Ujenzi bandari ya uvuvi Kilwa, Feri Kigamboni

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega

Muktasari:

  • Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatarajia kuendelea na ujenzi wa bandari ya uvuvi katika eneo la Kilwa Masoko mkoani Lindi, huku ikifanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa soko la samaki Kigamboni.

Dar es Salaam. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024, sekta ya uvuvi itaendelea na ujenzi wa bandari ya uvuvi katika eneo la Kilwa Masoko, mkoani Lindi pamoja na upembuzi yakinifu wa soko la samaki Feri Kigamboni.

Ulega amesema ujenzi huo ni utekelezaji wa  IIani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano (2021/2022 – 2025/2026).

Ulega ameyasema hayo leo Jumanne, Mei 2, 2023 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2023/2024.

Pia amesema Wizara itakamilisha ujenzi wa mialo minne ya Igabiro (Bukoba), Chifunfu (Sengerema), Igombe (Ilemela) na Kayenze (Ilemela) pamoja na vituo vitatu vya usimamizi wa rasilimali za uvuvi vya Sota (Rorya), Simiyu (Busega) na Nyakaliro (Sengerema).

Aidha, serikali itafanya Upembuzi Yakinifu wa ujenzi wa soko la samaki Kigamboni na maeneo nane ya ujenzi wa miundombinu ya Ofisi za Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi (Kigoma, Tanga, Mtwara, Muleba, Kagera, Mtera, Ikola, na Singida).