Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ushirika wa rushwa Trafiki, madereva wa daladala-1


Muktasari:

  • Chama cha Madereva na Makondakta chasema hakina malalamiko rasmi ya rushwa, trafiki yatoa kauli, Takukuru ikitoa onyo.

Dar es Salaam. “Ukiwa dereva wa daladala Dar es Salaam unawatumikia mabosi wawili; kwanza mmiliki wa gari na pili, trafiki.”

Ni kauli ya Bosco Joram (si jina halisi), dereva wa daladala linalofanya safari kati ya Buyuni Chanika na Ubungo Simu2000.

Malalamiko ya Joram yanatolewa na idadi kubwa ya madereva na makondakta wa daladala wakidai kuombwa rushwa kwa maelezo ya fedha za kubrashia viatu.

Kondakta akimpatia rushwa trafiki jijini Dar es Salaam. Picha na Mpiga Picha Wetu

Wameeleza hulazimika kila siku kutenga fedha kwa ajili ya askari wa usalama barabarani maarufu kama trafiki, ili kukwepa kutozwa faini ama kwa makosa ya usalama barabarani yanayohusu vyombo wanavyoendesha au wakati mwingine pasipo kosa lolote.

Uchunguzi wa Mwananchi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam umebaini madereva hao huwasilisha kwa wenye magari hesabu ya kati ya Sh80,000 hadi Sh200,000 kwa siku kutegemea ukubwa wa gari na umbali wa safari.

Mbali ya hilo, hutenga fedha kwa ajili ya mafuta na kiasi kinachosalia hugawa fungu kwa ajili ya posho yao na ya trafiki, ili kuwezesha siku kuisha vema.

Joram amesema hutenga kati ya Sh10,000 na Sh15,000 za kuwapa trafiki, akieleza maeneo ambayo hulazimika kuwa makini ni Vingunguti na Kipawa ambako mara nyingi trafiki husimama katika Barabara ya Nyerere. Iwapo akisimamishwa huacha Sh2,000 kwa trafiki aliyemkamata.

“Suala la kutoa hela haliwezi kwisha kwa kuwa usipofanya hivyo wanakuandikia faini. Sasa kama una kosa la kuandikiwa faini Sh30,000 halafu uone ubahili wa kutoa Sh2,000! Hiyo hapana," amesema Joram, mtazamo ambao pia wanao madereva wengine.

Saleh Kassim, dereva wa daladala kati ya Chanika-Gongo la Mboto amesema trafiki hukubali Sh2,000 kwa kosa lisilozidi faini ya Sh30,000, lakini ukiwa na zaidi ya moja wanakutaka kupeleka gari kituoni.

"Ukikamatwa ndiyo umetoka kuamka au umetoka gereji, unamwambia sina kitu nikirudi nitakucheki. Ukirudi unamalizana naye, ukijidai umesahau anakukamata," amesema akiainisha maeneo ambayo tafiki husimama kuwa ni Videte (Chanika), Magenge, Mapensheni na Shule ya Msingi Pugu.

Kwa wastani amesema hutumia Sh10,000 kwa ajili ya trafiki, kauli inayoungwa mkono na John Gabriel, anayefanya kazi kati ya Stesheni na Mbande.

Miraji Kiboko, dereva wa daladala kati ya Homboza na Machinga Complex, amesema wanapokutana na askari kutoka Makao Makuu ya Trafiki kiwango hupanda hadi Sh5,000.

"Kama ulishawahi kuona askari wanakuwa wengi kituoni, wakati mwingine wameegesha gari pembeni, ukikamatwa na hao ujue Sh5,000 itakuhusu, hawapokei Sh2,000," amesema.

Kondakta aliyejitambulisha kwa jina moja la Samson, anayefanya kazi katika daladala la Kigogo –Kivukoni akijibu swali ni kwa vipi askari atajua kwamba alishalipa fedha amesema: “Wanajua magari yote ya njia wanayopangiwa, hivyo kama kituoni wapo watatu, ujue kabisa wanaambiana yule mimi tayari nishachukua, hivyo hawakukamati.”

Nassor Imran, dereva wa daladala kati ya Tegeta Nyuki na Mwenge amesema mapato kwa siku ni kati ya Sh130,000 na Sh180,000 ikitegemea idadi ya abiria na unafuu wa msongamano barabarani.

Amesema Sh100,000 huzipeleka kwa mmiliki wa gari kila siku bila kujali limefanya kazi au la, huku akitenga Sh14,000 kwa ajili ya trafiki barabarani.

Kutokana na mazingira hayo, ameeleza kuna wakati hushindwa kugawana posho na kondakta wake, ingawa zipo siku hupata kiasi cha kuridhisha.

