Ujenzi nyumba za waathirika maporomoko ya Hanang waendelea

Muktasari:

  • Nyumba hizo zinajengwa na Serikali baada ya maporomoko ya matope, mawe na magogo kutoka Mlima Hanang, yaliyotokea Desemba 3, 2023 na kusababisha athari kubwa katika maeneo hayo ikiwemo vifo, majeruhi na kuharibu makazi ya wananchi.

Arusha.Ujenzi wa nyumba 108 za waathirika wa maafa ya maporomoko ya matope, mawe na magogo ya miti kutoka Mlima Hanang unaendelea katika eneo la Gidagamowd, Kata ya Mogitu.

 Nyumba hizo zinajengwa kwa waathirika wa maafa hayo waliopoteza makazi yao na chache kwa wale wanaoishi kwenye mazingira hatarishi.

Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Aprili 20, 2024, Mkuu wa wilaya ya Hanang, Almishi Hazali,amesema ujenzi wa nyumba hizo unaendelea na umefikia usawa wa dirisha  na kuwa unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa Juni, mwaka huu.

“Tunaishukuru Serikali zaidi ya Sh 1.6bilioni zimeshatolewa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo ambazo zinazoendelea kujengwa na kwa mujibu wa mkataba, wanatakiwa kumaliza mwanzoni wa Juni, 2024,”amesema mkuu huyo wa wilaya.

Amesema nyumba hizo zinajengwa na Suma JKT pamoja na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania-Red Cross ambapo kati ya nyumba 108, Suma JKT wanajenga nyumba zaidi ya 70.


Maafa hayo yalitokea Desemba 3, 2023 yalisababisha vifo 89 na majeruhi kadhaa, yaliharibu makazi ya watu, maeneo ya biashara na miundombinu mbalimbali, ikiwemo afya, barabara, umeme na maji.

Nyumba hizo zinajengwa na Serikali na kwa mujibu wa Msemaji wa Serikali, Mobhare Matinyi, Serikali imetenga ekari 100 kwa ajili ya makazi hayo mapya baada ya kupata eneo lilikokuwa shamba la Waret kutoka kwa Jeshi la Magereza.

Eneo hilo lipo Kijiji cha Godagamowl, Kata ya Mogitu wilayani Hanang ambalo ni umbali wa kilomita 4.5 kutoka Barabara kuu ya Babati- Singida na katika eneo hilo, Serikali imepima viwanja 269 kati ya hivyo 226 ni vya makazi na biashara, viwanja 17 eneo la huduma za kijamii kama zahanati, kuzikia, kiwanja cha michezo, eneo la wazi, majengo ya nyumba za ibada viwanja vitatu, ofisi ya kitongoji moja, soko moja na shule ya msingi moja.