Prime
Ugumu wa kudhibiti rushwa barabarani -2

Muktasari:
- Rushwa katika sekta ya usafiri inasababishwa na mnyororo wa wahusika, wakiwemo maafisa wa polisi.
Dar es Salaam. Licha ya madai ya kukithiri vitendo vya rushwa katika sekta ya usafiri na usafirishaji hasa daladala, wadau wameonyesha kuwapo mazingira magumu ya udhibiti wa vitendo hivyo.
Kwa mujibu wa wadau hao, ugumu unatokana na kuwapo mnyororo mrefu wa vitendo hivyo ukiwahusisha baadhi ya wanaodaiwa kuwa watu wazito ndani ya Jeshi la Polisi.
Mbali ya hilo, inaelezwa kuwa zipo changamoto za kisheria ambazo ni kikwazo cha udhibiti wa vitendo vya rushwa katika sekta ya usafiri na usafirishaji.
Hata hivyo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhan Ng’anzi anasema udhibiti wa rushwa katika sekta hiyo pamoja na mbinu nyingine unapaswa kuanza kwa wamiliki wa daladala kuhakikisha hawana makosa.
“Kama gari lako halina makosa, uko vizuri unatembea barabarani, askari atakusimamishaje au unawezaje kutoa rushwa wakati unajua huna kosa. Wanaotoa rushwa ni wale wanaojua wana makosa kwa hiyo ili kukwepa faini wanakubali kutoa rushwa,” anasema Ng’anzi.
Ingawa Kamanda Ng’anzi anasema askari atakayebainika kula rushwa atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwamo kufukuzwa kazi, anasisitiza umuhimu wa wamiliki wa magari kuhakikisha vyombo hivyo havina makosa ili kuepuka kujiweka katika mazingira ya kuombwa rushwa.
Anasema hakuna trafiki atakayekusimamisha iwapo huna kosa na hata mwenye gari hatatoa rushwa iwapo anajijua si mkosaji.
Kwa mujibu wa madereva na makondakta waliozungumza na Mwananchi, huona sawa kutoa Sh2,000 hadi Sh5,000 kukwepa kutoa Sh30,000 za faini kwa kosa la usalama barabarani baada ya kukamatwa na trafiki.
Baadhi ya madereva wanasema hulazimika kutenga kati ya Sh10,000 na Sh14,000 kwa siku kwa ajili ya kuwapa trafiki wanapokamatwa barabarani ili kuwezesha kazi zao kufanyika vizuri.
Kwa nini makosa kwa daladala
Magari mengi, hasa daladala hukutwa na makosa ya usalama barabarani kwa sababu ya kutofanyiwa matengenezo kama inavyoelezwa na Mkuu wa Idara ya Taaluma ya Usafirishaji na Biashara wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dk Prosper Nyaki.
Anasema kila aina ya gari lina maelekezo kutoka kwa mtengenezaji juu ya lini linapaswa kufanyiwa matengenezo.
Dk Nyaki anasema wazalishaji wa gari huelekeza yanapotembea umbali fulani yanapaswa kubadilishwa vilainishi na tairi.
Changamoto iliyopo kwa wamiliki wa daladala anasema wengi hawafuatilii maelekezo ya kitaalamu kuhusu matengenezo madogo ya magari husika, hivyo mengi ni mabovu.
"Mengi yanatembea yakiwa na ubovu kwa sababu wanaoyatumia hawazingatii maelekezo ya kitaalamu kuhusu matengenezo, hali hii inasababisha ukikagua ulikute na kasoro," anasema.
Hata hivyo, anaeleza ubora wa gari linalopaswa kutembea barabarani haupimwi kwa macho pekee, bali ni kufungua baadhi ya vitu, mathalani kujua iwapo vilainishi vipo na vinapaswa kuendelea kutumika.
Katika mazingira ya kutozingatiwa kwa matengenezo ya daladala, Dk Nyaki anasema ndipo madereva na makondakta wanajikuta wakiingiwa hofu ya kusimamishwa na trafiki wakijua watakutwa na makosa.
Kuhusu sheria
Sheria ya Usalama Barabarani imeainisha makosa mengi yanayoweza kutendeka barabarani, wasimamizi wa utekelezaji wa sheria hiyo wakiwa Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani.
