Ujasiriamali kupambana na taka za plastiki Ziwa Victoria

Wadau wa mazingira wakifanya maonyesho ndani ya moja ya mabanda yaliyojengwa na Shirika la Emedo kutokana na chupa za plastiki zilizokusanywa kutoka ndani ya Ziwa Victoria. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Mashirika kadhaa binafsi yanashirikiana kuwajengea uwezo wanawake na vijana kutumia plastiki zilizotumika kutengeneza bidhaa zenye manufaa kwa jamii kuepuka kuchafua Ziwa Victoria.


Mwanza. Shirika la Emedo kwa kushirikiana na wadau wa mazingira limeanzisha kampeni ya kupambana na uchafuzi wa mazingira ndani ya Ziwa Victoria kudhibiti taka za plastiki zinazoendelea kuongezeka.

Kampeni hiyo inayoitwa pambana na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na taka za plastiki inatekelezwa katika mikoa ya kanda ya ziwa ili kuyanusuru maisha ya viumbe wa majini.

"Taka za plastiki zinazokusanywa ndani ya ziwa kama vile ndala zilizoisha, mifuko na chupa za plastiki tunazitumia kutengenezea bidhaa kama mapambo, viti, boti na banda linaloweza kutumika kwa huduma za mgahawa kama tulilolijenga hapa Kamanga," amesema Editrith Lukungu, mkurugenzi mtendaji wa shirika binafsi la uhifadhi wa mazingira nchini.


Ili kuongeza ufanisi Editrith amesema, ujuzi na motisha kwa jamii kuhusu njia mbadala ya uhifadhi wa mazingira zinahitajika. Shirika hilo limeanza kutoa mafunzo ya utengenezaji bidhaa kwa vikundi vya wanawake na vijana katika jamii zinazoishi mwambao wa ziwa hilo.

"Tayari tuna vikundi zaidi ya 50 vya wanawake na vijana ambao tunawafundisha njia na namna ya kutengeneza bidhaa kwa kutumia taka hizi, bidhaa hizo mfano mapambo wataziuza na kujipatia kipato," amesema Lukanga.


Mkuu wa kitengo cha usafi na mazingira Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Ally Salim amesema utafiti uliofanywa mwaka 2015 mkoani Mwanza ulibaini asilimia 20 ya sangara na sato walikutwa na vipande vidogo vya taka za plastiki.

"Taka za plastiki zinazalisha sumu zinazoweza kusababisha samaki wafe. Wakati mwingine inaweza kuathiri kuzaliana kwao," amesema Salim.

Salim amesema uwepo wa taka hizo ndani ya ziwa unachangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa mazalia ya samaki katika  miaka ya hivi karibuni.