Baadhi ya madereva wamesema hubakiwa na wastani wa Sh40,000 ambazo hugawana na kondakta.

"Hii inategemea na biashara ilivyokuwa siku hiyo, ikiwa mbaya kati ya Sh25,000 hadi 20,000, hatukosi kwa siku kurudi nayo nyumbani," amesema mmoja wa madereva.

Nelson Manda, kondakta wa daladala katika njia hiyo amesema kuna wakati hulazimika kutoa fedha kwa trafiki hata kama hakuna kosa la usalama barabarani au kuhusu gari.

"Gari halina kosa, kama la kwangu ni jipya bosi kakamilisha taratibu zote, lakini kwa askari lazima utoe fedha," amesema.

Suala la rushwa kwa askari wa usalama barabarani, kwa mujibu wa mmoja wa madereva katika njia hiyo, lina mkono mrefu hivyo ni vigumu kudhibitiwa.

"Siku hizi tunawapa Sh2,000 hadharani hawajifichi, kwa nini hawajifichi ni kwamba mabosi zao wamehalalisha wanajua hakuna wa kuwafanya lolote," ameeleza.


Barabara ya Morogoro

Baadhi ya madereva na makondakta wanaofanya safari kati ya Mbezi na Mlandizi wamesema ukiacha maeneo mengine kwenye Barabara ya Morogoro, vituo maalumu vya kuacha hela kwa trafiki ni Kibamba kwa Mangi na Magari Saba.

Wameeleza kuanzia saa 1.30 asubuhi hadi saa sita mchana katika vituo hivyo daladala husimama na kuacha Sh2,000 kwa trafiki wanaokuwapo hapo.

"Huo ndiyo utaratibu, hauwezi kuukwepa kama ni konda au dereva wa daladala, ukishatoa Sh2,000  basi unafanya kazi kwa amani siku nzima, labda itokee tu umefanya kosa," amesema dereva wa daladala, James Peter.

Mwandishi wa Mwananchi aliyepiga kambi kituo cha Kibamba kwa Mangi asubuhi ya Ijumaa Julai 19, 2024 kati ya saa 2.00 na saa 3.00 alishuhudia trafiki watatu wakichukua fedha kutoka kwa madereva na makondakta wa daladala zilizotokea Mlandizi kwenda Mbezi.

Baada ya kushusha abiria, kondakta aliyekunja fedha kwenye tiketi, alikwenda upande wa dereva na kumkabidhi trafiki ambaye wakati huo alikuwa akizungumza na dereva.

Kituo cha Magari Saba, siku hiyo ya Ijumaa, Julai 19, 2024 saa 4.00 asubuhi walikuwapo trafiki wawili, mmoja akiwa amevaa koti la bluu na suruali ya kaki.

Dereva wa daladala alipomuona kabla hajasimama alimweleza kondakta kuna ‘kimeo.’

"Huyu (akimaanisha askari aliyevaa koti la bluu) huwa hakubali kupokea Sh2,000 kama wengine,” ameeleza dereva huyo katika mazungumzo na kondakta.

Baadaye alisimamisha daladala lingine, Mwananchi ilishuhudia trafiki huyo akipokea Sh5,000.

Dereva aliyejitambulisha kwa jina moja la Rashid amelieleza Mwananchi kwamba trafiki huyo hulazimisha kupewa Sh5,000 hadi Sh10,000 na usipompatia siku hiyo huwezi kufanya kazi kwa raha.

"Tunatoa mara moja kwa siku, ingawa kuna askari wanalazimisha Sh5,000, lakini mara nyingi tunaacha Sh2,000 miaka minne iliyopita ilikuwa ni wajibu kuitoa na trafiki hawakuona aibu kuchukua, kidogo kipindi hiki wanachukua kisirisiri, lakini huwezi kupita asubuhi Magari Saba au Kwa Mangi bila kuacha pesa hiyo," amesema.

John Tarimo, dereva wa daladala kati ya Gongo la Mboto na Kawe amesema ili abiria asione mara nyingi huenda nyuma ya gari na fedha hutolewa mkononi au hukunjwa kwenye tiketi. Trafiki humpa risiti kondakta, ili kuonyesha kaandikiwa faini.

Dereva wa daladala zinazotoa huduma kati ya Buza na Mwenge, Said Rashid amesema fedha hizo trafiki husema ni kwa ajili ya kubrashi viatu.