Kikosi hicho kimepewa wajibu wa kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usalama Barabarani.
Mbali ya hilo, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 3 ya mwaka 2019.
Sheria hii ilifuta sheria ya iliyokuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
Latra imepewa jukumu la kudhibiti sekta ya usafiri ardhini, hususan usafiri wa mizigo, abiria (mabasi ya njia ndefu, mabasi ya mijini, magari ya mizigo, teksi, pikipiki za magurumu mawili na matatu) na usafiri wa reli.
Katika utekelezaji wa majukumu yake Jeshi la Polisi na Latra, baadhi ya wadau wanaeleza kumekuwa na mgongano.
Mmoja wa wadau aliyewahi kufanya kazi Latra (aliyeomba hifadhi ya jina lake) anadai Sheria ya Latra kuanzia kifungu cha 5(1) D na kuendelea, kinaitambua mamlaka hiyo kama mratibu wa shughuli zote za usalama barabarani na siyo polisi.
Anasema vifungu hivyo vinaeleza Latra itaajiri wafanyakazi wote wa sekta ya barabara na reli, yaani hadi makondakta na madereva.
Pia, vinaipa Latra mamlaka ya kufanya ukaguzi wa magari yote ya biashara badala ya polisi.
Anasema kuna changamoto katika Sheria ya Usalama Barabarani, inayompa polisi mamlaka ya kutoa leseni lakini huyohuyo ndiye anayekagua.
Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Deus Sokoni anasema sheria ya usalama barabarani ndiyo msingi wa usimamizi wa shughuli zote za usalama barabarani na inapaswa kusimamiwa na polisi kama ilivyoelezwa ndani yake.
“Sheria ya usalama barabarani ndiyo inayomtambua askari polisi kusimamia usalama barabarani na siyo mamlaka nyingine au mtu mwingine,” anasema.
Kwa mujibu wa Sokoni, majukumu na shughuli za Latra zimetajwa katika sheria ya kuanzishwa kwake, lakini siyo kusimamia masuala ya usalama barabarani.
Anasisitiza sheria ya usalama barabarani inasimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani, kupitia Jeshi la Polisi na ndani yake jeshi hilo limetajwa.
Katika sheria hiyo, anasema Latra imetajwa ndani ya kifungu cha 44 kama mamlaka ya udhibiti.
Kwa upande wake, mwanataaluma wa usalama barabarani, Henry Bantu anasema changamoto zote zinazoikabili sekta ya usafiri na usafirishaji zinasababishwa na kutotekelezwa sheria inavyopaswa.
Bantu anasema sheria ya usalama barabarani na nyingine zote zinazosimamia eneo hilo, hazina tatizo bali matatizo wanayo wanaopaswa kuzitekeleza.
“Tatizo la utekelezaji linaanza na uelewa, tuna changamoto kubwa ya uelewa wa sheria kwa wananchi, ndiyo sababu wanajikuta watumwa wa sheria na wanashindwa kuitekeleza,” anasema.
Bantu anasema kuna umuhimu wa kuhakikisha elimu inatolewa ili wananchi waijue sheria husika, akieleza kufanya hivyo kutawawezesha kutambua namna ya kuitekeleza.
Anasisitiza wanaoona kuna changamoto za kisheria, pengine hawajaelewa.
Kauli ya Latra
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Latra, Salum Pazzy anasema kazi ya ukaguzi wa ubovu wa magari ni jukumu la polisi kupitia Sheria ya Hali ya Ukaguzi.
“Polisi ndio wanaohusika kukagua uzima wa gari na siyo Latra, kwani hata sisi gari ikiwa mbovu tunawahusisha wao kwa kuwa ndio wana utaalamu katika eneo hilo,” anasema Pazzy.
Baada ya Latra kutoa leseni ya gari kuingia barabarani, Pazzy anasema mmiliki anaandikiwa barua ya kuipeleka polisi kwa ajili ya kukaguliwa, kisha ataruhusiwa kuanza safari.
Katika utoaji wa leseni hiyo, anasema kinachozingatiwa ni idadi ya viti vya gari kulingana na safari kwa upande wa daladala, huku mabasi makubwa wanazingatia madaraja.