Wadau wachangia ujenzi nyumba za waathirika Hanang

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga akipokea msaada kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa kampuni ya EACOP, Catherine Mbatia. Picha na Mpiga picha wetu

Muktasari:

  • Ni baada ya Serikali kutangaza kujenga nyumba 101 za waathirika wa maporomoko ya tope Hanang ndani ya mwezi miezi mitatu.

Hanang. Wadau mbalimbali wamejitokeza kuunga mkono jitihada za Serikali za kujenga nyumba zaidi ya 101 kwa wakazi wa Hanang, mkoani Manyara walioathirika na maporomoko ya tope yaliyotokea Jumapili Desemba 3, 2023.

Kampuni ya Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) leo Jumatatu Januari 8, 2023 imetoa mifuko 1,000 ya saruji ikiwa ni msaada kwa jamii zilizoathirika.

Saruji hiyo itatumika kusaidia ujenzi wa nyumba zaidi ya 101 ambazo Serikali imepanga kuwajengea waathirika wa maafa hayo yaliyoathiri miji ya Katesh na Gendabi.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema msaada huo utakuwa chachu katika ujenzi wa nyumba mpya 101 za waathirika.

"Maafa ya hivi karibuni yaliyotokea katika Wilaya ya Hanang yameziacha jamii zetu katika uhitaji mkubwa, msaada wa ukarimu wa kibinadamu kutoka kampuni ya EACOP umekuja kama mwanga wa matumaini katika nyakati hizi za changamoto.

“Tunashukuru kwa mwitikio na msaada wao katika kusaidia juhudi zetu za kujenga upya na kurejesha maisha ya kawaida ya jamii kutokana na janga hili,” amesema RC Sendiga

Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano wa EACOP Tawi la Tanzania, Catherine Mbatia amesema msaada huo unaonyesha kuguswa kwa kampuni hiyo katika matatizo ya jamii wanayoifanyia kazi.

 "Mchango wetu wa msaada wa kibinadamu ni ushuhuda tosha wa dhamira yetu katika kusaidia wenye uhitaji na unasisitiza dhamira yetu ya uwajibikaji wa kampuni katika jamii,"amesema.

Maafa hayo yamegharimu maisha ya watu ambapo Serikali ilitangaza vifo 89 na kusababisha uharibifu wa mashamba na makazi.

Veronica John ni miongoni mwa waathirika wa mafuriko hayo, amesema msaada huo utasaidia wao kupata makazi yao mapya katika kipindi kifupi kama ilivyoahidi Serikali.

"Napenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa msaada wa EACOP. Msaada uliotolewa utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zinazotukabili, kutoa faraja na ahueni kwa familia zilizoathirika pia utasaidia kuharakisha ujenzi wa makazi mapya,”amesema Veronica.

Kauli ya Serikali

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Januari 5, 2024, Msemaji wa Serikali, Mobhare Matinyi alisema Serikali imetenga ekari 100 kwa ajili ya makazi hayo mapya baada ya kupata eneo lililokuwa shamba la Waret kutoka kwa Jeshi la Magereza.

Alisema eneo hilo lipo kwenye Kijiji cha Gidagamowd, Kata ya Mogitu wilayani Hanang ambalo ni umbali wa kilomita 4.5 kutoka barabara kuu ya Babati- Singida.

“Serikali mpaka sasa imesafisha eneo hilo na imepima viwanja 269 ambapo kati ya hivyo, 226 vya makazi pekee, 26 makazi na biashara, 17 eneo la huduma za kijamii kama zahanati, eneo la kuzikia, kiwanja cha michezo, eneo la wazi, majengo ya ibada viwanja vitatu, ofisi ya kitongoji moja, soko moja na shule ya msingi moja,” alisema Matinyi.