WHO, CDC kuchunguza ugonjwa usiojulikana Lindi

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imekubali ombi la Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha kukinga na kudhibiti magonjwa (CDC) kutoka Serikali ya Marekani ili kuongeza nguvu kwenye timu ya wataalam katika kubaini ugonjwa huo.

Dar es Salaam. Wakati timu ya wataalamu kutoka nje ikitarajiwa kuanza uchunguzi kubaini ugonjwa usiojulikana Lindi, Wizara ya Afya imesema sampuli za vipimo vya maabara zilizochukuliwa kutoka kwa wagonjwa zimeonyesha siyo ugonjwa wa Ebola, Maburg wala Uviko-19.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Julai 15, 2022 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipokuwa akizungumza kwenye Kikao cha 22 cha Kisekta cha Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kilichofanyika Jijini Arusha.

“Kuna mlipuko wa ugonjwa usiojulikana Kusini mwa Tanzania (Lindi) na tayari timu ya watalaam wetu iko huko. Sampuli zimechukuliwa kutoka kwa wagonjwa na kuonyesha kuwa siyo ugonjwa wa Ebola, Maburg wala Uviko19,” amesema Waziri Ummy.

Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imekubali ombi kutoka Shirikal la Afya Duniani (WHO) na kutoka Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa (CDC) kutoka Serikali ya Marekani ili kuongeza nguvu kwenye timu ya wataalam katika kubaini ugonjwa huo.

Julai 12, akihutubia Mkutano wa 20 wa Shirikisho la Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati (Amecea) Rais Samia Suluhu Hassan alisema kuna ugonjwa mpya umeingia katika mikoa ya Kusini ambapo baadhi ya watu wanatokwa damu puani na kuanguka.

Kufuatia ugonjwa huo watu watatu wamefariki dunia kati 13 waliougua mkoani Lindi ambapo moja ya dalili zake ni kuvuja damu puani.