kufanya maandalizi ya dawa, vifaatiba na vya kujikinga na maambukizi kwa ajili ya kuwahudumia waathirika endapo watajitokeza tena.


Dalili za ugonjwa

Wagonjwa wametajwa kuwa na dalili za homa, kuvuja damu (hasa puani), kichwa kuuma na mwili kuchoka sana.

Dk Sichwale alisema sampuli za awali zilizopimwa katika maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii zimeonyesha majibu hasi kwa ugonjwa wa Ebola, Marburg na Uviko-19.

“Tunaendelea kufanya uchunguzi zaidi wa kiepidemiolojia na kitabibu, pia tunasubiri matokeo ya vipimo zaidi vya maabara ya magonjwa ya binadamu, wanyama na Mkemia Mkuu wa Serikali,” alisema.

Jumanne ya wiki hii, Rais Samia akizungumza katika mkutano wa 20 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu katika nchi za Afrika Mashariki na kati (AMCEA), alisema kwa uharibifu wa mazingira unaoendelea, kuna hatari kuendelea kuibuka magonjwa mapya kutokana na viumbe hivyo kusogea kwa binadamu kutokana na makazi yao kuvamiwa.

Alitoa mfano kuna ugonjwa umeibuka katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Alisema taarifa za ugonjwa huo zinahusisha na athari za uharibifu wa mazingira.

“Juzi nilikuwa na Waziri Mkuu, alikuwa akinipa ripoti ya ziara yake aliyofanya katika mikoa ya kusini, anasema huko Lindi kuna ugonjwa umeingia watu wanatokwa na damu puani kisha wanaanguka chini. Hatujui ni kitu gani, wataalamu na wanasayansi wameweka kambi huko kujaribu kuangalia kwa ukaribu.

“Kwa nini mwanadamu atokwe na damu puani, angekuwa mmoja au wawili tungesema presha imepanda na mishipa imepasuka, lakini ni wengi. Hii yote ni kwa sababu tunaharibu makazi ya viumbe, matokeo yake tunawasogeza kwetu wanatuletea haya maradhi mapya.”