Uhaba wa rasilimali kikwazo kwa wadau wa ulinzi wa watoto
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa akizungumza katika semina iliyohusisha taasisi takribani 100 za watetezi wa haki za binaadamu iliyofanyika leo Julai 23, 2026 jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Watetezi wa haki za watoto nchini wameonya kuwa uhaba wa rasilimali, ikiwamo fedha, wataalamu, miundombinu na ushirikiano kati ya taasisi, unadhoofisha juhudi za kulinda watoto.
Dar es Salaam. Watetezi wa haki za watoto nchini wamesema kutokuwepo kwa rasilimali za kutosha kufadhili shughuli za ulinzi wa haki za watoto kunatishia juhudi za kulinda kizazi kijacho, wakisisitiza kuwa uwekezaji kwa watoto ndiyo msingi wa maendeleo endelevu ya taifa.
Hayo yameelezwa na wadau mbalimbali walioshiriki katika semina iliyohusisha taasisi takribani 100 za watetezi wa haki za binadamu iliyofanyika leo Juni 23, 2026 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa amesema moja ya changamoto inayokabili watetezi wa haki za binadamu kwa sasa ni kupungua kwa rasilimali za kifedha kutokana na mabadiliko ya vipaumbele vya wafadhili duniani.
Amesema katika mkutano mkuu wa 15 wa mtandao huo wa watetezi wa haki za binadamu unaotarajiwa kufanyika kesho utajadili kwa kina athari za upungufu wa rasilimali hizo na kuweka mikakati ya kuhakikisha kazi za utetezi zinaendelea bila kuyumbishwa na mabadiliko ya mazingira ya ufadhili.
"Tutatafakari kwa pamoja namna ya kupata rasilimali mbadala na jinsi ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau ili kuhakikisha watetezi walioko mashinani wanaendelea kuwafikia watoto wanaohitaji msaada," amesema.
Amesisitiza Tanzania haiwezi kufikia maendeleo ya kiuchumi na kijamii ikiwa haitaweka mkazo katika kulinda na kuendeleza watoto, ambao ni takribani nusu ya idadi ya watu nchini.
"Ikiwa tunataka Tanzania ya miaka 20 ijayo iwe na watu wenye elimu, wanaoheshimu haki za binadamu na wenye uwezo wa kuzalisha, lazima tuanze kuwekeza kwa watoto leo. Taifa lisilowekeza kwa watoto linaweka rehani maendeleo yake ya baadaye," amesema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Mratibu wa Kliniki ya Msaada wa Kisheria ya chuo hicho, Veronica Buchumi (kushoto) akiwasilisha mada wakati wa semina iliyohusisha taasisi takribani 100 za watetezi wa haki za binaadamu iliyofanyika leo Julai 23, 2026 jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Mratibu wa Kliniki ya Msaada wa Kisheria ya chuo hicho, Veronica Buchumi amesema Tanzania ina mfumo imara wa sheria unaolinda haki za watoto ukiongozwa na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 kwa Tanzania Bara na Sheria ya Watoto ya mwaka 2011 kwa Zanzibar.
Buchumi amesema sheria hizo ndizo msingi wa ulinzi wa mtoto nchini, lakini zinasomwa na kutekelezwa sambamba na sheria nyingine zinazochangia kuimarisha haki na usalama wa watoto.
Amesema pamoja na uwepo wa sheria hizo, utekelezaji wake unapaswa kuzingatia mazingira halisi ya jamii kwa kuwa watoto wanaishi katika mazingira yanayotofautiana kiuchumi, kijamii na kitamaduni.
Mhandhiri kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Zachayo Shigongo amesema kufanikiwa katika kuimarisha ulinzi wa mtoto nchini kunategemea ushirikiano wa taasisi za Serikali, wataalamu na wadau wengine wanaohusika na ustawi wa mtoto.
Shigongo ametaja miongoni mwa taasisi hizo kuwa ni Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu inayosimamia sera na miongozo ya ulinzi wa mtoto, pamoja na Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto linaloratibu na kushughulikia mashauri yanayohusu watoto.
Pia, amesema Idara ya Ustawi wa Jamii, yenye maofisa waliopo katika mikoa, wilaya na halmashauri mbalimbali nchini, ina jukumu la kupokea na kufuatilia kesi zinazohusu watoto kwa kuzingatia taaluma, maadili na taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha maslahi bora ya mtoto yanalindwa.