Uingereza yasaini mkataba kusaidia sekta ya afya nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya,  Zanzibar, Fatma Mrisho (kulia) Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya (katikati) Dk Seif Shekalaghe na kushoto Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar.

Muktasari:

  • Baada ya kupokea misaada mbalimbali kutoka Uingereza kwa miongo kadhaa Serikali ya Tanzania imesaini hati ya makubaliano na Serikali hiyo kwa ajili ya kusaidia huduma mbalimbali za afya Tanzania Bara na Zanzibar.

Dar es Salaam. Serikali imesaini hati ya mkataba wa ushirikiano kati yake na Uingereza kwa ajili ya kusaidia huduma za afya katika maeneo mbalimbali ikiwemo tafiti, magonjwa ya milipuko na tiba.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Mei 18, 2023 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe, mara baada ya kusaini makubaliano hayo na serikali ya Uingereza kupitia Diaspora ambao walianzisha suala hilo na kuishirikisha Wizara ya Afya.

Amesema ushirikiano huo unalenga katika maeneo ya tafiti, mafunzo, tiba na shughuli mbalimbali zinazohusisha afya na zitahusisha taasisi zao.

Amesema huo ni mkataba wa kwanza wa mashirikiano kati ya Wizara ya afya na Uingereza na wamekuwa wakishirikiana kwa muda mrefu bila kuwa na makubaliano ya mkataba kama waliyofanya leo.

"Hii ni hatua muhimu na ni jambo ambalo limekuwepo kwa muda mrefu na hatimaye jambo hilo limekamilika haya ni matunda na matokeo ya ziara tuliyoifanya na wenzangu wiki tatu zilizopita tulipohudhuria mkutano Uingereza,” amesema Dk Shekalaghe.

Aidha, amesema jambo jingine ambalo lipo katika majadiliano na Balozi amekubali kulifanyia kazi ni Uingereza kuingia katika ule mfuko wa pamoja ambao nchi mbalimbali zinachangia kuwezesha kutoa huduma hasa katika ile huduma ya afya ya msingi.

Amesema mazungumzo yameshanza na tayari wameshaandaa timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya ambao watakutana na wataalamu waliopo kwenye ubalozi huo ili kuhakikisha Uingereza inakuwa mojawapo ya nchi zinazochangia.

Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar, amesema kwa mujibu wa mkataba huo, nchi yake itachangia zaidi katika magonjwa mbalimbali yakiwemo yale ya kuambukiza, yasiyo ya kuambukiza na yale ya mlipuko.

Pia amesema watachangia katika masula ya dawa, tafiti na kwamba msaada huo ni kwa ajili ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Kwa upande mwingine Concar amesema wanafikiria namna ya kuanza kuchangia katika mfuko wa pamoja wa afya.

Katibu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Fatma Mrisho amesema watafaidika katika utafiti, maeneo ya huduma za afya kuanzia ngazi ya chini hadi daraja la juu na kujenga miundo ambayo itawasaidia kuendesha huduma zao kwa ubora Zaidi.

Amesema Zanzibar imekubaliana kuwepo na bima ya afya kwa wote, hivyo wataomba kusaidiwa katika hilo ili kila mmoja aweze kupatiwa huduma za afya.

Mrisho amesema jambo jingine wanalolitegemea katika makubaliano hayo ni kuwapeleka wataalamu kwa ajili ya kusoma ili kuwajengea uwezo, lakini pia kupatiwa vifaa vya kisasa vitakavyosaidia kuboresha huduma.