Ugonjwa wa akili washtua

Muktasari:

  • Zama hubadilika na kupita. Zamani iliwezekana kumuelezea mtu mwenye tatizo la afya akili kuwa amepatwa na hali hiyo kutokana na msongo wa mawazo, matumizi ya dawa za kulevya au vilevi. Lakini wapo pia waliohusisha na imani za kishirikina.


Dar es Salaam. Zama hubadilika na kupita. Zamani iliwezekana kumuelezea mtu mwenye tatizo la afya akili kuwa amepatwa na hali hiyo kutokana na msongo wa mawazo, matumizi ya dawa za kulevya au vilevi. Lakini wapo pia waliohusisha na imani za kishirikina.

Hata hivyo, tangu dunia ikumbatie utandawazi na uvumbuzi wa teknolojia ya habari na mawasiliano hasa ujio wa mitandao ya kijamii, teknolojia hiyo pamoja na mengi mazuri, sasa inaelezwa kuwa kichocheo kimojawapo cha baadhi ya watu hususan vijana kupatwa na tatizo la afya ya akili, ambalo linapofika hatua ya juu zaidi pasipo mhusika kupata matibabu linaweza kumfanya kuwa kichaa.

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani ambayo hufanyika Oktoba 10 kila mwaka, wataalamu wa afya ya akili na wanasaikolojia wamechambua kwa kina hali hiyo, huku takwimu zikionyesha katika kila Watanzania wanne, mmoja ana tatizo la afya ya akili.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu maadhimisho hayo ambayo mwaka huu yana kauli mbiu isemayo: ‘Afya ya akili katika ulimwengu usio sawa,’ mtaalamu wa afya ya akili na mwanasaikolojia kutoka Taasisi ya Mental Health Tanzania, Semeni Lukaga, alisema wapo wanaoathirika kupitia mitandao ya kijamii kwa kuangalia maisha ya watu wengine kwa namna wanavyoweka picha mitandaoni kuhusu maisha yao na namna wanavyofanya starehe.

“Wapo ambao hawaonyeshi wazi kuathirika, lakini wanaanza kuumia akili kwa kuona kwamba wao wana maisha duni, hawajafanikiwa na maisha yamewapiga, hivyo wanaanza kupata msongo wa mawazo na hatimaye kupata tatizo la afya ya akili, kumbe yule mtu si maisha yake halisi,” alisema.

Aidha, Lukaga alisema unaweza kumtambua mtu mwenye tatizo la afya ya akili kupitia maandishi yake mitandaoni au namna anavyotoa maoni katika kurasa mbalimbali.

“Wanaotoa lugha mbaya kwa wengine mara zote wameathirika kiakili. Asili ya binadamu mara nyingi anapokuwa ameathirika kisaikolojia kila anachofanya ni mihemko, ndiyo maana tunashauri ukiwa na furaha usifanye maamuzi na ukiwa na huzuni hali kadhalika.

“Kila mtu ajipime, ukiona huwezi kupita mtandaoni bila kudhihaki watu, kutukana, kushambulia viongozi au watu mashuhuri, wewe upo vizuri katika afya yako ya akili. Kinyume chake tafuta mtaalamu wa saikolojia ili upate tiba,” alisema Lukaga.

Alisema baadhi ya watu wana matarajio fulani katika maisha yao, yanapotoweka huanza kuathirika katika afya ya akili.

“Mtu huyu amekuwa na matarajio katika maisha yake, lakini hakufikia ndoto hivyo anamuona kila mtu ni sababu ya yeye kutofanikiwa. Mitandao ndiyo itamsukuma zaidi ataanza kuzomea wengine kwa kutumia maandishi kwa lengo la kuwaumiza,’’ alisema.

“Hawa namna ya kuwadhibiti huwa ni changamoto, kwani wengi wanahisi kwamba ni sehemu salama kwao kutoa dukuduku lao, wakiamini hakuna atakayewabaini lakini pia hawana pa kusemea.’’

Alitolea mfano wa vijana wanaomaliza masomo wakakosa ajira au hawakuweza kujiajiri, hawa wengi wao wanakuwa wameathirika katika afya ya akili.