“Ukianza safari Buza Kwalulenge kituo cha kwanza unasimamishwa na askari kwa Mama Kibonge, Temeke Usalama, halafu ukifika Tabata Mwananchi unawakuta, kisha utawakuta  Ubungo River Side na Mpakani Mwenge. Kila kituo lazima uache Sh2,000,” amesema.

Jackson Masia, dereva wa daladala kati ya Mnazi Mmoja hadi Simu2000 kupitia Buguruni amesema:“Kuna wakati wanadiriki hata kunyang’anya ufunguo wa gari, kisa wamenyimwa Sh2,000 na wanatutukana hadharani na abiria wanasikia wanapotoa maneno ya fedheha.”

“Nyakati za asubuhi abiria wanataka kuwahi kwenye majukumu yao, lakini wanakusimamisha pembeni wanazunguka nyuma kama hujawafuata wanakuchukulia kuwa una kiburi hutaki ushirikiano,” amesema.


Kauli ya Darcoboa

Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Shifwaya Lema akizungumzia na Mwananchi amesema kama chama hawajawahi kupokea malalamiko kutoka kwa madereva.

“Hao ni madereva waliosema, inawezekana ni sahihi kwa sababu wao ndio wako kazini, lakini siwezi nikakubali wala kukataa kwa sababu hakuna anayesema moja kwa moja,” amesema.

Amesema licha ya chama hicho kusikiliza kero za madereva na makondakta, suala hilo halijawahi kufikishwa kwenye vikao kama hoja rasmi.

“Hoja ikiletwa huwa tunakaa tunaijadili kwa pamoja na kama kuna changamoto tunaitatua. Kwa bahati nzuri wakileta hoja zao, huwa kuna mfumo tunao kama ni Jeshi la Polisi tunaongea nao, lakini mpaka sasa hazijaletwa hoja na kwa kuwa hazijaja, siwezi kuvalia njuga hoja ambayo haijaja,” amesema.


Wasemavyo trafiki

Akizungumzia tuhuma hizo za rushwa, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhan Ng’anzi amekiri kusikia malalamiko ya madereva na makondakta kuhusu vitendo hivyo.

Amesema jeshi hilo lipo makini kufanya uchunguzi kubaini askari yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa, ili achukuliwe hatua za kinidhamu, ikiwemo kufukuzwa kazi.

Hata hivyo, amesema anatambua juu ya uwepo wa baadhi ya askari wasio waadilifu, hivyo wanajihusisha na vitendo vya rushwa licha ya kuzuiwa na kanuni na taratibu za kazi zao.

Amesema kuna ugumu wa kupambana na vitendo hivyo unaosababishwa na kukosekana ushahidi wa moja kwa moja, ambao kimsingi ndiyo utakaomtia mtendaji hatiani.

“Inaonekana kama pande zote mbili zina masilahi kati ya mtoa rushwa na mpokeaji, kwa sababu wanajificha inakuwa ngumu kupata ushahidi,” amesema.

Wakati wowote atakapobainika askari anayejihusisha na vitendo hivyo kwa mujibu wa Ng’anzi, hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.

Amesema hatua hiyo haitakuwa mara ya kwanza, kwani wapo askari kadhaa waliowahi kuadhibiwa, ikiwemo kufukuzwa kazi kwa vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa fedha.

Alipoulizwa kuhusu vitendo hivyo kuhusishwa na viongozi wa jeshi hilo, amesema jukumu lao ni kusimamia sheria na watahakikisha hilo linatekelezwa wakati wote.

Kamanda Ng’anzi amesisitiza yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo na ukapatikana ushahidi atachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria.


Takukuru yaonya

Akizungumza na Mwananchi Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Salum Hamduni amewaonya madereva na makondakta akiwataka kuepuka kutoa rushwa kwa trafiki kwa sababu nao wanaingia mtegoni.

“Suala la rushwa lina sehemu mbili, lina mtoaji na mpokeaji, kama madereva wanatoa maana yake kuna makubaliano kati yao na wapokeaji.

“Nawashauri hao madereva wasitoe rushwa, badala yake wakiombwa au kushawishiwa, watoe taarifa kwa viongozi wa Jeshi la Polisi au Takukuru, ili hatua zichukuliwe,” amesema.

Amesema wamekuwa wakifuatilia vitendo hivyo na kuchukua hatua pale wanapobaini makosa.

“Kuna hatua mbalimbali sisi kama taasisi tunachukua, kwa kuendelea kutoa elimu kwa Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani juu ya madhara ya rushwa,” amesema na kuongeza:

“Pia tumetoa taarifa nyingi ambazo wamechukuliwa hatua, wamefukuzwa kazi na wengine pia mafaili yao yamefikishwa mahakamani,” amesema.


Itaendelea kesho.


Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917