VIDEO-Ugonjwa usiofahamika waua watatu Lindi

Ugonjwa usiofahamika waua watatu Lindi

Muktasari:

Watu watatu wamefariki dunia kati 13 waliougua ugonjwa usiofahamika mkoani Lindi ambapo moja ya dalili zake ni kuvuja damu puani.

Dodoma. Watu watatu wamefariki dunia kati 13 waliougua ugonjwa usiofahamika mkoani Lindi nchini Tanzania ambapo moja ya dalili zake ni kuvuja damu puani.

 Taarifa hiyo inakuja siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzungumzia ugonjwa huo alipokuwa akifungua Mkutano mkuu wa 20 wa Shirikisho la mabaraza ya maaskofu wa Kanisa Katoliki Afrika Mashariki na Kati (AMECEA) jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Julai 14, 2022 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Alfello Sichalwe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Dk Sichalwe amesema ugonjwa huo umetokea katika Halmashauri ya Ruangwa mkoani Lindi ambapo kumekuwa na ugonjwa usio wa kawaida kutoka Kituo cha Afya Mbekenyera.

“Ndani ya siku 3 (Julai 5 na 7, 2022) walipokea wagonjwa wawili katika kituo hicho wakiwa na dalili za homa, kuvuja damu (hususan puani), kichwa kuuma na mwili kuchoka sana,” amesema.

Amesema hadi kufikia Julai 12, 2022, kulikuwa na wagonjwa 13, kati yao, watatu wamefariki dunia.

Amesema wagonjwa wengine wawili waliokuwa wametengwa katika kituo cha Afya Mbekenyera, wamepona na kuruhisiwa kurudi majumbani mwao.

Profesa Sichalwe amesema wagonjwa wengine watano wamejitenga katika makazi yao ya muda kwenye kitongoji cha Naungo, Kata ya Nanjilinji Wilayani Kilwa.

Mganga Mkuu huyo amesema mgonjwa mmoja ambaye amepona, anaendelea kufanya shughuli zake kijijini Mbekenyera.

Aidha amesema, watu waliotangamana na wagonjwa hao (contacts) wamekuwa wakifuatiliwa afya zao kila siku na hadi sasa hakuna aliyeonesha dalili zozote zinazofanana na za wagonjwa hao.

“Sampuli za awali zilizopimwa katika maabara ya Taifa zimeonesha majibu hasi (negative) kwa ugonjwa wa Ebola, Marburg na Uviko-19,” amesema na kuongeza:

“Tunaendelea kufanya uchunguzi zaidi wa kiepidemiolojia na kitabibu pia tunasubiri matokeo ya vipimo zaidi vya maabara ya magonjwa ya binadamu, wanyama na mkemia Mkuu wa Serikali.”

Profesa Sichalwe amesema, wanaendelea kutafuta watu wengine wenye dalili kama hizi ili kutambua mapema na kuwatenga ili kuzuia ugonjwa usisambae

“Kuwatambua watu wote waliotangamana (Contacts) na wagonjwa/wahisiwa/marehemu na kuwafuatilia kwa siku 21,” amesema

Amesema kutoa matibabu kwa wagonjwa waliobainika kuwa na dalili pia kuwashauri wajitenge wakati wakisubiria majibu ya vipimo vya maabara,” alisema Profesa Sichalwe na kuongeza:

 “Kutoa elimu kwa jamii kwa kutumia vyombo mabalimbali vya habari e. Yamefanyika Maandalizi ya dawa, vifaa tiba na vifaa vya kujikinga na maambukizi kwa ajili ya kuwahudumia waathirika endapo watajitokeza tena.”