Alisema vijana wa aina hiyo wamekuwa na hulka ya kushinda mitandaoni, hivyo wamekuwa wakiendelea kuumia kiakili na wengi wao huishia kuwaumiza watu wengine kwa maoni yasiyofaa au yasiyo na maadili.

Mwanasaikolojia Josephine Tesha alisema mitandao ya kijamii inachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa tatizo la afya ya akili.

“Mitandao ni kitu kigeni, watu wazima miaka 30 hadi 40 tumekua bila mitandao ya kijamii. Ukiangalia watoto wa siku hizi hata ukiwaweka kwenye kundi la watu, kuna tofauti sana jinsi tulivyokuwa na walivyo.”

Alitaja matumizi ya simu na namna wazazi wasivyoelewa athari za kuwaachia watoto kifaa hicho ikiwamo kukosa maadili.

“Vijana wengi wanapenda kuwafuatilia watu maarufu na mabinti ndiyo wanaumia zaidi upande huo bila kujua kwamba wale wanaigiza maisha, wanafanya biashara lakini wao wanahisi ndiyo maisha halisi, wengi wanajikuta wanaishi maisha wanayoishi wengine.”

Utajuaje kama umeathirika?

Lukaga alisema unaweza kumtambua mtu mwenye matatizo katika afya yake ya akili kwa kumtazama katika mapokeo yake iwe katika mazungumzo au maamuzi pindi linapotokea jambo lolote.

“Kuna watu ukimwambia jambo kwa nia nzuri, lakini yeye atalipokea kwa kukasirika na wakati mwingine mnaweza hata kugombana,” alisema.

Alitaja athari nyingine kuwa mhusika atapokea mabadiliko kwenye mzunguko wake wa damu, kupata shinikizo la damu, kupoteza hamu ya kula.

“Athari nyngine ni pamoja na kuzalishwa kwa wingi kwa homoni za hasira, mtu anaweza kuhisi homa, akapata msongo wa mawazo na wengine wanakula sana,” alisema.

Alisema wengi huanza kukosa usingizi wa kutosha na hayo yote huchangamana kwa pamoja na mtu huanza kupoteza nuru katika ngozi.

Ukubwa wa tatizo

Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk Omary Ubuguyu alisema idadi ya wagonjwa wa akili imekuwa ikiongezeka, mwaka hadi mwaka.

“Mwaka 2018 tulikuwa na wagonjwa 357,799 waliokwenda kupatiwa matibabu, 2019 walikuwa 380,000, mwaka 2020 walifika zaidi ya 500,000,” alisema.

Hata hivyo, takwimu za wagonjwa kwa mwaka 2020 zimejumuisha na takwimu za hospitali za kanda na Taifa, takwimu za awali zilikuwa hazijajumuishwa.

Pia, alisema takwimu walizonazo ni wagonjwa wanaofika hospitalini kupatiwa matibabu, huku ikielezwa kuwapo kwa uwezekano mkubwa wa wagonjwa walioko mitaani, kutokana na jamii kuwa na uelewa mdogo kuhusu afya ya akili.

Undani magonjwa ya akili

Dk Ubuguyu alisema kuna magonjwa zaidi ya 340 ya akili yaliyogawanywa katika makundi tofauti.

“Kwa kiasi kikubwa magonjwa ya akili yanahusishwa na kupotea kwa nguvukazi, kwa kuwa magonjwa haya yasipotibiwa kwa wakati, wagonjwa wengi hushindwa kurudi kwenye uwezo wao na hivyo kuathiri uwezo wa uzalishaji.

Kwa jumla magonjwa ya akili yanachangia kwa zaidi ya asilimia 40 ya athari za kiafya kwa mtu mmoja mmoja na jamii,’’ alisema.

“Hii inamaanisha kuwa, jamii yetu inapaswa kuwekeza kwenye afya ya akili kwa kiasi kikubwa zaidi. Uwekezaji katika afya ya akili haulengi tu katika kutibu wale wenye mahitaji, lakini unalenga katika kuimarisha afya ikiwamo udhibiti kwenye matumizi ya vilevi kama pombe na sigara, kufanya mazoezi, lishe bora na kuimarisha uhusiano kwenye jamii,” alisema Dk Ubuguyu.